Aya 15 – 18: Kuwa Na Msimamo Kama Ulivyoamrishwa
Maana
Basi kwa hiyo waite! Nawe simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa,
‘Hiyo’ ni hiyo dini. Maana ni kuwa ewe Muhammad! Lingania kwenye dini safi aliyowausia Mwenyezi Mungu (s.w.t.) mitume wote; na uwe imara kwenye hiyo dini na kwenye mwito wake. Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 12 (11:113). Huko tumezungumzia kusimama na sawa sawa (msimamo) na mafungu yake.
Wala usifuate matamanio yao.
Nabii ni maasumu anafuata anayopewa wahyi, wala hafuati matamanio ya wengine. Mara nyingi tumesema kuwa kukataza kitu hakufahamishi kuwa kinaweza kutokea kwa anayekatazwa, na kwamba aliye juu anaweza kumkataza yeyote anachotaka. Jumla hii Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 6 (5:48).
Na sema: Naamini aliyoteremsha Mwenyezi Mungu katika Kitabu. Na nimeamrishwa nifanye uadilifu baina yenu. Mwenyezi Mungu ni Mola wetu, na Mola wenu. Vitendo vyetu ni kwa ajili yenu, na vitendo vyenu ni kwa ajili yenu. Hapana ugomvi baina yetu na yenu. Na Mwenyezi Mungu atatukusanya pamoja, na marejeo ni kwake.
Ewe Muhammad! Tangaza imani yako kwa watu katika vitabu vyote alivyoviteremsha Mwenyezi Mungu kwa vyovyote iwavyo; na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mola wa wote. Wewe unahukumu kwa uadilifu ukichunga haki ya mdhulumiwa kutoka kwa dhalimu, unachukua kisasi cha mnyonge kutoka kwa dhaifu hata kama ni ndugu. Vile vile utangaze kwamba kila mtu ana majukumu ya matendo yake mbele ya Mwenyezi Mungu yeye peke yake, huna ugomvi na mtu yeyote na kwamba marejeo ni kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu ailipe kila nafsi ilichokichuma.
Kwa njia hii iliyo sawa na mantiki yaliyo salama, utaweza kusimamisha hoja kwa maadui zako na hawatabaki na vijisababu vyovyote.
Na wanaohojiana juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kukubaliwa. Hoja zao ni batili mbele ya Mola wao, na juu yao ipo ghadhabu, na itakuwa kwao adhabu kali.
Watu wa Kitabu walikuwa wakibishana na waislamu na wakijaribu kuwatoa kwenye dini yao baada ya Mwenyezi Mungu kuwaongoza kwenye Uislamu. Kuna mapokezi katika Tafsir At-Tabari kwamba mayahudi na wanaswara walikuwa wakiwaambia waislmu: “Kitabu chetu kimekuja kabla ya chenu na Mtume wetu ni kabla ya wenu, kwa hiyo sisi ni bora kuliko nyinyi.”
Haya si mageni katika ubishi wa maadui wa haki na dini, lakini hoja yao ni batili, kwa sababu ubora unakuwa kwa matendo sio kwa wakati na kutangulia; vinginevyo angelikuwa ibilisi ni bora kuliko Adam (a.s.), kwa vile amemtangulia.
Vyovyote iwavyo, mwisho wa ubishi wa batili ni maangamivu na hasara dunini na Akhera.
Mwenyezi Mungu ndiye aliyeteremsha Kitabu kwa Haki na Mizani
Makusudio ya Kitabu ni Qur’an na mizani ni uadilifu. Maana ni kuwa kushuka kwake ni haki, kila kilichomo ndani yake ni haki na inakubali kila lilio haki. Maana ya kushuka kwake kwa uadilifu ni kuwa inahukumu baina ya watu kwa uadilifu. Uadilifu unahitaji pande mbele kinyume cha haki; yaani haki ni kwa ujumla. Kwa hiyo kila uadilifu ni haki, lakini sio kila haki ni uadilifu. Jua ni haki liko, lakini sio uadlifu.
Na nini kitakujulisha pengine Saa ya Kiyama ipo karibu.
Hili ni jawabu la kauli ya wanaofanya stihizai wakiuliza: Kiyama kitakuwa lini? Kuhusu ukaribu wake ni kuwa kila kinachokuja kiko karibu na mwenye kufa kiyama chake kimeanza.
Wasioamini huihimiza hiyo Saa ifike upesi kwa stihzai.
Mara ngapi anayehimiza jambo likimfika hutamani angelikuwa mbali nalo kwa umbali wa mashariki na magharibi.
Lakini wanaoamini wanaiogopa, na wanajua kwamba hakika hiyo ni kweli.
Ndio! Kwa sababu wanaijua hakika yake kama vile wamekiona, ndio maana wakakihofia. Miongoni mwa aliyoyasema Imam Ali (a.s.) kuhusiana nacho ni: “Hofu imewachoma kama mshale.
Mtu akiwaangalia anawadhania ni wagonjwa, lakini jamaa hawana ugonjwa wowote. Wanasema: wamechanganyikiwa! Ndio kuna jambo kubwa limewafanya wachanganyikiwe.”
Kuna mshairi mmoja alitunga kuhusiana na maana haya: ref nguzo pg 518. Wanaambiwa ni wagonjwa wala sivyo, Au wamechanganyikiwa kamwe sivyo, Hofu imekuwa sawa na matarajio, Si kikomo cha hofu wala matamanio,
Ehe! Hakika hao wanaobishana katika hiyo Saa wamo katika upotofu wa mbali kabisa.
Upotevu wa mbali ni kuzama kabisa kwenye upotevu, kwa sababu wanakanusha ufufuo wa mwisho na hali wao wameona ufufuo wa kwanza.
اللَّهُ لَطِيفٌ بِعِبَادِهِ يَرْزُقُ مَنْ يَشَاءُ ۖ وَهُوَ الْقَوِيُّ الْعَزِيزُ {19}
مَنْ كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الْآخِرَةِ نَزِدْ لَهُ فِي حَرْثِهِ ۖ وَمَنْ كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ نَصِيبٍ {20}
أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُمْ مِنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَنْ بِهِ اللَّهُ ۚ وَلَوْلَا كَلِمَةُ الْفَصْلِ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ ۗ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ {21}
تَرَى الظَّالِمِينَ مُشْفِقِينَ مِمَّا كَسَبُوا وَهُوَ وَاقِعٌ بِهِمْ ۗ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فِي رَوْضَاتِ الْجَنَّاتِ ۖ لَهُمْ مَا يَشَاءُونَ عِنْدَ رَبِّهِمْ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ {22}