read

Aya 46 – 56 :Musa

Maana:

Na hakika tulimtuma Musa kwa Ishara zetu aende kwa Firauni na waheshimiwa wake, na akasema: Hakika mimi ni Mtume wa Mola wa walimwengu wote! Lakini alipowajia na Ishara zetu wakaingia kuzicheka.

Hii ni mara ya kumi na sita kukaririka kisa cha Musa (a.s.), mbali na zile Aya alizotajwa. Tumekwishazungumzia kisa hiki, mara nyingine kwa ufafanuzi zaidi na mara nyingine kwa ujumla.

Katika Juz. 16 (20:9) tumetaja sababu za kukaririka. Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa Mwenyezi Mungu mtukufu amekirudia kisa cha Musa hapa kwa sababu vigogo wa kikuraishi walimtia ila Muhammad (s.a.w.), ndio akabainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwamba Yeye alimtuma Musa fukara kwa Firauni tajiri. Aya iliyotangulia inatilia nguvu hili.

Vyovyote iwavyo, maana ya Aya tuliyo nayo yako wazi. Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu alimtuma Musa kwa Firauni na watu wake na miujiza inayojulisha utume wake; kama vile fimbo na mkono mweupe, lakini wakamdharau yeye, mwito wake na miujiza yake.

Na hatukuwaonyesha Ishara yoyote ila hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuliko nyengineyo.

Makusudio ya ishara hapa ni adhabu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t.):

فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمُ الطُّوفَانَ وَالْجَرَادَ وَالْقُمَّلَ وَالضَّفَادِعَ وَالدَّمَ آيَاتٍ مُفَصَّلَاتٍ فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا مُجْرِمِينَ {133}

“Basi tukawapelekea tufani na nzige na chawa na vyura na damu kuwa ishara mbalimbali, lakini wakatakabari na wakawa watu wakosefu.” Juz. 9 (7:133).

Na tukawakamata kwa adhabu ili warejee kutoka kwenye upotevu kwenda kwenye uongofu na kutoka kwenye ufisadi wa nchi hadi kwenye kuitengeneza, lakini ishara na maonyo hayakuwafuaa watu wasioona ispokuwa manufaa na chumo lao tu.

Na wakasema: Ewe mchawi! Tuombee kwa Mola wako kwa ile ahadi aliyokuahidi; hakika sisi tutakuwa wenye kuongoka.

Katika Aya hii Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasimulia kuwa watu wa Firauni walimwita Musa mchawi, na katika Juz.9 (7:134) walimwita kwa jina lake. Sio mbali kuwa kuna wakati walimwambia kwa jina lake na wakati mwingine walimwambia kwa kumwita mchawi. Hili ni jambo la kawaida katika mabishano ya watu.

Basi tulipowaondolea adhabu hiyo, mara wakaingia kuvunja ahadi.

Mwenyezi Mungu aliwakamata na adhabu kwa miaka, wakamtaka Musa awaombee kuondolewa adhabu na wakamwahidi kutubia, lakini waliivunja ahadi yao na wakaendelea na kufuru na upotevu baada ya kuondokewa na adhabu.

Na Firauni alitangaza kwa watu wake, akisema: Enyi watu wangu! Kwani mimi sinao huu ufalme wa Misri, na hii mito inapita chini yangu? Je, hamwoni?

Chini yangu ni kinaya cha kuwa mito iko chini yake akiitumia vile atakavyo. Firauni anautolea dalili ukuu wake na cheo chake kwa mali na ardhi. Hii ndio hali iliyoenea kwa wengi kila wakati na kila mahali. Wenye mali hivi sasa ndio watawala kwenye nchi nyingi.

Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge, wala hawezi kusema waziwazi?

Ni mnyonge eti kwa kuwa ni fukara na kutosema waziwazi ni kwa kuwa alikuwa ana kigugumizi, lakini Mwenyezi Mungu alikiondoa kwa dalili ya kauli yake Musa kumuomba Mola wake:
“Na ulifungue fundo lililo katika ulimi wangu.” Na Mwenyezi Mungu naye akamjibu: “Hakika umepewa maombi yako ewe Musa!” Juz.16 (20:27,36). Na Firauni alimwita Musa kwa alivyokuwa si kwa alivyo.

Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu, au hawakuja Malaika pamoja naye wakamwandama?

Yaani Malaika wawe wapambe wake; kama wanavyofanya viongozi kuwa na wapambe. Wafasiri wanasema kuwa ilikuwa ni desturi ya watu wa firauni wakimchagua kiongozi wao wanamvisha vikuku na mkufu wa dhahabu, kuwa ndio alama ya uongozi wake. Ndio maana Firauni akasema, atakuwaje Musa ni nabii na hali hana dhahabu mikononi mwake wala shingoni mwake. Lililompa ujasiri wa hilo ni ujinga wa watu wake, upotevu wao na udhaifu wa akili zao; kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t.):

Basi aliwachezea watu wake, na wakamtii. Kwa hakika hao walikuwa watu mafasiki.

Mwaka uliopita nilimwita fundi wa umeme anirekebishie kwenye maktaba yangu. Basi alipoona vitabu vimetapakaa huku na huko, aliniambia: “Mke wangu ananichukia sana, nakuomba uniandikie dawa ya mapenzi.” Nikwambia mimi sijui fani hiyo. Akasema: “Kwa nini una vitabu vyote hivi?”

Walipotukasirisha kwa kumkadhibisha Mtume, kuvunja ahadi na kuendelea na ukafiri na upotevu, tuliwapatiliza tukawagharikisha wote, viongozi na wafuasi.

Kisha tukawafanya kuwa watangulizi wa motoni na mfano kwa wa baadaye, wapate funzo na mawaidha wale watakaokuja baada yao.

Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَقَوْمَ نُوحٍ لَمَّا كَذَّبُوا الرُّسُلَ أَغْرَقْنَاهُمْ وَجَعَلْنَاهُمْ لِلنَّاسِ آيَةً ۖ {37}

“Na watu wa Nuh walipowakadhibisha Mitume, tuliwagharikisha na tukawafanya ni ishara kwa watu: Juz. 19 (25:37).

وَلَمَّا ضُرِبَ ابْنُ مَرْيَمَ مَثَلًا إِذَا قَوْمُكَ مِنْهُ يَصِدُّونَ {57}

Na alipopigiwa mfano Mwana wa Maryam, watu wako waliupigia ukelele.

وَقَالُوا أَآلِهَتُنَا خَيْرٌ أَمْ هُوَ ۚ مَا ضَرَبُوهُ لَكَ إِلَّا جَدَلًا ۚ بَلْ هُمْ قَوْمٌ خَصِمُونَ {58}

Wakasema: Miungu yetu kwani ni bora au Yeye? Hawakukupigia mfano huo ila kwa ubishi tu. Bali hao ni watu wagomvi!

إِنْ هُوَ إِلَّا عَبْدٌ أَنْعَمْنَا عَلَيْهِ وَجَعَلْنَاهُ مَثَلًا لِبَنِي إِسْرَائِيلَ {59}

Hakuwa yeye Isa ila ni mja tuliyemneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili.

وَلَوْ نَشَاءُ لَجَعَلْنَا مِنْكُمْ مَلَائِكَةً فِي الْأَرْضِ يَخْلُفُونَ {60}

Na tungelipenda tungeliwafanya badala yenu Malaika katika ardhi kuwa makhalifa.

وَإِنَّهُ لَعِلْمٌ لِلسَّاعَةِ فَلَا تَمْتَرُنَّ بِهَا وَاتَّبِعُونِ ۚ هَٰذَا صِرَاطٌ مُسْتَقِيمٌ {61}

Na kwa hakika hiyo ni elimu ya Saa. Basi usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndiyo njia iliyonyooka.

وَلَا يَصُدَّنَّكُمُ الشَّيْطَانُ ۖ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُبِينٌ {62}

Wala asiwazuie Shetani. Hakika yeye ni adui yenu wa dhahiri.

وَلَمَّا جَاءَ عِيسَىٰ بِالْبَيِّنَاتِ قَالَ قَدْ جِئْتُكُمْ بِالْحِكْمَةِ وَلِأُبَيِّنَ لَكُمْ بَعْضَ الَّذِي تَخْتَلِفُونَ فِيهِ ۖ فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ {63}

Na alipokuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimewajia na hikima, na ili niwaeleze baadhi ya yale mliyokhitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnitii.

إِنَّ اللَّهَ هُوَ رَبِّي وَرَبُّكُمْ فَاعْبُدُوهُ ۚ هَٰذَا صِرَاطٌ مُسْتَقِيمٌ {64}

Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu, na Mola wenu. Basi Mwabuduni Yeye tu. Hii ndiyo njia iliyonyooka.

فَاخْتَلَفَ الْأَحْزَابُ مِنْ بَيْنِهِمْ ۖ فَوَيْلٌ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْ عَذَابِ يَوْمٍ أَلِيمٍ {65}

Lakini makundi yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao waliodhulumu kwa adhabu ya siku chungu.

هَلْ يَنْظُرُونَ إِلَّا السَّاعَةَ أَنْ تَأْتِيَهُمْ بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ {66}

Hawangoji ila Saa iwajie ghafla na hali wao hawatambui?