Aya 1 – 6: Katika Mbingu Na Ardhi Kuna Ishara Kwa Waumini
Maana
Haa miim.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:1).
Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Makusudio ya kitabu ni Qur’an, na yote kuanzia mwanzo wake hadi mwisho wake ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu si kwa mwenginewe. Mwenye Ruhul-bayan anasema: “Wasifu wa Mwenyezi Mungu kuwa Mwenye nguvu, hapa unafahamisha kuwa Qur’an ni muujiza unaomshinda nguvu kila mwenye kuipinga. Na wasifu wake kuwa ni mwenye hikima unajulisha kuwa Qur’an ina hikima ya hali ya juu yenye kunufaisha. Hakuna mwenye shaka kuwa Qur’an ni muujiza unaomshinda kila mwenye kupingana nayo na kwamba hiyo ni chimbuko la hekima na kianzio chake.”
Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akaishiria kwenye dalili ya hisia zinazotamka kuweko kwake na utukufu wake; miongoni mwazo ni:
Hakika katika mbingu na ardhi kuna Ishara kwa waumini.
Yaani kwa anayetaka kuamini haki kwa kuwa ni haki. Makusudio ya Ishara hapa ni yale yanayovumbuliwa na akili kama vile nidhamu ya ulimwengu na sera yake kwenye desturi isiyokuwa na mabadiliko wala mageuzi. Lau si uthabiti wake isingeliwezekana kuipima na kufaidika nayo; hatimae ilimu ya sayari isingelikuwa na athari yoyote.
Na katika umbo lenu na katika wanyama aliowatawanya zimo ishara kwa watu wenye yakini.
Mwenye kutaka kujua kwa yakini kuweko Mwenyezi Mungu, naafikirie na kujitaamali yeye mwenyewe na katika kila kilicho na uhai, je, atapata kiungo hata kimoja kisicho na kazi au silika yoyote isiyokuwa na hikima?
Hii inafahamisha kwa dalili mkataa ya kuweko utashi na azma, ikiwa hatumuoni huyo mwenye utashi na azma basi tunaona athari yake kwa macho kabisa, kwa hiyo basi imani yetu kwa mambo ya ghaibu inategemea hisia na kuona.
Na kupishana usiku na mchana.
Mara nyingi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameashiria kuhitalifiana usiku na mchana ili kuizindua akili kwenye siri za ajabu katika mzunguko wa ardhi, kwa vile ndio sababu ya kuja usiku baada ya mchana.
Yote yaliyosemwa kuhusu sababu za mzunguko wa ardhi hiyo yenyewe au kando ya jua na sababu nyinginezo, zote zinaishia kwenye matakwa ya muumbaji wa kwanza na uwezo wake na hekima yake. Ni jambo lisiloingilika akilini kuwa chimbuko la maajabu yote haya liwe ni mada pofu inayohukumiwa na sadfa, bila ya mpangilio, wala makusdio au lengo!
Na riziki anayoiteremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwayo akaifufua ardhi baada ya kufa kwake.
Makusudio ya riziki hapa ni kila kitu chenye athari katika uhai; kama vile maji na joto la jua nk. Ambayo ndani yake kuna ufahamisho wa kuweko muumba wa viliomo mbinguni na katika ardhi. Kwa sababu vyote hivyo vimepatikana kwa lengo na hekima iliyo sahihi.
Na mabadiliko ya upepo, kusi na kaskazi, matlai na umande na joto na baridi ni Ishara kwa watu wenye akili.
Yote hayo na mengineyo ni dalili mkataa ya utashi wa mwenye ujuzi na hikima
Hizo ni Ishara za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki.
Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyoweka mbele ya akili ushahidi na dalili za hisia za kumjua muumba na uweza wake.
Basi hadithi gani watakayoiamini baada ya Mwenyezi Mungu na Ishara zake?
Ambaye hakunufaika na ubainifu wa Mwenyezi Mungu na kutokinai na dalili zake basi hakuna hoja yoyote itakayomfaa. Maana ya Aya hii yamekaririka mara nyingi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu; miongoni mwazo ni ile iliyo katika Juz. 2 (2:164).
Katika Nahjul-balagha kuna maelezo haya: “Katika kuumba kwake, kikubwa, kidogo, kizito, chenye nguvu na hafifu, ni sawa tu. Vile vile mbingu hewa, upepo na maji. Hebu angalia jua, mwezi, mimea, miti, maji, na jiwe. Pia kupishana huu usiku na mchana, kububujika hizi bahari, kukithiri milima, urefu wa vilele hivi na kutofautiana lugha na lahaja. Ole wake mwenye kumkataa mkadiriaji na akamkana mpangiliaji. Wanajifikiria ni kama mimea isiyokuwa na mkulima wala kuwa kutofautiana sura zao kusiwe na mtengenezaji. Hawana hoja na wanayodai wala uhakiki kwa waliyoyasikia. Je, jengo linaweza kuwa bila ya fundi? Au hatia bila ya kuweko mkosaji?”
وَيْلٌ لِكُلِّ أَفَّاكٍ أَثِيمٍ {7}
يَسْمَعُ آيَاتِ اللَّهِ تُتْلَىٰ عَلَيْهِ ثُمَّ يُصِرُّ مُسْتَكْبِرًا كَأَنْ لَمْ يَسْمَعْهَا ۖ فَبَشِّرْهُ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ {8}
وَإِذَا عَلِمَ مِنْ آيَاتِنَا شَيْئًا اتَّخَذَهَا هُزُوًا ۚ أُولَٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُهِينٌ {9}
مِنْ وَرَائِهِمْ جَهَنَّمُ ۖ وَلَا يُغْنِي عَنْهُمْ مَا كَسَبُوا شَيْئًا وَلَا مَا اتَّخَذُوا مِنْ دُونِ اللَّهِ أَوْلِيَاءَ ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ {10}
هَٰذَا هُدًى ۖ وَالَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ لَهُمْ عَذَابٌ مِنْ رِجْزٍ أَلِيمٌ {11}
اللَّهُ الَّذِي سَخَّرَ لَكُمُ الْبَحْرَ لِتَجْرِيَ الْفُلْكُ فِيهِ بِأَمْرِهِ وَلِتَبْتَغُوا مِنْ فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ {12}
وَسَخَّرَ لَكُمْ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مِنْهُ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ {13}
قُلْ لِلَّذِينَ آمَنُوا يَغْفِرُوا لِلَّذِينَ لَا يَرْجُونَ أَيَّامَ اللَّهِ لِيَجْزِيَ قَوْمًا بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ {14}
مَنْ عَمِلَ صَالِحًا فَلِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ أَسَاءَ فَعَلَيْهَا ۖ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ {15}