Tutawaonyesha Ishara Zetu Aya 51 – 54
Maana
Na tukimneemesha mwanadamu hugeuka na kujitenga upande, na inapomgusa shari, huwa na madua marefu marefu.
Akiwa amejitosha anakuwa makini, lakini akiwa fukara anakata tamaa na kuwa mnyonge; kama alivyosema Imam Ali (a.s.). Umetangulia mfano wake katika Juz. 11 (10:12), Juz. 12 (11:9) na Juz. 15 (17:83).
Sema: Mnaonaje! Ikiwa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, kisha mkayakataa, ni nani aliyepotea zaidi kuliko aliye katika upinzani wa mbali?
Wanaambiwa walioikadhibisha Qur’an. Upinzani wa mbali ni inadi. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimwamrisha Mtume wake mtukufu kuwaambia kuwa mnadai Qur’an ni vigano, hebu niambieni itakuwaje hali yenu ikiwa Qur’an ni haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hali nyinyi mnaipinga kwa inadi na kiburi? Je, hamjihurumii na mkajitoa shakani na adhabu ya moto?
Ulimwengu Ni Qur’an Kubwa Ya Mwenyezi Mungu
Tutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) analeta dalili kwa waja wake ili awakinaishe kuwa yeye yuko na dini yake ni sahihi na mitume na vitabu vyake ni vya kweli. Amewawekea dalili ya hilo kwa hisia na ushahidi kutoka kwao wenyewe na kwenye ulimwengu wa dhahiri ya macho; anazifunua dalili hizo na anazitanabahisha akili kwa muumba wa mbingu na ardhi, kutofautiana mchana na usiku, kuvuma pepo na mawingu, kuhuishwa ardhi baada ya kufa harakati za nyota na manufaa yake, kuumbwa katika uzuri wa sura na mengineyo anayoyatambua mtu ambayo hisia zake zinafahamisha kuweko Mwenyezi Mungu kwa dalili mkataa na kwamba Yeye ndiye muumba wa pekee wa kila kitu.
Ikiwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametegema dalili za hisia kuwakinaisha waja wake na kuwaambia:
اعْتَبِرُوا يَا أُولِي الْأَبْصَارِ {2}
“Je, hawapati busara.” (32:15).
Sasa inakuwje kusemwa kuwa dini ni ya ghaibu ndani ya ughaibu, haitegemei hisia wala majaribio?
Hapana! Dini inathibitika kwa hisia na ushahidi; sawa na tunavyothibitisha akili ya mwenye akili kutokana na kauli yake na vitendo vyake. Wataalamu wa kisayansi wanathibitisha mambo mengi yasiyohisiwa wala kuonekana.
Kwa hiyo yanatubainikia makosa ya mwanafasihi mmoja aliyesema: “Mwenyezi Mungu daima anawatakabalia wale ambao wanaamini ghaibu bila ya kuwa na haja ya dalili wala kuona” Jarida la Sabahul-khayr la 26-2-1970.
Zaidi ya hayo maulamaa wa kiislamu wamekongamana kuwa ni wajibu kuchunguza na kumjua Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumwamini. Wametegema hukumu ya kiakili na Aya za Qur’an katika hilo. Lakini anayoyasema mwanafasihi huyo ni kinyume na yanagongana na tafsiri ya Qur’an.
Ibn Al-Arabi anasema katika Futuhatil-makkiyya: “Wewe huwezi kuyakana unayoyaona; kama ambavyo huwezi kuacha kuyajua unayoyajua. Wewe unaona na kujua kwa uhakika kuweko herufi, matamshi sura na Aya zinazotamka kuweko mwandishi wake ambaye ni Mwenyezi Mungu, hata kama humuoni.
Kwa hiyo kuweko Mwenyezi Mungu ni Qur’an ambayo haifikiwi na upotofu mbele yake wala nyuma yake. Tazama Juz. 7 (6:4-6), kifungu cha ‘Hakuna udikteta Ardhini wala mbinguni.’
Je! Haikutoshi Mola wako kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kusema kuwa yeye anasimamisha dalilili kwa waja wake katika mbingu na ardhi na katika nafsi zao kuwa Mwenyezi Mungu ni kweli, Qur’an ni kweli na utume wa Muhammad ni kweli, sasa anasema kuwa inatosha kuwa dalili zake ni ushahidi wa ukweli na uadilifu wa hilo. Sufi wanasema kuhusu maana ya Aya hii kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anayeshuhudia na kufahamisha kupatikana kingine, lakini Yeye haihitajii shahidi mwingine wa kumjulisha kuwa yuko.
Ehe! Hakika wao wamo katika shaka ya kukutana na Mola wao!
Wao wameikadhibisha Qur’an kwa vile tu wao hawaamini ghaibu na malipo. Hii inafahamisha kwamba asiyeamini kukutana na Mwenyezi Mungu, basi hawezi kuongoka kwenye kheri.
Ehe! Hakika Yeye amekizunguka kila kitu.
Anajua dhahiri ya waja na undani wao na atamlipa kila mmoja kwa yaliyochumwa na mikono yake. Ikiwa kheri basi ni kheri na ikiwa shari basi ni shari. Kwa ajili hii ndio atawaadhibu wale ambao wamekana kukutana naye na wakakadhibisha kitabu chake, yakiwa ni malipo kwa yale waliyoyachuma.