read

Aya 23 – 26: Ni Nani Hao Ndugu?

Maana

Hayo ndiyo aliyowabashiria Mwenyezi Mungu waja wake walioamini na wakatenda mema.

‘Hayo’ ni hayo ya fadhila kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amewaandalia wenye takua huko Akhera. Ameyaeleza kwenye kitabu kuwa ni bishara ili nyoyo zao zitulie.

Sema: Kwa haya siwaombi malipo yoyote kwenu isipokuwa mapenzi katika ndugu.
Katika tafsiri ya Al-Bahrul-muhit ya Abu Hayan Al-Andalusi na Ruhul-bayani ya Ismail Haqqi, kuna maelezo haya: “Iliposhuka Aya hii, Mtume (s.a.w.) aliulizwa: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: ni kina nani hao ndugu zako tuliowajibishiwa kuwapenda? Akasema: Ali, Fatima, Hasan na Husein.”

Ibn Al-arabi anasema katika Futuhati, kwa anuani ya ‘La takhunullah war-rasul’ (msimfanyie hiyana Mwenyezi Mungu na Mtume): “Mtume wa Mwenyezi Mungu ametutaka tuwapende akraba wake na watu wa nyumba yake (Ahlbayt) na yeye pia anaingia, kwa vile pendo la Ahlu Bayt haligawanyiki.

Kwa sababu mwenye kuwafanyia hiyana watu wa nyumba ya Mtume ndio amemfanyia hiyana Mtume. Na haishii hapo, kwa sababu mwenye kumfanyia hiyana Mtume wa Mwenyezi Mungu ndio amemfanyia hiyana Mwenyezi Mungu.”

Baadhi ya wafasiri wamenukuu riwaya katika mategemezi yake Muawiya kuwa maana ya Aya hii ni, sema ewe Muhammad kuwaambia makuraishi kuwa msiniudhi na ndugu zangu.

Katika Tafsir Gharaibul-Furqani ya Nidhamuddin Al-Hasan bin Muhammad An-naysaburi, amesema: “Imepokewa kwa Sai’d bin Jubayr, kuwa iliposhuka Aya hii walisema: Ni nani hao ambao Mwenyezi Mungu amewajibisha kuwapenda? Akasema: Ali, Fatima na watoto wao wawili. Hapana shaka kwamba hii ni fahari kubwa na utukufu uliokamilika.

Hiyo inatiliwa nguvu na riwaya kuwa Ali siku moja alimshtakia Mtume husuda ya watu kwake. Mtume akamwambia: “Kwani huridhii kuwa wane wa wane! Wa kwanza atakayeingia Peponi ni mimi na wewe na Hasan na Husein, na wake wetu wakiwa kuumeni kwetu na kushotoni kwetu na dhuria wetu wakiwa nyuma ya wake wetu.”

Imepokewa kutoka kwa Mtume amesema: “Pepo imeharamishiwa mwenye kuwadhulumu watu wa nyumba yangu na akaniudhi kwa kizazi changu.” Na alikuwa akisema: “Fatima ni sehemu yangu linaniudhi lile linalomuudhi.”Imethibiti kwa nukuu mutawatir kwamba yeye alikuwa akimpenda Ali, Hasan na Hussein na akatuwajibishia kuwapenda.

Ni utukufu kwa watu wa Mtume kuishilizwa tashahhud kwa kutajwa wao na kuswalia katika kila swala. Na akasema: mfano wa watu wa nyumba yangu ni kama Safina ya Nuh, mwenye kuipanda aliokoka na aliyeiacha aliangamia.” Mwisho wa kunukuu.

Na anayefanya wema tutamzidishia wema.

Mfano wake ni:

مَنْ جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ {160}

“Mwenye kufanya vizuri atalipwa mfano wake mara kumi.” Juz. 8 (6:160).

Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira Mwingi wa shukrani; yaani anawapa thawabu wenye kushukuru. Au wanasema: Amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo? Mwenyezi Mungu akipenda atapiga muhuri juu ya moyo wako.

Wazushi wanasema kuwa wewe Muhammad unamzulia Mwenyezi Mungu kwa kudai kwako utume na hawajui kwamba Mwenyezi Mungu amekuhifadhi na makosa na hatia. Na hata kama ungejaribu – kukisia muhali sio muhali – basi Mwenyezi Mungu angelipiga muhuri moyo wako na kukuzuia kwa nguvu.

Na Mwenyezi Mungu anaifuta batili na anaithibitisha Haki kwa maneno yake.

Wewe Muhammad uko kwenye haki na maadui zako wako kwenye ubatilifu; na Mwenyezi Mungu ataiondoa batili na ataithibitisha haki kwa dalili na ubainifu ulio wazi aliokuunga mkono nao Mwenyezi Mungu na kulifanya neno lako liko juu na neno la maadui wako liko chini pamoja na wingi wao na wanavyokuduilia wewe na Uislamu.
Hakika Yeye anayajua yaliyomo vifuani.

Anayajua yanayofichwa na nyoyo zilizo vifuani na atawalipa wenye nyoyo hizo wanayostahiki iwe ni thawabu au adhabu.

Naye ndiye anayepokea toba kwa waja wake, na anasamehe makosa.

Mwenye kufanya dhambi kisha akatubia, Mwenyezi Mungu humkubalia toba yake na humsamehe dhambi yake isipokuwa haki ya watu.

Vile vile akiwa na mema yaliyo sawa na maovu, yasiyohusika na haki za watu, basi Mwenyezi Mungu humsamehe maovu yote na kubakia kama mtu ambaye hakufanya wema wala uovu. Ikiwa mema yatayazidi maovu basi atabakiwa na yale yaliyozidi.

Haya yanasadikishwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ۚ ذَٰلِكَ ذِكْرَىٰ لِلذَّاكِرِينَ {114}

“Hakika mema huondoa maovu. Hiyo ni ukumbusho kwa wanaokumbuka.” Juz. 12 (11:114)

Pia kauli yake:

وَآخَرُونَ اعْتَرَفُوا بِذُنُوبِهِمْ خَلَطُوا عَمَلًا صَالِحًا وَآخَرَ سَيِّئًا عَسَى اللَّهُ أَنْ يَتُوبَ عَلَيْهِمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِيمٌ {102}

“Na wengine wamekiri dhambi zao; wakachanganya vitendo vyema na vingine viovu. Huenda Mwenyezi Mungu akapokea toba zao.” Juz.11(9:102).

Na anayajua mnayoyatenda katika mema na maovu.

Ambaye mizani yake ya maovu itakuwa nzito atakuwa miongoni mwa waliohasirika na ambaye mizani yake ya wema itakuwa nzito basi atakuwa miongoni mwa wenye kufaulu.

Na anawaitikia walioamini na wakatenda mema, na anawazidishia fadhila zake. Na makafiri watakuwa na adhabu kali.

Yaani waumini wanasikia mwito wa Mwenyezi Mungu na kuuitikia, kwa hiyo naye anawalipa kutokana na kuitkia kwao na utiifu na anawazidishia ziada nyingi kutokana na fadhila zake. Na wakosefu hawataki mwito wa Mwenyezi Mungu, kwa hiyo anawadhibu adhabu kubwa kutokana na upinzani wao na uasi.

وَلَوْ بَسَطَ اللَّهُ الرِّزْقَ لِعِبَادِهِ لَبَغَوْا فِي الْأَرْضِ وَلَٰكِنْ يُنَزِّلُ بِقَدَرٍ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ بِعِبَادِهِ خَبِيرٌ بَصِيرٌ {27}

Na lau Mwenyezi Mungu angeliwakunjulia riziki waja wake basi bila ya shaka wangeliasi katika dunia, lakini anaiteremsha kwa kipimo akitakacho. Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye habari, Mwenye kuona.

وَهُوَ الَّذِي يُنَزِّلُ الْغَيْثَ مِنْ بَعْدِ مَا قَنَطُوا وَيَنْشُرُ رَحْمَتَهُ ۚ وَهُوَ الْوَلِيُّ الْحَمِيدُ {28}

Naye ndiye anayeiteremsha mvua baada ya wao kukata tamaa, na hueneza rehema yake. Naye ndiye Walii Mwenye kuhimidiwa.

وَمِنْ آيَاتِهِ خَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَثَّ فِيهِمَا مِنْ دَابَّةٍ ۚ وَهُوَ عَلَىٰ جَمْعِهِمْ إِذَا يَشَاءُ قَدِيرٌ {29}

Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na wanyama aliowaeneza humo. Naye ni Mwenye uweza wa kuwakusanya apendapo.

وَمَا أَصَابَكُمْ مِنْ مُصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَنْ كَثِيرٍ {30}

Na misiba inayowasibu ni kwa sababu ya yaliyotendwa na mikono yenu. Naye anasamehe mengi.

وَمَا أَنْتُمْ بِمُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ ۖ وَمَا لَكُمْ مِنْ دُونِ اللَّهِ مِنْ وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ {31}

Na nyinyi si wenye kushinda ardhini wala mbinguni. Na hamna walii wala msaidizi isipokuwa Mwenyezi Mungu.

وَمِنْ آيَاتِهِ الْجَوَارِ فِي الْبَحْرِ كَالْأَعْلَامِ {32}

Na katika Ishara zake ni vyombo baharini kama vilima.

إِنْ يَشَأْ يُسْكِنِ الرِّيحَ فَيَظْلَلْنَ رَوَاكِدَ عَلَىٰ ظَهْرِهِ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ {33}

Akitaka, huutuliza upepo navyo husimama tutwe juu ya bahari. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.

أَوْ يُوبِقْهُنَّ بِمَا كَسَبُوا وَيَعْفُ عَنْ كَثِيرٍ {34}

Au huviangamiza hivyo vyombo kwa sababu ya waliyoyatenda. Naye husamehe mengi.

وَيَعْلَمَ الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِنَا مَا لَهُمْ مِنْ مَحِيصٍ {35}

Na ili wajue wale wanaojadiliana katika Ishara zetu kwamba hawana pahala pa kukimbilia.