read

Aya 27 – 35: Riziki Ni Kwa Kufanya Kazi Sio Kwa Dua

Maana

Na lau Mwenyezi Mungu angeliwakunjulia riziki waja wake basi bila ya shaka wangeliasi katika dunia.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameitegemeza riziki kwa waja wake kwa kuchuma kwao na kufanya kazi si kwa matakwa yao na matamanio; vinginevyo ingelienea vurugu na kufanya ufisadi katika ardhi.

Lakini anaiteremsha kwa kipimo akitakacho.

Yaani anamrukuzu kwa kadiri ya utendaji wake wa kazi. Mara nyingine Mwenyezi Mungu hutoa riziki nyingi kwa kazi chache au riziki chache kwa kazi nyingi kulingana na hekima anayoijua Yeye zaidi. Ama utajiri unaotokana na haramu; kama vile kughushi na kupora, hiyo ni riziki ya shetani sio ya kutokana na kutoa kwa Mwingi wa rehema; vipi isiwe hivyo na hali mwenye riziki hiyo amepewa kiaga cha adhabu chungu?

Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye habari, Mwenye kuona.

Anamjua anayeishi kwa hisabu ya kupora na anayeishi kwa jasho lake. Wa kwanza amemwahidi hizaya na adhabu na wa pili ni heshima na thawabu.

Naye ndiye anayeiteremsha mvua baada ya wao kukata tamaa, na hueneza rehema yake.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja riziki, anasema kuwa sababu za hizo riziki, kama vile mvua, ziko mikononi mwake. Huipeleka anapotaka na huizuia anapotaka. Basi ikichelewa kidogo, wao hukata tamaa, lakini anawawahi kwa rehema yake iliyoenea katika kila kitu.

Naye ndiye Walii anayewasimamia waja wake kwa wema Mwenye kuhimidiwa anyestahiki sifa njema na kushukuriwa. Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na wanyama aliowaeneza humo.

Makusudio ya mbingu ni kilicho juu, iwe sayari au anga; na makusudio ya wanyama hapa ni kila mwenye uhai wakiwemo malaika ndege au yoyote mwenye uhai anayeishi nchi kavu au baharini na kwenye anga au kwenye nyota. Wote hao wanaonyesha kuweko mtengenezaji wake na mtia sura wake. Naye ni Mwenye uweza wa kuwakusanya apendapo; sawa na alivyoweza kuwaumba na kuwaeneza mbinguni na ardhini.

Na misiba inayowasibu ni kwa sababu ya yaliyotendwa na mikono yenu.

Aya hii inafahamisha waziwazi, wala haikubali taawili yoyote, kuwa dhulma na ufukara unatokana na watu sio Mwenyezi Mungu na wala hautokani na hukumu ya Mwenyezi Mungu na sharia yake; hata kahati na kuzuilika mvua, sababu yake ni dhulma na ufisadi; kama ilivyoelezwa katika Hadith na katika kitabu cha Mwenyezi Mungu: “Lau wangelisimamisha Tawrat na Injil na yale yaliyoteremshwa kwao kutoka kwa Mola wao, kwa hakika wangelikula vya juu yao na vya chini ya miguu yao. ‘Juz. 6 (5:66), kifungu cha ‘Riziki na ufisadi’

Naye anasamehe mengi katika madhambi isipokuwa shirki na dhulma, kwa sababu Yeye ndiye aliyesema:

إِنَّ اللَّهَ لَا يَغْفِرُ أَنْ يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَنْ يَشَاءُ ۚ {48}

“Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kufanyiwa mshirika, lakini husamehe yasiyokuwa hayo.” Juz. 5 (4:48).

Na akasema:

يَوْمَ لَا يَنْفَعُ الظَّالِمِينَ مَعْذِرَتُهُمْ ۖ وَلَهُمُ اللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوءُ الدَّارِ {52}

“Siku ambayo hautawafaa madhaalimu udhuru wao, nao watapata laana, na watapata makazi mabaya kabisa.” Juz. 24 (40:52)

Na nyinyi si wenye kushinda ardhini wala mbinguni. Na hamna walii wala msaidizi isipokuwa Mwenyezi Mungu.

Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 20 (29:22)

Na katika Ishara zake ni vyombo baharini kama vilima.

Ikiwa jahazi limetengenezwa na mtu lakini maji linayoyapitia na upepo unaolisukuma ni katika matengenezo yake Mwenyezi Mungu na hata miti iliyotengenezewa nk. Pia ndege zinazopaa kwenye anga ya Mwenyezi Mungu, magari yanayotembea kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu na vingenevyo hata mtu mwenyewe pia. Vyote hivyo vinadhihirisha uweza wake Mwenyezi Mungu Mtukufu na rehema zake.

Akitaka, huutuliza upepo navyo hivyo vyombo husimama tutwe juu ya bahari.

Akizuia upepo au akiyagandisha maji basi majahazi yatasimama tu.

Hakika katika hayo zipo Ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.

Mwenye kuwa na subira ya tafakuri na kuutazama ulimwengu na maajabu ya siri zake, hana budi kuishia kwenye imani ya Mwenyezi Mungu na utukufu wake, na atamshukuru kwa fadhila zake na mwongozo wake.

Au huviangamiza hivyo vyombo kwa sababu ya waliyoyatenda hao watu. Naye husamehe mengi; yaani hawaharakishi pamoja na dhambi zao nyingi.
Na ili wajue wale wanaojadiliana katika Ishara zetu kwamba hawana pahala pa kukimbilia.

Wanaojadiliana katika ishara za Mwenyezi Mungu ni wale wanaosema kuwa hakuna kitu kinachofahamisha kuwa Mwenyezi Mungu yuko. Maana ni kuwa makafiri hawamuamini Mwenyezi Mungu na kupinga kila dalili inayotamka kuweko kwake.

Hata hivyo iko njia moja ya kuamini na kukiri kwao ambayo ni kuona maangamizi kwa macho yao na kujua kuwa hakuna pa kukimbilia; mfano jahazi likisimama baharini au upepo mkali. Kwa maneno mengine hawaamini mpaka waone adhabu.

فَمَا أُوتِيتُمْ مِنْ شَيْءٍ فَمَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَمَا عِنْدَ اللَّهِ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ لِلَّذِينَ آمَنُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ {36}

Basi vyote mlivyopewa ni starehe ya maisha ya dunia tu, lakini kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora, na cha kudumu zaidi. Kwa ajili ya walioamini na wakawa wanamtegemea Mola wao.

وَالَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ وَإِذَا مَا غَضِبُوا هُمْ يَغْفِرُونَ {37}

Na wanayaepuka madhambi makubwa na mambo machafu na wanapokasirika wao husamehe.

وَالَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَمْرُهُمْ شُورَىٰ بَيْنَهُمْ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنْفِقُونَ {38}

Na wanaomwitikia Mola wao na wakasimamisha Swala. Na mambo yao ni kwa kushauriana baina yao na wanatoa katika yale tuliyowapa.

وَالَّذِينَ إِذَا أَصَابَهُمُ الْبَغْيُ هُمْ يَنْتَصِرُونَ {39}

Na ambao wanapofanyiwa jeuri hujitetea.

وَجَزَاءُ سَيِّئَةٍ سَيِّئَةٌ مِثْلُهَا ۖ فَمَنْ عَفَا وَأَصْلَحَ فَأَجْرُهُ عَلَى اللَّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ {40}

Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo. Lakini mwenye kusamehe na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu.

وَلَمَنِ انْتَصَرَ بَعْدَ ظُلْمِهِ فَأُولَٰئِكَ مَا عَلَيْهِمْ مِنْ سَبِيلٍ {41}

Na wanaojitetea baada ya kudhulumiwa, hao hapana njia ya kuwalaumu.

إِنَّمَا السَّبِيلُ عَلَى الَّذِينَ يَظْلِمُونَ النَّاسَ وَيَبْغُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ ۚ أُولَٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ {42}

Bali njia ya lawama ipo kwa wale wanaowadhulumu watu, na wanafanya jeuri katika ardhi bila ya haki. Hao watapata adhabu iliyo chungu.

وَلَمَنْ صَبَرَ وَغَفَرَ إِنَّ ذَٰلِكَ لَمِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ {43}

Na anayesubiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.