read

Aya 22 – 33: Watu Hawa Ni Wakosefu

Maana

Ndipo akamwomba Mola wake kuwa watu hawa ni wakosefu.

Musa alikata tamaa na Firauni na watu wake, ndipo akawaombea mabaya na akasema: “Ewe Mwenyezi Mungu waharakishie maangamizi duniani kwa sababu ya kufuru yao.” Mwenyezi Mungu akamwitikia dua yake na kumwambia: Basi nenda na waja wangu usiku. Hakika mtafuatwa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimwamrisha atoke Misri yeye na wana wa Israil usiku na akamjulisha kuwa Firauni na watu wake watawafuata.

Na iache bahari imetulia, hakika wao ni jeshi litakalozamishwa.
Fuata njia ya baharini, ukishavuka upande wa pili, wewe iwache kama ilivyo, kwa sababu jeshi la adui litaingia na wataangamia wote.

Mabustani mangapi, na chemchem ngapi waliziacha! Na mimea na mahala pa fahari! Na neema walizokuwa wakijistareheshea! Ndivyo hivyo! na tukawarithisha haya watu wengine.

Watu wa Firauni walikuwa katika starehe za vyakula na vinywaji, wana utawala, makasri, mito na matunda. Mwenyezi Mungu akawatumia Musa kuwalingania kwenye uadilifu na kuacha ufisadi katika nchi, lakini hawakumwitikia mlinganiaji wa Mwenyezi Mungu. Basi akawaangamiza na akawarithisha watu ambao hawakuwa na uhusiano wowote na wao.

Sheikh Al-Maraghi anasema akifasiri Aya hii: “Wakati fulani wasyria walichukua Misr na wakati mwingine ikachukuliwa na wababilon na pia wahabeshi. Kisha wafursi, wayunani (wagiriki), waroma, na waarabu. Vile vile utawala wa Altoulenion, Alikhchidip, Fatimid, Ayyubids, Mamluk, Uturuki, Ufaransa na Uingereza. Na sisi hivi sasa tunapigana ili kuwatoa katika nchi yetu ili tuweze kumakinika na uhuru wa chi yetu.”

Sheikh huyu alikuwa katika zama za mfalme Faruk Bin Fuad. Nasi tunaunganisha maneno yake kwa kusema: Hivi sasa Uzayuni umepora Sinai na ukanda wa mashariki katika mfereji wa Suez, kwa msaada U.S.A. kambi mpya ya ukoloni.

Na wamisri wanajitahidi na kupigana kuwatoa wavamizi kwenye ardhi yao. Haya ndio maisha ya jihadi na mapigano. Mtu kufa na bunduki mkononi akipigania nchi yake na heshima yake ni bora zaidi kuliko kuishi maisha ya udhalili na utwevu.

Mbingu na ardhi hazikuwalilia.

Hiki ni kinaya cha kutowapa umuhimu watu wa Firauni pale Mwenyezi Mungu alipowagharikisha baharini, wala hawakupewa muda; bali Mwenyezi Mungu aliharakisha maangamizi yao duniani.

Na hakika tuliwaokoa wana wa Israili katika adhabu ya kuwadhalilisha ambayo ni kuuawa watoto wao wa kiume na kutumikishwa wanawake wao na mabinti zao na pia kudhalilishwa wanaume kwa kazi za sulubu
Ya Firauni. Hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupituka mipakaya kila ufisadi, uasi na kiburi. Na hakika tuliwachagua kwa ujuzi kuliko walimwengu wengine.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.), katika Kitabu chake, amewasifu kwa sifa mbaya wana wa Israil, akasajili
makosa makubwa waliyoyafanya; kama vile usaliti, kuifanyia jeuri haki na kula mali kwa dhulma.

Vile vile amewasifu kwa ukafiri, dhulma na akawalaani katika Aya kadhaa na kuwatishia kwa adhabu kali.

Kwa maana hii ndio wafasiri wakakongamana kuwa makusudio ya walimwengu, katika Aya hii na mfano wake, ni walimwengu wa zama zao si kila zama.

Katika Juz. 1 (2:47-48) tulisema kuwa Mwenyezi Mungu aliwafadhilisha juu ya watu wa zama hizo kwa vile tu Mwenyezi Mungu aliwatuma mitume wengi kutokana na wao. Hivi sasa tumepata wazo kutokana na Aya tuliyo nayo kuwa makusudio ya walimengu ni Firauni na wale walioukubali uungu wake na wala sio watu wote wa wakati ule. Siri ya kufadhilishwa huko ni kuwa waisrail hawakumwabudu Firauni kama wamisri waliotangulia.

Na tukawapa katika ishara zenye majaribio yaliyo wazi.

Makusudio ya ishara hapa ni miujiza; kama kupasuka bahari, kufunikwa na kiwingu, kuteremshiwa Manna na Salwa na kububujika maji kutoka kwenye jiwe. Na Makusudio ya majaribio ni neema. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

وَنَبْلُوكُمْ بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً ۖ وَإِلَيْنَا تُرْجَعُونَ {35}

“Na tutawajaribu kwa mtihani wa shari na heri na kwetu mtarejeshwa.” Juz. 17 (21:35).

إِنَّ هَٰؤُلَاءِ لَيَقُولُونَ {34}

Hakika hawa wanasema:

إِنْ هِيَ إِلَّا مَوْتَتُنَا الْأُولَىٰ وَمَا نَحْنُ بِمُنْشَرِينَ {35}

Hapana ila kufa kwetu mara ya kwanza tu, wala sisi hatu- fufuliwi.

فَأْتُوا بِآبَائِنَا إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {36}

Basi warudisheni baba zetu, ikiwa mnasema kweli.

أَهُمْ خَيْرٌ أَمْ قَوْمُ تُبَّعٍ وَالَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ ۚ أَهْلَكْنَاهُمْ ۖ إِنَّهُمْ كَانُوا مُجْرِمِينَ {37}

Je, wao ni bora au watu wa Tubbaa’ na walio kuwa kabla yao? Tuliwaangamiza. Hakika hao walikuwa wakosefu.

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا لَاعِبِينَ {38}

Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake kwa mchezo.

مَا خَلَقْنَاهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ {39}

Hatukuviumba ila kwa haki. Lakini wengi wao hawajui.

إِنَّ يَوْمَ الْفَصْلِ مِيقَاتُهُمْ أَجْمَعِينَ {40}

Hakika siku ya Upambanuzi ni wakati uliowekwa kwa wao wote.

يَوْمَ لَا يُغْنِي مَوْلًى عَنْ مَوْلًى شَيْئًا وَلَا هُمْ يُنْصَرُونَ {41}

Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala hawatanusuriwa.

إِلَّا مَنْ رَحِمَ اللَّهُ ۚ إِنَّهُ هُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ {42}

Isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu atamrehemu Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.