read

Aya 57 – 66: Alipopigiwa Mfano Mwana Wa Maryam

Maana

Na alipopigiwa mfano Mwana wa Maryam, watu wako waliupigia ukelele. Wakasema: Miungu yetu kwani ni bora au Yeye?

Anaambiwa Mtume (s.a.w.). Wafasiri wamesema kuwa aliyempigia mfano mwana wa Maryam ni Abdallah bin Ziba’ara. Aya inaashiria tukio lililotokea baina ya Mtume (s.a.w.) na makafiri wa kikuraishi; kwa ufupi ni kama ifuatavyo:

Iliposhuka Aya: “Hakika nyinyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannam mtaifikia” Juz. 17 (21:98), makuraishi waliona vibaya sana, wakamwendea Abdallah bin Ziba’ara, kabla ya kusilimu, naye akamwambia Mtume: “Manaswara wanamwabudu Masih, ikiwa Masih atakuwa katika Moto sisi tutakuwa radhi kuwa miungu yetu iko pamoja naye kwa sababu yeye ni bora kuliko hiyo au hiyo siyo bora kuliko yeye” Makuraishi waliposikia walilipuka kwa makelele ili wamnyamazishe Mtume asiweze kujibu na watu wafikirie kuwa ameshindwa kujibu.”

Mapokezi mengine yanasema kuwa Mtume (s.a.w.) alimwambia Bin Zab’ara: “Ni ujinga ulioje wako kutojua lugha ya watu wako? Hujui kuwa herufi ‘ma’ ni ya wasio na akili?” yaani ‘hayo mnayoyaabudu.’

Hawakukupigia mfano huo ila kwa ubishi tu.

Kukupinga kwako makuraishi kwa kumtolea mfano Masih sio kwa makusudio ya kuihakiksha haki na kuidhihirisha, isipokuwa ni kwa makusudio ya kuikimbia haki na kuvungavunga tu. Wao wanajua wazi kuwa makusudio ya hayo mnayoyaabudu ni masanamu yao hasa.

Bali hao ni watu wagomvi! Wanazidisha ugomvi na uhasama ili kulinda masilahi yao.

Hakuwa yeye Isa ila ni mja tuliyemneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili.

Isa ni mja katika waja wa Mwenyezi Mungu, aliyeneemeshwa kwa utume na kaumbwa bila ya baba, kama Adam, ili awe ni ishara kuwafahamisha Wana wa Israil uweza wa Mwenyezi Mungu na ukuu wake, waweze kuongoka na kuwa na takua. Lakini wao walizidi inadi na ujeuri, wakasema kuhusu Bwana Masih na mama yake mambo ambayo yanaweza kuitingisha Arshi.
Na tungelipenda tungeliwafanya badala yenu Malaika katika ardhi kuwa makhalifa.

Hili ni kemeo na karipio kwa washirikina. Maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu hana haja na nyinyi wala ibada yenu. Kama angelitaka anageliwaangamiza na mahala penu pakachukuliwa na Malaika watakomtakasa na kumsifu kwa sifa njema bila ya kumuasi na jambo lolote.

Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَإِنْ تَتَوَلَّوْا يَسْتَبْدِلْ قَوْمًا غَيْرَكُمْ ثُمَّ لَا يَكُونُوا أَمْثَالَكُمْ {38}

“Na mkigeuka atawaleta watu wengine na hawatakuwa mfano wenu.” (47:38).

Na kwa hakika hiyo ni elimu ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndiyo Njia iliyonyooka.

‘Hiyo’ ni hiyo Qur’an. Maana ni kuwa Qur’an inawaelimisha watu siku ya Kiyama na kuwapa uhakika wake na pia kuwahadharisha na vituko vyake; wala haifai kukitilia shaka. Na hii Qur’an ni njia ya Mwenyezi Mungu iliyonyooka. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

إِنَّ هَٰذَا الْقُرْآنَ يَهْدِي لِلَّتِي هِيَ أَقْوَمُ {9}

“Hakika hii Qur’an inaongoza kwenye yaliyonyooka kabisa.” 15 (17:9).

Iliyonyooka kabisa ndio hiyo njia iliyonyooka. Unaweza kuuliza: kwanini isiwe hakika huyo, yaani Isa, kwa vile Isa ndiye aliyetajwa na Qur’an haikutajwa kwenye Aya?

Jibu: maudhui ya Aya ni mjadala kuhusiana na Isa, na masimulizi yake yamesimuliwa na Qur’an. Kwa hiyo kutajwa Bwana Masih ni kutajwa Qur’an. Hili linatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwenye Aya hiyo hiyo: “Hii ndiyo njia iliyonyooka” ambayo makusudio yake ni Qur’an kama tulivyoeleza. La kushangaza ni mfasiri mmoja aliyeirudisha dhamir kwa Isa na kufasiri njia iliyonyooka kuwa ni mwito wa Muhammad (s.a.w.) na Qur’an.

Wala asiwazuie Shetani na haki na kuitumia. Hakika yeye ni adui yenu wa dhahiri.

Uadui wa wazi na chuki inamfanya awaghuri kwa mambo machafu. Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

لَا يَفْتِنَنَّكُمُ الشَّيْطَانُ كَمَا أَخْرَجَ أَبَوَيْكُمْ مِنَ الْجَنَّةِ {27}

“Shetani asiwatie katika fitna, kama alivyowatoa wazazi wenu katika Bustani (Pepo).”
Juz. 8 (7:27).

Na alipokuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimewajia na hikima, na ili niwaeleze baadhi ya yale mliyokhitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnitii.

Makusudio ya dalili hapa ni miujiza inayofahamisha utume wa Isa; kama vile kuponesha upofu na ukoma. Na makusudio ya hikima ni elimu ya dini ya Mwenyezi Mungu na sharia yake.

Maana ni kuwa Isa, ambaye utume wake umethibiti kwa dalili wazi, aliwaambia Wana wa Israili: Nimewajia na hukumu zote za dini, kiitikadi na kisharia na kwazo mtamjua mwenye haki na mbatilifu, basi mcheni Mwenyezi Mungu mtaongoka.

Unaweza kuuliza: Kwa nini amesema baadhi ya mnayohitalifiana na asiseme yote?

Wamejibu kundi katika wafasiri kwamba Makusudio yake ni kuwa Isa (a.s.), kwa wasifu wake kama Mtume, huwa anawabainishia mambo ya dini tu, lakini haingilii mambo ya dunia.
Kuna riwaya ya maulama wa kisunni kutoka kwenye sahihi zao kwamba Mtume (s.a.w.) amesema: “Nyinyi ni wajuzi zaidi wa mambo ya dunia yenu na mimi ni mjuzi zaidi wa mambo ya dini yenu.”

Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu, na Mola wenu. Basi mwabuduni Yeye tu. Hii ndiyo njia iliyonyooka.

‘Hii’ ni ishara ya Tawhid na kukataza shirki. Maana yako wazi, kama alivyosema Razi.

Lakini makundi yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao waliodhulumu kwa adhabu ya siku chungu.

Makusudio ya makundi ni mayahudi na manaswara kwa upande mmoja, na manaswara wenyewe kwa upande wa pili. Mayahudi walisema kuwa Isa ni mtoto wa zina (mwanaharamu), wakipingana katika hilo na manaswara wote na waislamu wote. Na hao manaswara wenyewe nao walikhitalifiana, baada ya Masihi, makundi mbali mabli. Kuna waliosema Isa ni mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wengine wakasema ni mwana wa Mungu na wengine wakasema kuwa yeye ni mungu hasa. Ametakata Mwenyezi Mungu na wanayomsifia.

Hawangoji ila Saa iwajie ghafla na hali wao hawatambui?

Hili ni karipio na kemeo kwa yule anayemfanya Isa kuwa ni Mungu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (12:107).

الْأَخِلَّاءُ يَوْمَئِذٍ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ عَدُوٌّ إِلَّا الْمُتَّقِينَ {67}

Siku hiyo marafiki watakuwa maadui, wao kwa wao, isipokuwa wenye takua.

يَا عِبَادِ لَا خَوْفٌ عَلَيْكُمُ الْيَوْمَ وَلَا أَنْتُمْ تَحْزَنُونَ {68}

Enyi waja wangu! Leo hamtakuwa na khofu, wala hamtahuzunika.

الَّذِينَ آمَنُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا مُسْلِمِينَ {69}

Ambao waliziamini Ishara zetu na wakawa Waislamu.

ادْخُلُوا الْجَنَّةَ أَنْتُمْ وَأَزْوَاجُكُمْ تُحْبَرُونَ {70}

Ingieni kwenye Bustani (Pepo), nyinyi na wake zenu katika hali ya kufurahishwa.

يُطَافُ عَلَيْهِمْ بِصِحَافٍ مِنْ ذَهَبٍ وَأَكْوَابٍ ۖ وَفِيهَا مَا تَشْتَهِيهِ الْأَنْفُسُ وَتَلَذُّ الْأَعْيُنُ ۖ وَأَنْتُمْ فِيهَا خَالِدُونَ {71}

Watapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe; Na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda, na macho yanavifurahia. Na nyinyi mtakaa humo milele.

وَتِلْكَ الْجَنَّةُ الَّتِي أُورِثْتُمُوهَا بِمَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ {72}

Na hiyo ni Bustani (Pepo) mliyorithishwa kwa hayo mliyokuwa mkiyafanya.

لَكُمْ فِيهَا فَاكِهَةٌ كَثِيرَةٌ مِنْهَا تَأْكُلُونَ {73}

Mnayo humo matunda mengi mtakayoyala.

إِنَّ الْمُجْرِمِينَ فِي عَذَابِ جَهَنَّمَ خَالِدُونَ {74}

Hakika wakosefu watakaa milele katika adhabu ya Jahannamu.

لَا يُفَتَّرُ عَنْهُمْ وَهُمْ فِيهِ مُبْلِسُونَ {75}

Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa.

وَمَا ظَلَمْنَاهُمْ وَلَٰكِنْ كَانُوا هُمُ الظَّالِمِينَ {76}

Wala Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio waliokuwa madhalimu.

وَنَادَوْا يَا مَالِكُ لِيَقْضِ عَلَيْنَا رَبُّكَ ۖ قَالَ إِنَّكُمْ مَاكِثُونَ {77}

Na watapiga kelele: Ewe Malik! Na atufishe Mola wako! Atasema: Hakika nyinyi mtakaa humo humo!

لَقَدْ جِئْنَاكُمْ بِالْحَقِّ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَكُمْ لِلْحَقِّ كَارِهُونَ {78}

Kwa yakini tuliwaletea Haki, lakini wengi katika nyinyi mlikuwa mnaichukia Haki.

أَمْ أَبْرَمُوا أَمْرًا فَإِنَّا مُبْرِمُونَ {79}

Au wamekata shauri? Bali ni Sisi ndio tunaopitisha.

أَمْ يَحْسَبُونَ أَنَّا لَا نَسْمَعُ سِرَّهُمْ وَنَجْوَاهُمْ ۚ بَلَىٰ وَرُسُلُنَا لَدَيْهِمْ يَكْتُبُونَ {80}

Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong’ono yao? Wapi! Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika.