read

Aya 81 – 89: Ingelikuwa Mwingi Wa Rehema Ana Mwana

Maana

Sema: Ingelikuwa Mwingi wa rehema ana mwana, basi mimi ningelikuwa wa kwanza kumwabudu.

Mwenye Majamaul-abayan, ameitajia Aya hii ktk njia tano na akarefusha maneno bila ya kuwa na haja ya kufanya hivyo, kwa sababu maana yako wazi nayo ni sema: ewe Muhammad (s.a.w.) kumwambia yule anayedai kuwa Mwenyezi Mungu ana mwana kwamba mimi nitakuwa na wewe lakini kwa sharti ya kunithibitishia dalili mkataa ya hilo.
Lakini hakuna dalili ya madai haya; bali kuna dali ya kinyume chake. Kwa hiyo mimi ni katika wanaompwekesha Mwenyezi Mungu kwa kuamini kuwa Mwenyezi Mungu hakuzaa wala hakuzaliwa.

Kwa ufupi ni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alikufunga kukubali kwake na jambo lilio muhali. Hakuna mwenye shaka kuwa kuli- funga jambo na muhali ni sawa na muhali. Mfumo huu ni maarufu kwa maulama katika kujadiliana, na ni wa kumnyamazisha mbishi.

Ametakasika Mola wa mbingu na ardhi, Mola wa Arshi, na hayo wanayomsifia ya kumnasibishia mtoto na mshirika. Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na hiyo siku yao wanayoahidiwa. Makusudio ya porojo na kucheza ni kusema kuhusu Mwenyezi Mungu bila ya ujuzi. Siku yao ni Siku ya Kiyama.

Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika ardhi. Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi.

Mwenyezi Mungu pekee ndiye muumba wa ulimwengu pamoja na ardhi yake na mbingu yake, ndiye mpangiliaji wake kwa ujuzi wake na hekima yake; hakuna yoyote asiyekuwa Yeye anayestahiki ibada.

Na amekuwa na baraka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa ya Kiyama.

Kaulia yake ‘na viliomo kati yake’ inaashiria kuwa katika anga kuna vitu tusivyovijua uhakika wake, na hakuna anayejua Kiyama kitakuwa lini isipokuwa Mwenyezi Mungu tu.

Na kwake Yeye mtarudishwa kwa ajili ya hisabu na malipo.

Wala hao wanoaomba badala yake Yeye hawana uweza wa uombezi, isipokuwa anayeshuhudia kwa haki, na wao wanajua.

Wao wanaabudu masanamu kwa kudai kuwa yatawaombea kwa Mwenyezi Mungu. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawaambia, hapana, hakuna anayeweza kuombea kwake isipokuwa yule anayemtamkia neno la Tawhid, akaliamini kwa ujuzi, na lazima anayeombewa awe anastahiki uombezi na msamaha

Na ukiwauliza ni nani aliyewaumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu! Basi wanageuzwa wapi?

Wao wanakubali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Aliewaumba, lakini bado wanaacha kumwabudu na kuayendea masanamu. Umetangulia mfano wake katika Aya 9 ya sura hii tuliyo nayo.

Na usemi wake Mtume ni: Ewe Mola wangu! Hakika hawa ni watu wasioamini. Basi wasamehe, na uwaambie manenoyasalama. Watakuja jua.

Maana ni kuwa Mtume alimwambia Mola wake kuwa wale ulionituma kwao hawakuniitikia. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akamwambia usijali na upinzani wao, kwani mwisho ni wako sio wao. Makusudio ya salama hapa ni kama makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَإِذَا خَاطَبَهُمُ الْجَاهِلُونَ قَالُوا سَلَامًا {63}

“Na wajinga wakiwasemesha husema: Salama” Juz. 19 (25:63).