read

Aya 21 – 26: Ameifanya Hawa Yake Ndio Mungu Wake

Maana

Je, wanadhani wanaotenda maovu kuwa tutawafanya kama walioamini, na wakatenda mema, sawa sawa uhai wao na kufa kwao? Ni mabaya wanayohukumu.

Inawezekana mwema na muovu wawe na daraja sawa mbele ya Mwenyezi Mungu na katika mtazamo wa kiakili? Basi kutakuwa na haja gani ya kuitwa mwema na mwengine muovu? Nini itakuwa tofauti ya heri na shari?

Wataalamu wa ilimu ya teologia wamechukua madhumuni ya Aya hii na wakasema kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewaahidi watiifu thawabu na akawahidi waasi adhabu, na duniani hakutokei kitu katika hayo. Kwa hiyo basi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawajibisha kurudisha uhai baada ya mauti ili upatikane utekelezaji wa ahadi yake.

Vile vile Mwenyezi Mungu ni mwadilifu, hilo halina shaka, na tunamuona dhalimu akimaliza maisha yake bila ya kulipizwa kisasi na yoyote aliyedhulumiwa. Lau si kurudi kwa hisabu na malipo, basi mdhulumiwa angelikuwa na hali mbaya zaidi ya dhalimu na Mwenyezi Mungu angelikuwa dhalimu. Ametakata sana Mwenyezi Mungu na hayo.

Ama neema za dunia sio alama ya kuridhia Mwenyezi Mungu. Wala shida ya dunia sio dalili ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Imam Ali (a.s.) anasema: “Enyi watu! Hakika dunia ni ya kupita na akhera ni ya kutulia, basi chukueni kutulia kwenu katika mapito yenu…nyoyo zenu zitoeni duniani kabla hazijatoka milini mwenu. Kwenye hiyo dunia mnapewa mtihani na mmeumbwa kwa ajili ya kwengine sio duniani.”

Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki.

Hii ni sababu ya kutofanywa sawa mwema na muovu. Ubainifu wake ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameumba ulimwengu kwa haki na uadilifu; vinginevyo ingelikuwa kuumbwa ulimwengu ni kwa mchezo na ubatilifu.

Kwa sababu mwenye kufanya mchezo kwenye jambo moja anaweza kufanya kwenye jambo jingine.

Na ili kila nafsi ilipwe yale iliyoyachuma. Nao hawatadhulumiwa.

Hii ndio njia ya usawa – njia ya haki na uadilifu; mwenye kufanya heri kwa uzani wa chembe ataiona, na mwenye kufanya shari kwa wizani wa chembe ataiona. Tazama Juz. 11 (10:4) kifungu cha: ‘Hisabu na malipo ni lazima.’

Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu ana hekima na ameepukana na makosa, na hekima yake Mwenyezi Mungu Mtukufu inapelekea kuwafufua watu baada ya mauti, ili kumpambanua mwema na muovu na kumlipa kila mmoja stahiki yake. Kama si hivyo basi kuumbwa ingelikuwa ni kwa mchezo. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Je, mnadhani kuwa tuliwaumba bure na kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa? Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa haki.” yaani ametakasika na mchezo. Juz. 18 (23:115-116)

Je, umemwona aliyefanya hawa yake kuwa ndio mungu wake?

Miongoni mwa watu kuna yule ambaye haamini chochote isipokuwa nafsi yake na masilahi yake tu. Anaweza kuwa anasoma tahlili na takbira; bali anaweza pia kuwa anafunga na kuswali, madamu hilo haliingiliani na anayoyapenda na kuyatamani. Hawa yake ndiyo muabudiwa wa haki peke yake, mengineyo ni nyenzo tu, sio lengo; au ni mazoweya tu sio ibada. Haya ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘aliyefanya hawa yake kuwa ndio mungu wake.’

Neno hawa limetokana na neno la kiarabu linalotamkwa hivyo hivyo ‘Hawaa’ lenye maana pia ya kuanguka chini. Kuna mmoja amesema, hali hiyo imeitwa hawa kwa sababu inamwangushwa kwenye Jahannam aliye nayo. Msemaji amechukua fikra hii kutokana kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَىٰ {40}

فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِيَ الْمَأْوَىٰ {41}

“Na ama yule mwenye kuogopa kusimama mbele ya Mola wake, na akaikataza nafsi na hawa, basi hakika Pepo ndio makazi (yake).” (79:40-41).

Kuna tafsiri inayosema kuwa mshirikina aliye jahili, alikuwa akiangukia jiwe kuliabudu, kisha anaona jingeni analiangukia na kulitupa lile la kwanza. Ndio hivyo anayemtupa Mungu na kuangukia kwenye ‘hawa’ kuwa ndio Mungu wake.

Hakuna mwenye shaka kwamba mshirikina mpumbavu, hatia yake mbele ya Mwenyezi Mungu inazidiwa na kibaraka anyeiuza dini yake na dhamira yake kwenye mnada na kushikana na yule anayezidisha bei.

Na Mwenyezi Mungu akampoteza licha ya ilimu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hampotezi. Atampotezaji na hali Yeye ndiye aliyekataza upotevu na akautolea kiaga kikali? Lakini anyefuata njia ya upotevu kwa hiyari anamwachila mbali na upotevu wake, wala hapatwi na upole wake na msaada wake, baada ya kujua kwa mbali upotevu wake na inadi yake.

Ama kauli yake: na akapiga muhuri juu ya masikio yake, na moyo wake, na akaweka kizibo machoni mwake, maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anampofusha na kumtia uziwi mwenye inadi baada ya kuitambua haki kwa macho yake na masikio yake, baada ya kubainishiwa na kuhimizwa, lakini akipinga bila ya sababu za maana. Mwenyezi Mungu nasema:

فَلَمَّا زَاغُوا أَزَاغَ اللَّهُ قُلُوبَهُمْ ۚ وَاللَّهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ {5}

“Lakini walipopotoka, Mwenyezi Mungu akazipotoa nyoyo zao, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu mafasiki.” (61:5).

Basi nani atamwongoza baada ya Mwenyezi Mungu? Hamkumbuki? Asiyenufaika na mawaidha ya Mwenyezi Mungu basi hayawezi kumfaa mwaidha na nasaha zote.

Na walisema: Hapana ila uhai wetu wa duniani - twafa na twaishi, na hapana kinachotuhilikisha isipokuwa dahari.

Wamaada au wadahari, vyovyote utakavyowaita, wanasema kuwa binadamu ni mchanaganyiko wa vitu vya kimaada vilivyokusanyika kutoka huku na huko na vikafanyika. Kwa hiyo akifa ndio amekwisha, hakuna chochote baada ya mauti, sawa na mimea na wadudu. Na kwamba hizi hisia na utambuzi tunaouna kwa binadamu zimezalishwa na mwili kutokana na mchanganyiko wa hali. Yaani akili ya mwanadamu ni mkondo wa pili usiokuwa na asili na chanzo.

Lakini wao hawana ilimu ya hayo, ila wao wanadhani tu.

Yaani kauli yao hii ni madai yasiyokuwa na hoja; bali kuna hoja ya kuayavunja. Yule ambaye anaihukumu maada, kuipatia manufaa na kujua mengi zaidi kuihusu, lakini yenyewe isimjue yeye, hapana budi kuwa, mtu huyu wa ajabu, awe ni mkuu na yuko zaidi kuliko maada. Yametangulia maneno kuhisiana na hayo mara nyingi; kama vile kwenye Juz. 14 (16:78).

Na wakisomewa Aya zetu zilizo wazi hawana hoja ila kusema: Waleteni baba zetu, ikiwa nyinyi ni wakweli.

Hii ni sawa na anayesema, siwezi kuamini kuwa mtofahaa unaweza kuzaa matunda wakati wa kaskazi mpaka niuone una mimba wakati wa kusi. Mtoto huyu akishakuwa mkubwa, atajua kuwa kila kitu kina muda wake na kwamba kila ajali ina maandishi haikawii wala kuwahi. Umetangulia mfano wake katika Juzuu hii tuliyo nayo kwenye (44:36).

Sema: Mwenyezi Mungu anawapa uhai, kisha anawafisha, kisha anawakusanya, Siku ya Kiyama isiyo na shaka.

Ikiwa Mwenyezi Mungu ndiye anayempa uhai mtu alipokuwa si chochote, atashindwa vipi kumpa uhai mara ya pili? Lakini watu wengi hawajui kuwa kurudishwa mara ya pili ni rahisi kuliko kuumbwa kwa kwanza. Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa, zikiwemo: Juz. 1 (2:28) na Juz.17 (22:66).

وَلِلَّهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ يَوْمَئِذٍ يَخْسَرُ الْمُبْطِلُونَ {27}

Na ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu. Na siku itaposimama Saa, siku hiyo watahasirika wenye batili.

وَتَرَىٰ كُلَّ أُمَّةٍ جَاثِيَةً ۚ كُلُّ أُمَّةٍ تُدْعَىٰ إِلَىٰ كِتَابِهَا الْيَوْمَ تُجْزَوْنَ مَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ {28}

Na utauona kila umma umepiga magoti. Kila umma utaitwa kwenye kitabu chake: Leo mtalipwa mliyokuwa mkiyatenda.

هَٰذَا كِتَابُنَا يَنْطِقُ عَلَيْكُمْ بِالْحَقِّ ۚ إِنَّا كُنَّا نَسْتَنْسِخُ مَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ {29}

Hiki kitabu chetu kinasema juu yenu kwa haki. Hakika Sisi tulikuwa tukiyaandika mliyokuwa mkiyatenda.

فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَيُدْخِلُهُمْ رَبُّهُمْ فِي رَحْمَتِهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْمُبِينُ {30}

Ama wale walioamini na wakatenda mema, Mola wao atawaingiza katika rehema yake. Huko ndiko kufuzu kulio wazi.

وَأَمَّا الَّذِينَ كَفَرُوا أَفَلَمْ تَكُنْ آيَاتِي تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَاسْتَكْبَرْتُمْ وَكُنْتُمْ قَوْمًا مُجْرِمِينَ {31}

Na ama wale waliokufuru: Kwani hamkuwa mkisomewa Aya zangu nanyi mkawa na kiburi, na mkawa watu wakosefu?