read

Aya 36 – 43: Kilichoko Kwa Mwenyezi Ni Bora Na Kitabakia

Maana

Basi vyote mlivyopewa ni starehe ya maisha ya dunia tu,

Starehe za dunia ni kila kinachostarehesha katika maisha haya; kama vile afya cheo, mali, wanawake, watoto, majengo, samani na mengineyo. Anasa za dunia hata zikiwa nyingi, zinaondoka na kuisha. Ama neema za Akhera zinabaki kwa kubakia kwake:

مَا عِنْدَكُمْ يَنْفَدُ ۖ وَمَا عِنْدَ اللَّهِ بَاقٍ ۗ {96}

“Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu ndivyo vitakavyobakia.”
Juz.
14 (16:96).

Anaendelea kusema Mwenyezi Mungu: lakini kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora, na cha kudumu zaidi.

Kila amali itakayotekeleza haja yoyote katika maisha basi hiyo ni akiba mbele ya Mwenyezi Mungu kwa Masharti yafuatayo:-

1. Kwa ajili ya walioamini Mwenyezi Mungu. Ama wale waliomkufuru hawana chochote mbele ya Mwenyezi Mungu isipokuwa adhabu, kwa vile wao hawakiri isipokuwa kuweko kwake. Kuna Hadithi inayosema: “Mwenye kumfanyia amali asiyekuwa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atamwachia aliyemfanyia amali, na kesho ataambiwa: chukua malipo yako kwa uliyemfanyia.”

2. Na wakawa wanamtegemea Mola wao katika mambo yao yote, wala hawajienzi isipokuwa kwa kumcha Mwenyezi Mungu na radhi yake.

3. Na wanayaepuka madhambi makubwa na mambo machafu, ikiwemo dhulma, uongo na ufisadi. Tazama Juz. 5 (4:31) na Juz. 8 (6:151)

4. Na wanapokasirika wao husamehe; yaani si wepesi wa kukasirika na wasiokasirika isipokuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu.

5. Na wanaomwitikia Mola wao, hawamuasi katika amri yake wala makatazo yake.

6. Na wakasimamisha Swala. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameihusisha kuitaja hapa kwa vile ndio nguzo ya dini, na Mtume (s.a.w.) alikuwa akiita ‘kitulizo cha jicho.’ Baadhi ya wataalamu wameiita ‘Uhakika wa Mwislamu’

7. Na mambo yao ni kwa kushauriana baina yao

Kauli ‘mambo yao’ inaashiria mambo mema ya uma na kwamba wao wanasaidiana kuufanyia kazi uma. Kushauriana huku si katika halali ya Mwenyezi Mungu na haramu yake, kwa sababu zinatokana na Mwenyezi Mungu tu peke yake. Tazama Juz. 4 (3:159). Katika Nahjul-balagha amesema: “Kutaka ushauri ni jicho la mwongozo na amejiingiza kwenye hatari anayetosheka na rai yake.”

8. Na wanatoa katika yale tuliyowapa, katika mali

9. Na ambao wanapofanyiwa jeuri hujitetea.

Unaweza kuuliza: Tutaichanganya vipi Aya hii na ile isemayo: ‘Na wanapokasirika wao husamehe?’

Jibu: Kusamehe uovu ni vizuri ikiwa kutasababisha muovu kujirekebisha na kutubia au ikiwa ni kukinga ugomvi na fitina, lakini si kuzuri ikiwa kutasababisha ujeuri na usafihi kwa muasi. Imam Ali (a.s.) anasema: “Kuwatekelezea ahadi wavunja ahadi ni kuvunja ahadi mbele ya Mwenyezi Mungu na kuvunja ahadi kwa wavunja ahadi ni kutekeleza ahadi.”

Tumeelezea hayo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 24 (41:34).

Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo.

Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

فَمَنِ اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ فَاعْتَدُوا عَلَيْهِ بِمِثْلِ مَا اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ ۚ {194}

“Anayewachokoza nanyi mchokozeni kwa kadiri alivyowachokoza.” Juz.2 (2:194).

Lakini mwenye kusamehe na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu.

Mfano wake ni

وَأَنْ تَعْفُوا أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ۚ {237}

“Na kusamehe ndiko kuliko karibu zaidi na takua” Juz. 2 (2:237).

Vile vile:

فَمَنْ تَصَدَّقَ بِهِ فَهُوَ كَفَّارَةٌ لَهُ ۚ {45}

“Lakini atakayesamehe itakuwa kafara kwake.” Juz. 6 (5:45).

Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu.

Makusudio ya madhalimu hapa ni wale wanaopita mpaka wa kisasi.

Na wanaojitetea baada ya kudhulumiwa, hao hapana njia ya kuwalaumu kabisa wala hakuna kuadhibiwa, kwa sababu mwenye kuanza ndiye dhalimu, na mwenye kudhulimiwa anayo haki ya kujitetea; bali akimnyamazia aliyemdhulumu basi atakuwa ni mshirika katika dhulma, kwa sababu kumnyamazia dhalimu kunamtia mori. Na lau dhalimu atajua kuwa mdhulumiwa ataitetea heshima yake basi atajizuia.

Bali njia ya lawama ipo kwa wale wanaowadhulumu watu, na wanafanya jeuri katika ardhi bila ya haki. Hao watapata adhabu iliyo chungu.

Huko nyuma tumewahi kueleza kuwa dhalimu anahukumiwa kuwa ni kafiri mbele ya Mwenyezi Mungu, ajapotamka shahada mbili. Ndio! Hapa duniani atachukuliwa kama Mwislamu, lakini Akhera atakuwa pamoja na madhalimu. Hilo ni kwa ushahidi wa Aya kadhaa, zinazomwita kafiri kuwa ni dhalimu na dhalimu kuwa ni kafiri. Tazama Juz. 3 (2:254) na Juz. 9 (25:55-62).

Na anayesubiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa; yaani ni mambo mazuri ya kuazimiwa kufanywa. Aina bora ya subira ni kuvumilia udhia katika kuithibitisha haki na kuitangaza. Na aina bora zaidi ya kusamehe ni kule kutakakosababisha kuondoa fitina na ufisadi.

وَمَنْ يُضْلِلِ اللَّهُ فَمَا لَهُ مِنْ وَلِيٍّ مِنْ بَعْدِهِ ۗ وَتَرَى الظَّالِمِينَ لَمَّا رَأَوُا الْعَذَابَ يَقُولُونَ هَلْ إِلَىٰ مَرَدٍّ مِنْ سَبِيلٍ {44}

Na ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza, hana walii baada yake. Na utawaona madhalimu watakapoiona adhabu watasema: Je, ipo njia ya kurudi?

وَتَرَاهُمْ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا خَاشِعِينَ مِنَ الذُّلِّ يَنْظُرُونَ مِنْ طَرْفٍ خَفِيٍّ ۗ وَقَالَ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ الْخَاسِرِينَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنْفُسَهُمْ وَأَهْلِيهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ أَلَا إِنَّ الظَّالِمِينَ فِي عَذَابٍ مُقِيمٍ {45}

Na utawaona wanapelekwa kwenye Moto, nao wamenyenyekea kwa unyonge, wanatazama kwa mtazamo wa kificho. Na walioamini watasema: Hakika waliopata hasara ni hao waliohasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Ehe! Hakika wenye kudhulumu watakuwa katika adhabu ya kudumu.

وَمَا كَانَ لَهُمْ مِنْ أَوْلِيَاءَ يَنْصُرُونَهُمْ مِنْ دُونِ اللَّهِ ۗ وَمَنْ يُضْلِلِ اللَّهُ فَمَا لَهُ مِنْ سَبِيلٍ {46}

Wala hawatakuwa na walii wa kuwanusuru asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemepoteza, basi hana njia yoyote.

اسْتَجِيبُوا لِرَبِّكُمْ مِنْ قَبْلِ أَنْ يَأْتِيَ يَوْمٌ لَا مَرَدَّ لَهُ مِنَ اللَّهِ ۚ مَا لَكُمْ مِنْ مَلْجَإٍ يَوْمَئِذٍ وَمَا لَكُمْ مِنْ نَكِيرٍ {47}

Mwitikieni Mola wenu kabla haijafika siku isiyoepukika itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo hamtakuwa na pa kukimbilia wala hamtakuwa na cha kukataa.

فَإِنْ أَعْرَضُوا فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا ۖ إِنْ عَلَيْكَ إِلَّا الْبَلَاغُ ۗ وَإِنَّا إِذَا أَذَقْنَا الْإِنْسَانَ مِنَّا رَحْمَةً فَرِحَ بِهَا ۖ وَإِنْ تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ فَإِنَّ الْإِنْسَانَ كَفُورٌ {48}

Na wakipuuza, basi hatukukupeleka uwe mwenye kuwalinda. Si juu yako ila kufikisha tu. Na hakika tukimwonjesha mtu rehema kutoka kwetu, huifurahia. Na akisibiwa na ovu kwa sababu ya iliyotanguliza mikono yao, basi hakika mtu huyu anakufuru.

لِلَّهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ يَهَبُ لِمَنْ يَشَاءُ إِنَاثًا وَيَهَبُ لِمَنْ يَشَاءُ الذُّكُورَ {49}

Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; anaumba apendavyo, anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye watoto wa kiume.

أَوْ يُزَوِّجُهُمْ ذُكْرَانًا وَإِنَاثًا ۖ وَيَجْعَلُ مَنْ يَشَاءُ عَقِيمًا ۚ إِنَّهُ عَلِيمٌ قَدِيرٌ {50}

Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza.