Aya 51 – 53: Sura Ya Mawasiliano Baina Mwenyezi Mungu Na Mitume Wake
Maana
Na haikuwa kwa mwanaadamu kwamba Mwenyezi Mungu amsemeze ila kwa Wahyi, au kwa nyuma ya pazia, au kumtuma Mjumbe. Naye humletea wahyi ayatakayo kwa idhini yake. Hakika Yeye ni Mtukufu, Mwenye hikima.
Maneno ya Mwenyezi Mungu yana maana nyingi; miongoni mwayo ni haya yafuatayo:
Kadha yake na kadari yake: “Na lau si neno lilikwishatangulia kutoka kwa Mola wako.” Aya 45
Kuuumba:
إِنَّمَا الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ رَسُولُ اللَّهِ وَكَلِمَتُهُ أَلْقَاهَا إِلَىٰ مَرْيَمَ وَرُوحٌ مِنْهُ ۖ {171}
Haki:
وَكَلِمَةُ اللَّهِ هِيَ الْعُلْيَا ۗ {40}
Ulimwengu aliouleta kwa neno
كُنْ{82}
Ilhamu kama inavyoelezewa kwenye Aya hii tuliyo nayo: “kwamba Mwenyezi Mungu amsemeze ila kwa Wahyi.”
Maneno yanayosikiwa:
أَفَتَطْمَعُونَ أَنْ يُؤْمِنُوا لَكُمْ وَقَدْ كَانَ فَرِيقٌ مِنْهُمْ يَسْمَعُونَ كَلَامَ اللَّهِ ثُمَّ يُحَرِّفُونَهُ مِنْ بَعْدِ مَا عَقَلُوهُ وَهُمْ يَعْلَمُونَ {75}
Maneno haya ndiyo anayoyasikia Mtume nyuma ya pazia au kupelekewa mjumbe.
Katika Aya hii tuliyo nayo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja njia tatu za kuzungumza kwake Mwenyezi Mungu na mitume na namna ya kuwasiliana nao:
1. Kuyaingiza maana katika moyo wa Mtume moja kwa moja bila ya kuweko kati chochote. Hii ndiyo iliyokusudiwa katika kauli yake: ‘Ila kwa wahyi’
2. Kuumba Mwenyezi Mungu maneno, kama anavyoumba vitu vingine na kuyasikia mtume nyuma ya pazia; yaani bila ya kumuona mzungumzaji. Ndio makusudio ya kauli yake:
وَكَلَّمَ اللَّهُ مُوسَىٰ تَكْلِيمًا {164}
3. Kumpeleka Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Malaika kwa Mtume wake, atakayemfikishia risala ya Mola wake. Mula Sadra anasema katika Asfar: “Usije ukadhani Mtume (s.a.w.) alipokea maneno ya Mwenyezi Mungu kupitia kwa Jibril kama unavyosikia wewe kutoka kwa Mtume, au kusema kuwa Mtume (s.a.w.) alikuwa akimwiga Jibril.”
Hakuna mwenye shaka kuwa hakuna anayedhania au kusema hivi isipokuwa mjinga tu. Kwa sababu Jibril aliyomfikishia Muhammad (s.a.w.) ni maneno ya Mwenyezi Mungu hasa na Mtume (s.a.w.) akayaelewa kiuhakika wake.
Kwa hiyo basi kule kujua Mtume maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ndio maneno ya Mwenyezi Mungu, na maneno ya Mwenyezi Mungu ndio kujua Mtume.
Na hivyo ndivyo tulivyokupa roho kwa amri yetu.
Makusudio ya roho hapa ni Qur’an, kwa sababu hiyo ni uhai wa roho na mwili vile vile. Imam Ali (a.s.) anasema: “Kitabu cha Mwenyezi Mungu mnaona kwacho, mnatamka kwacho na manasikia kwacho”
Ulikuwa hujui Kitabu ni nini, wala imani.
Makusudio ya Kitabu ni Qur’an na imani ni sharia ya Mwenyezi Mungu ambayo ameibainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa Nabii wake mtukufu baada ya kumchagua Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa risala yake. Wametofautiana katika tafsiri ya Aya hii kwenye kauli ambazo Razi ameishilizia tano. Yenye nguvu zaidi – kama tuonavyo – ni kauli ya Sheikh Ismail Haqqi, katika Tafsir Ruhul-bayan, ninamnukuu:
“Makusudio ya imani ni ufafanuzi uliokuja kwenye Qur’an ambao akili hauwezi kuupata, sio ile imani ambayo inakuwa kwenye akili na maarifa. Kwa sababu uzoefu wa Mtume (s.a.w.) hauna shaka.
Wamekongamana watu wa Usul – kwenye maarifa ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake – kwamba mitume walikuwa ni waumini kabla ya wahyi, wakiwa wamehifadhika (maasumu) na madhambi makubwa na madogo ambayo yangeliweza kuwafanya watu wawakimbie kabla na baada ya utume, zaidi ya kwamba hawakuwa makafiri.”
Lakini tumeifanya hiyo Qur’an kuwa ni Nuru ambayo kwayo tunamwongoza tumtakaye katika waja wetu ambao wametafuta uongofu kwa nia safi na wakaitafuta haki kwa haki. Ama yule aliyeasi na akafanya jeuri, Mwenyezi Mungu anaachana naye:
إِنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ كَاذِبٌ كَفَّارٌ {3}
Na hakika wewe unaongoza kwenye Njia Iliyonyooka, njia ya Mwenyezi Mungu.
Nabii (s.a.w.) anatoa mwito wa Uislamu, dini ya Mwenyezi Mungu na njia yake iliyonyooka. Mwenye kufuata njia hii atakuwa amefuata njia ya wazi itakayompeleka kwa Mwenyezi Mungu na atasalimika na mwisho mbaya.
Ambaye ni vyake vilivyomo mbinguni na katika ardhi. Ehe! mambo yote yanarudi kwa Mwenyezi Mungu.
Mwito wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ndio njia ya kueleka kwa Mfalme wa ulimwengu Ambaye atawakusanya Siku isiyo na shaka. Basi mwenye kuusikiliza mwito wa Mtume na akauitikia, kesho atakuwa pamoja na wakweli na manabii.
Hao ndio marafiki wazuri. Na mwenye kuuacha, akajiweka mbali nao, atakuwa katika Jahannam na rafiki yake shetani.