Aya 44 – 50:Mwenye Hasara Ni Yule Aliyejihasiri Mwenyewe
Maana
Na ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza, hana walii baada yake.
Mwenye kufuata njia ya upotevu kwa uchaguzi wake mbaya, basi atakuwa ni katika wapotevu. Wala hakuna wa kumlaumu ila yeye mwenyewe. Ambaye Mwenyezi Mungu amemuhizi hawezi kupata wa kumuokoa na hizaya hii.
Na utawaona madhalimu watakapoiona adhabu watasema: Je, ipo njia ya kurudi?
Walijikuza, wakafanya kiburi na kutakabari katika maisha ya dunia, lakini watakapofufuliwa wakiwa dhalili, watanyenyekea na watatafuta njia ya kuokoka na adhabu au kurudi duniani mara nyingine.
Hivi ndivyo walivyo mataghuti, wanajikuza ikiwa hakuna nguvu ya kuwarudi na wananyewa ikiwadhihirikia dalili yake.
Na utawaona wanapelekwa kwenye Moto, nao wamenyenyekea kwa unyonge, wanatazama kwa mtazamo wa kificho.
Wataukabili moto kwa matendo yao, wataichungulia Jahannam wakiwa wanatetemeka kwa hofu kuu, na hapo mwanzo walikuwa wakiifanyia mzaha.
Na walioamini watasema: Hakika waliopata hasara ni hao waliohasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Ehe! Hakika wenye kudhulumu watakuwa katika adhabu ya kudumu.
Waumini watayasema haya watakapowaona wakosefu wakisukumwa kwenye mwisho wa matendo yao, watamshukuru Mwenyezi Mungu aliyewaokoa na hizaya hii. Umetangulia mfano wake katika Juz. 23 (39:15).
Wala hawatakuwa na walii wa kuwanusuru asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
Sharti la kwanza la walii (mlinzi) atakayeweza kusaidia, ni kuwa yeye mwenyewe awe na nguvu za kujikinga na kujisadia au kumsadia mwingine. Siku hiyo hakutakuwa na yeyote atakayekuwa na uwezo au nguvu.
Na ambaye Mwenyezi Mungu amemepoteza, basi hana njia yoyote ya kuokoka na moto.
Hapa tutaufasiri upotevu kwa maana ya moto, kwa sababu mfumo wa maneno unaishiria hilo; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Juz. 24 (40:34): “Kama hivyo Mwenyezi Mungu humpoteza yule aliyepita kiasi mwenye shaka.” Yaani anamwadhibu.
Mwitikieni Mola wenu kabla haijafika siku isiyoepukika itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo hamtakuwa na pa kukimbilia wala hamtakuwa na cha kukataa
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewakalifisha waja yale yaliyo na manufaa kwao na heri yao, akawapa uwezo wa kuyatekelza yale aliyowakalifisha, akawapa muda wa kuyatenda na kutubia na akwahadharisha na matokeo ya kupuuza na uzembe – hakumwachia yeyote hoja ya kukimbilia siku ile ambayo mtu hataweza kurudishwa kwenye maisha yake ya kwanza wala hataweza kuyakana yaliyofanywa na mikono yake.
Na wakipuuza, basi hatukukupeleka uwe mwenye kuwalinda. Si juu yako ila kufikisha tu.
Maana yako wazi. Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa; kama vile: Juz. 5 (4:80) na Juz. 7(6:107).
Na hakika tukimwonjesha mtu rehema kutoka kwetu, huifurahia. Na akisibiwa na ovu kwa sababu ya iliyotanguliza mikono yao, basi hakika mtu huyu anakufuru.
Makusudio ya rehema ni neema; kama vile afya na mali, na ovu ni balaa; kama vile ufukara na maradhi. Ama Makusudio ya mtu ni wengi katika wao sio kila mtu; vinginevyo ingelikuwa mtu hana taklifa yoyote, ikiwa ndio hivyo alivyo; kama tulivyobainisha katika Juz.13 (14:32-34).
Maana ni kuwa mjinga mwenye hasara huwa anafurahi kwa starehe za dunia akizipata na anakufuru akikosa kitu, hata kama ni kwa rai yake mbaya na matamanio ya nafsi yake. Umetangulia mfano wake katika Juz. 12 (11:9-10).
Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; anaumba apen- davyo, anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye watoto wa kiume. Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza.
Hakuna mwenye shaka kwamba mtu hana hiyari wala uweza wowote wa kupata watoto wa kike tu au wa kiume tu au mchanganyiko. Ni Mwenyezi Mungu tu ndiye mwenye uwezo wa kumpa mtu watoto wa kike, wa kiume, mchanganyiko au kumfanya asizae kabisa. Mpaka sasa bado madaktari hawajaweza kutibu utasa kwa mwanamume au kwa mwanamke. Waliloweza ni kuchukua mbegu za mwanamume mwingine, bila ya kufanyika tendo la kujamiaana, na kuzitia kwa mke wa mume tasa.
Tumeweka mlango maalum wa hilo katika kitabu chetu Al-islamu walhay-at (Uislamu na maisha) na tukatoa fatwa ya kuharamisha hilo na kwamba mtoto atakayezaliwa katika njia hiyo hawezi kuwa wa mume, kwa ijimai, na atakuwa ni wa mama.
وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَنْ يُكَلِّمَهُ اللَّهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِنْ وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا فَيُوحِيَ بِإِذْنِهِ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ عَلِيٌّ حَكِيمٌ {51}
وَكَذَٰلِكَ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ رُوحًا مِنْ أَمْرِنَا ۚ مَا كُنْتَ تَدْرِي مَا الْكِتَابُ وَلَا الْإِيمَانُ وَلَٰكِنْ جَعَلْنَاهُ نُورًا نَهْدِي بِهِ مَنْ نَشَاءُ مِنْ عِبَادِنَا ۚ وَإِنَّكَ لَتَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ {52}
صِرَاطِ اللَّهِ الَّذِي لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ أَلَا إِلَى اللَّهِ تَصِيرُ الْأُمُورُ {53}