Chakula Cha Mwenye Dhambi Na Cha Mwenye Takua Aya 43 – 59
Maana
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwataja wakosefu, katika Aya iliyotangulia, na kwamba ahadi yao ni siku ya Kiyama, sasa anataja hali yao itakavyokuwa, kama ifuatavyo:
Hakika Mti wa Zaqqum, Ni chakula cha mwenye dhambi, ambaye dhambi zake na makosa yake yalikithiri duniani. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameyasifu matunda ya mti huu kuwa ni kama mafuta mazito, hutokota matumboni kama kutokota kwa maji ya moto.
Sio mbali kuwa hiki ni kinaya cha uchungu wa adhabu na ukali wake. Mulla Sadra anasema katika Al-asfar: Mti wa Zaqqum ni itikadi za ubatilifu na tabia mbaya zinazompeleka mtu kwenye moto. Baadhi ya mapokezi yanaeleza kuwa ubakhili ni mti miongoni mwa miti ya Motoni na ukarimu ni mti miongoni mwa miti ya Peponi.
Mkamateni na mburuzeni mpaka katikati ya Jahannamu!
Yaani wataambiwa Malaika wa motoni mburuzeni hadi katikati ya Jahannam, kisha mmwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayochemka.
Hii inaashiria kuwa kwenye Jahannam kuna matunda, hamamu na mavazi, lakini yote yanatokana na moto.
Onja! Hakika wewe ndiye mwenye nguvu, mtukufu! Hakika haya ndiyo mliyokuwa mkiyatilia shaka.
Malaika wa adhabu watamwambia taghuti mwenye dhambi: wewe ulipinga siku ya ufufuo na ukadai kuwa ni mkubwa na mtukufu, basi hivi sasa onja malipo ya kujitukuza kwako na kiburi chako.
Kadiri ninavyotia shaka, lakini siwezi kutia shaka yoyote kuwa wale wanaopora mali za watu na kuzitengenezea silaha za maangamizi kwa ajili ya kuwaua wasiokuwa na hatia, wakiwemo wanawake na watoto, na wala wasione haki wala uadilifu isipokuwa yale wanayoyataka na kuyatamani, sitii shaka kabisa kwamba hawa wanastahiki aina hii ya adhabu; bali wanastahiki zaidi ya adhabu hii kama ingeliokuwako. Tazama Juz. 13 (14:46-52), kifungu cha ‘Jahannam na silaha za maangamizi.’
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kubainisha hali za wakosefu, sasa anaashiria hali za wenye takua siku ya Kiyama, kwa Aya zinazofuatia:
Hakika wenye takua watakuwa katika mahali pa amani, hawatakuwa na hofu wala kuhuzunika. Katika mabustani na chemchem, wakistarehe kadiri watakavyo.
Watavaa hariri nyepesi na hariri nzito wakikabiliana.
Nguo zao ni hariri laini na nzito na watakaa kwenye viti wakielekeana wao kwa wao, wakibarizi huku wanashukuru kwa kukumbuka neema ya Mwenyezi Mungu na radhi zake.
Ndio kama hivyo! na tutawaoza mahurulaini, ambao hajawagusa mtu kabla yao wala jinni.
Humo watataka kila aina ya matunda, na wakae kwa amani.
Watataka matunda bila ya kuhofia kuwa yataisha.
Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na Mwenyezi Mungu atawalinda na adhabu ya Jahannamu.
Kila mtu atakufa mauti ya kwanza na baadae ataguria Peponi au Motoni, hakuna kufa huko, lakini kufa ni bora sana kuliko uhai katikati ya Jahannam.
Ni fadhila zitokazo kwa Mola wako. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
Kuna kufuzu gani kukubwa zaidi ya kuokoka na adhabu ya moto na ghad- habu ya Mwenyezi Mungu?
Basi tumeifanya nyepesi hii kwa ulimi wako, ili wapate kukumbuka.
Iliyofanywa nyepesi ni Qur’an. Wanaotakiwa kukumbuka ni waarabu na ulimi ni wa Mtume. Maana ni kuwa tumeiteremsha Qur’an kwa kiarabu ili waarabu wanufaike na mafunzo yake na mawaidha.
Basi ngoja tu, na wao wanangoja.
Ngoja kidogo ewe Muhammad, utaona mwisho utakuwa wako. Wao wanakuduia ufikwe na mabaya, lakini: “Ameaangamia mwenye kuduia na amerudi utupu mwenye kuzua na mwenye kuigeukia haki ameangamia,” kama anavyosema Imam Ali. (a.s.).