Aya 47 – 50: Elimu Ya Saa Inarudishwa Kwake
Maana
Ilimu ya Saa (ya Kiyama) inarudishwa kwake (Mwenyezi Mungu.)
Hakuna yoyote anayejua Kiyama kitakuwa lini isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake. Katika Nahjul-balagha imesemwa: ”Nyinyi na Kiyama kimewatia kamba” Yaani mnacho. Mwenye kufa ndio kiyama chake kimeanza.
Na matunda hayatoki katika mafumba yake, wala mwanamke hachukui mimba, wala hazai, ila kwa kujua kwake.1
Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:59).
Na siku atakayowaita, akawaambia: Wako wapi washirika wangu? Hapo watasema: Hapana miongoni mwetu anayeshuhudia.
Kesho Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atawaambia washirikina kwa kuwatahayariza: Wako wapi wale mliokuwa mkiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu? Je, watawasaidia? Nao watamwambia Mwenyezi Mungu, hakuna yeyote miongoni mwetu mwenye ushahidi leo, kuwa wewe una mshirika.
Na wakawapotea wale waliokuwa wakiwaomba hapo mwanzo.
Siku ya Kiyama mtu hatapata sanamu, wala mali, mtoto, mbinu wala wasila au chochote kile isipokuwa hisabu na malipo ya matendo waliyoyatenda.
Na wakaona kuwa hawana pa kukimbilia.
Kesho vifuniko vitawafanukia wakosefu na watajua kuwa hakuna kwa kuikimbia adhabu.
Mwanaadamu hachoki kuomba kheri, na inapomgusa shari, mara huvunjika moyo akakata tamaa.
Mtu huwa anataka sana kupata mali, cheo, afya na amani; anakuwa na bidii ya kuyafikia hayo bila ya kuchoka. Lakini likimsibu jambo lolote katika dunia yake basi anavunjika nguvu na kukata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu.
Na tukimwonjesha rehema itokayo kwetu baada ya kumgusa dhara, bila ya shaka husema: hii ni yangu.
Anatafuta dunia kwa bidii na anakata tamaa akikosa kitu chochote kwenye hiyo dunia. Kama Mwenyezi Mungu akimwokoa na misukosuko husema: Nimeokoka kwa nguvu zangu na uwezo wangu wala hakuna yeyote aliyenifadhili.
Hakuna mwenye kusalimika na ghururi hii isipokuwa mtu wa haki na mwenye akili salama.
Wala sidhani kuwa Kiyama kitakuwa. Na hata nikirudishwa kwa Mola wangu bila ya shaka nina mema yangu kwake!
Bado mazungumzo ya mjinga aliyeghurika yanaendelea. Maana yake ni kuwa anasema mpumbavu huyu, kuwa mimi ndiye niliyefanya katika maisha ya dunia. Ama yale wanayonihofisha nayo ya baada ya mauti hayo ni njozi tu; na hata ikiwa ni kweli basi mimi huko Akhera nitakuwa na riziki bora zaidi kwa sababu mimi ni katika watu watukufu.
Mjinga huyu hata kama hana dhambi isipokuwa ufedhuli huu tu, unamtosha kuwa ni dhambi. Umetangulia mfano wake kwa upana zaidi katika Juz. 15 (18:32 – 44).
Basi kwa yakini tutawaelezea wale ambao wamekufuru walioyoyatenda, na kwa yakini tutawaonjesha adhabu ngumu.
Hakuna ovu lolote analolitenda mtu ila atalikuta kesho kwa Mwenyezi Mungu na kuulizwa nalo, kisha aadhibiwe kwalo kwa kiasi anachostahiki. Ikiwa ni katika aina ya madhambi makubwa, kama kufuru ushirikina na dhulma, basi atapata adhabu kubwa.
Na likiwa ni chini ya hapo atapata adhabu hafifu, lakini ieleweke kuwa kila balaa lisilokuwa moto wa Akhera basi si chochote.
وَإِذَا أَنْعَمْنَا عَلَى الْإِنْسَانِ أَعْرَضَ وَنَأَىٰ بِجَانِبِهِ وَإِذَا مَسَّهُ الشَّرُّ فَذُو دُعَاءٍ عَرِيضٍ {51}
قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ كَانَ مِنْ عِنْدِ اللَّهِ ثُمَّ كَفَرْتُمْ بِهِ مَنْ أَضَلُّ مِمَّنْ هُوَ فِي شِقَاقٍ بَعِيدٍ {52}
سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنْفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ ۗ أَوَلَمْ يَكْفِ بِرَبِّكَ أَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ {53}
أَلَا إِنَّهُمْ فِي مِرْيَةٍ مِنْ لِقَاءِ رَبِّهِمْ ۗ أَلَا إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ مُحِيطٌ {54}
- 1. Mwisho wa utafiti wa kitiba (mnamo mwaka 1970) umefikia kuweza kujua aina ya mtoto aliye tumboni kuwa ni wa kiume au kike kuanzia mwezi wa tatu wa mimba. Tazama Juz. 21 (31:34)