read

Aya 16 – 20: Wana Wa Israil Tena

Maana

Na hakika tuliwapa Wana wa Israili Kitabu na hukumu na Unabii, na tukawaruzuku vitu vizuri, na tukawafadhilisha kuliko walimwengu.

Katika Aya zilizotangulia, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewataja wazushi wenye dhambi ambao wamezikanusha dalili za Mwenyezi Mungu na wakaidharau haki na watu wake.

Kwa kuwa Wana wa israil ni mfano halisi wa sifa hizi, ndio akafuatishia kuwataja na yale waliyo nayo ya upinzani na madhambi; pamoja na kuwa Mwenyezi Mungu aliwaneemesha kwa Tawrat na Injil alizoziashiria kwa neno Kitab. Akawafahamisha mawaidha na hukumu zilizomo ndani ya vitabu hivyo. Na hayo ndio makusudio ya ‘Hukumu.’

Akawafanyia mitume kutokana na wao na akawateremshia Manna na Salwa, alizoziashiria Mwenyezi Mungu kwa neno ‘Vitu vizuri.’ Pia akawafadhilisha juu ya watu wa Firauni pale alipowagharikisha na waisrail wakapumua kutokana na adhabu yao.
Na tukawapa maelezo wazi ya amri.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwafafanuliwa Wana wa Israil mahitaji yao ya mambo ya dini, hawakubakiwa na udhuru au visababu vya kutofautiana na kufarikiana.

Basi hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa ajili ya uhasidi uliokuwa baina yao.

Waliyajua kwa yakini yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu kwa Musa, lakini wao wakajitia kutojua na wakayageuza kulingana na matamanio na masilahi yao:

مِنَ الَّذِينَ هَادُوا يُحَرِّفُونَ الْكَلِمَ عَنْ مَوَاضِعِهِ وَيَقُولُونَ سَمِعْنَا وَعَصَيْنَا {46}


“Miongoni mwa mayahudi wako ambao hugeuza maneno kutoka mahali mwake na husema: tumesikia na tumeasi.” Juz. 5 (4:46).

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Basi hawakukhitalifiana,” inaashiria kuwako wachache kwa nadra waliothibiti katika haki.

Hakika Mola wako atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika waliyokuwa wakikhitalifiana.

Katika maisha ya duniani, mara nyingine asiyekuwa na haki humshinda mwenye haki, lakini akhera itakayokuwa juu ni haki peke yake; vinginevyo mwenye haki angekua ni mbaya kuliko asiyekuwa na haki.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 11 (10:93).

Waisrail Wamepigwa Na Udhalili Kwa Hukumu Ya Tawrat

Qur’an imewazungumzia Wana wa Israil kwa kusema: “Wamepigwa na udhalili popote wanapokutanikana” Juz. 4 (3:112). Huko tumezungumza kwa ufafanuzi zaidi kuhusu Aya hii na tukasema kuwa Israil ni kambi ya kijeshi ya ukoloni na kwamba itaisha tu, sasa au baadaye.

Hivi sasa tutanukuu kitabu kitakatifu kwa Mayahudi yale yanayofahamisha kwa uwazi kuwa Mwenyezi Mungu amewaandikia Waisrail udhalili hadi siku ya mwisho: “Kwa hiyo BWANA akawaghadhibikia Israel sana…. Kwa hiyo BWANA akakitaa kizazi chote cha Israel, akawatesa.”
(2 Wafalme 17:18 – 20)

“Basi BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawalisha pakanga, naam, watu hawa nami nitawapa maji ya uchungu wanywe. Nami nitawatawanya kati ya mataifa, ambao hao hawakuwajua; wala baba zao; nami nitatuma upanga nyuma yao, hata nitakapowaangamiza.” (Yeremia 9:15-16)

“Nanyi mtasalia wachache kwa hisabu…..Nanyi mtanyakuliwa katika hiyo nchi” Kumbukumbu la (Torati 28: 62-63). Maneno katika nukuu zote hizo yanaelekwezwa kwa Wana wa Israil. Kuna nukuu nyinginezo zaidi ya hizi.

Tunawauliza wazayuni: Ikiwa nyinyi ni taifa teule la Mwenyezi Mungu, kama mnavyodai, basi kwa nini nyinyi na kizazi chenu Mwenyezi Mungu amewahukumia udhalili, kufukuzwa hadi kung’olewa kabisa? Vipi Mola akatoa ahadi kuwa ataifanya Jerusalem ni magofu na makao ya mbweha? Kama ilivyoelezwa katika Yeremia 9:11, “Nami nitafanya Yerusalem kuwa magofu, makao ya mbweha; Nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa, isikaliwe na mtu awaye yote.”

Ni kipi hicho Kitabu kitakatifu kwa ajili ya dola yenu ya kidini ya kiubaguzi, kama alivyosema Pompidou, raisi wa ufaransa? Je, ni Tawrat iliyowasifu nyinyi na mji wenu kwa kusema: “Bwana asema hivi; mji – yaani Yerusalem – umwagao damu ndani yake…Tazama, wakuu wa Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya nguvu zake, wamekuwamo ndani yako, ili kumwaga damu.”
(Ezekieli 22: 3,6.)
Vile vile umeshutumiwa mji wa Jerusalemu, kwenye Luka mtakatifu 13:34: “Ewe Yerusalemu, Yerusalemu, wewe uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako!”

Inasema Biblia kuwa kila mahali na kila wakati Mayahudi ni washirika wa hatia ya mababu zao waliomsulubu Bwana Masih, kwa sababu wanaliridhia hilo kwa vitendo vyao kwa kusema kuwa Yeye ni mwanaharamu.

Hayo yanaafikiana na msingi wa kiislamu unaosema kuwa mwenye kufanya dhulma, mwenye kuisaidia na mwenye kuiridhia wote ni washirika.

Ndio maana kanisa la Khufti (Coptic), likaingilia kati kumpinga Baba mtakatifu, wakati yeye na wasaidizi wake walipotoa tamko rasmi la kukisafisha kizazi cha kiyahudi na damu ya Bwana Masih.

Ieleweke kuwa Baba mtakatifu alitoa tamko hili kabla ya muda mchache Israil kuvamia miji ya Kiarabu.

Kisha tukakuweka juu ya sharia katika amri, basi ifuate.

Neno sharia katika Lugha lina maana ya chemchem ya maji. Kisha likaazimwa kutumiwa kwenye hukumu za dini. Kwa sababu zinaipa uhai roho; kama maji yanayvoupa uhai mwili. Makusudio ya amri hapa ni dini. Maana ni kuwa Ewe Muhammad tumekujaalia kwenye itikadi ya Tawhid na kuing’oa shirki na tukakupa sharia nyepesi, basi shikamana nayo. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: wala usifuate matamanio ya wasiojua, maana yake ni kuwa wakosefu hawafuati isipokuwa matamanio na lengo.

Na wala usizichukulie lawama za mwenye kulaumu, na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atakutosha na vitimbi vya wenye vitimbi na shari za wenye njama.

Kwa hakika hao hawatakufaa kitu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kwa sababu anayeshindwa kujikinga yeye mwenyewe hawezi kumsaidia mwingine.

Na hakika wenye kudhulumu ni mawalii wao kwa wao.

Mwenye hatia duniani hapati wa kumsaidia na kumnusuru isipokuwa aliye kama yeye katika hatia na dhambi, na walio wema ni maadui zake na wagomvi wake. Lakini huko Akhera, wenye hatia watalaniana wao kwa wao. Na Mwenyezi Mungu ni walii wa wenye takua, duniani na Akhera.

Hizi ni dalili zilizo wazi kwa watu wote, na ni mwongozo, na rehema kwa watu wanaoyakinisha.

Ni dalili zinazowaonyesha haki na njia ya uongofu. Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kufuata Qur’an anakuwa na yakini kwamba yeye yuko kwenye uongofu Kutoka kwa Mola na kuingia kwenye rehema yake. Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7:203).

أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ اجْتَرَحُوا السَّيِّئَاتِ أَنْ نَجْعَلَهُمْ كَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَوَاءً مَحْيَاهُمْ وَمَمَاتُهُمْ ۚ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ {21}

Je, wanadhani wanaotenda maovu kuwa tutawafanya kama walioamini, na wakatenda mema, sawa sawa uhai wao na kufa kwao? Ni mabaya wanayohukumu.

وَخَلَقَ اللَّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ وَلِتُجْزَىٰ كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ {22}

Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki. Na ili kila nafsi ilipwe yale iliyoyachuma. Nao hawatadhulumiwa.

أَفَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَٰهَهُ هَوَاهُ وَأَضَلَّهُ اللَّهُ عَلَىٰ عِلْمٍ وَخَتَمَ عَلَىٰ سَمْعِهِ وَقَلْبِهِ وَجَعَلَ عَلَىٰ بَصَرِهِ غِشَاوَةً فَمَنْ يَهْدِيهِ مِنْ بَعْدِ اللَّهِ ۚ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ {23}

Je, umemwona aliyefanya hawaa yake kuwa ndio mungu wake? Basi nani atamwongoza baada ya Mwenyezi Mungu? Hamkumbuki?

وَقَالُوا مَا هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا يُهْلِكُنَا إِلَّا الدَّهْرُ ۚ وَمَا لَهُمْ بِذَٰلِكَ مِنْ عِلْمٍ ۖ إِنْ هُمْ إِلَّا يَظُنُّونَ {24}

Na walisema: Hapana ila uhai wetu wa duniani - twafa na twaishi, na hapana kinachotuhilikisha isipokuwa dahari. Lakini wao hawana ilimu ya hayo, ila wao wanadhani tu.

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ مَا كَانَ حُجَّتَهُمْ إِلَّا أَنْ قَالُوا ائْتُوا بِآبَائِنَا إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {25}

Na wakisomewa Aya zetu zilizo wazi hawana hoja ila kusema: Waleteni baba zetu, ikiwa nyinyi ni wakweli.

قُلِ اللَّهُ يُحْيِيكُمْ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يَجْمَعُكُمْ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ لَا رَيْبَ فِيهِ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ {26}

Sema: Mwenyezi Mungu anawapa uhai, kisha anawafisha, kisha anawakusanya, Siku ya Kiyama isiyo na shaka.