Aya 23 – 29: Musa
Maana
Maelezo kuhusiana na Musa yamepita mara kadhaa, tukiwa tunaashiria jina la sura na Aya iliyopita kila inapokuja Aya nyingine. Hivi sasa kimerudi kisa cha Musa na kitaendelea kurudi kwenye Aya za mbele.
Katika Juz. 16 (20:9 – 16) kifungu cha ‘kukaririka kisa’ tumebainisha sababu za kukaririka huku. Na hivi sasa tunaunganisha tuliyoyabainisha huko na hapa; kwamba sio mbali kuwa kila Aya, hata kama ikikaririka, huwa inatoa mwanga mpya uliofichika kwetu, kwa kuwa sisi hatukufikia utafiti wake au hatukuwa na uwezo wa kuutambua. Vyovyote iwavyo, jipya katika Aya hizi tulizo nazo sasa, ni kuwa zinamzungumzia mumin wa watu wa Firauni.
Na kwa hakika tulimtuma Musa pamoja na Ishara zetu na hoja zilizo wazi, kwa Firauni na Hamana na Qaruni,
Hamana ni waziri wa Firauni na Qaruni alikuwa tajiri mkubwa kuliko wote wakati wa Firauni. Inasemekana alikuwa waziri wa fedha wa utawala wa Firauni. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimtuma Musa kwa watu wote wa zama zake. Wamehusishwa kutajwa hawa watatu, kwa sababu wao ndio msingi wa ufisadi na chimbuko la upotevu. Kama wangeliamini hawa, basi wangeliamini wote.
Wakasema: Ni mchawi, mwongo mkubwa; sawa na walivyosema waliokuwa kabla yao na baada yao, kumwambia kila anyayewajia na ubainifu na hoja.
Basi alipowaletea Haki inayotoka kwetu, walisema: Waueni watoto wanaume wa wale waliomuamini na wawacheni hai wanawake wao.
Aliamrisha kuuliwa watoto wa kiume kwa kuwahofia na kuwabakisha wa kike kwa ajili ya kuwahudumia. Unaweza kuuliza: Firauni alitoa amri hii kabla ya kuzaliwa Musa. Je kuna makusudio gani ya kukaririka tena?
Baadhi ya wafasiri wamejibu kuwa Firauni alizuia kuuliwa watoto baada ya kuzaliwa Musa, lakini Musa alipotumwa na Mwenyezi Mungu, Firauni alirudia kuua. Kauli hii inahitaji kuthibitishwa. Sio mbali kuwa amri ya pili ya kuua ni kuendeleza ile amri ya kwanza; kwamba kuua kuendelee tu wala kusisimamishwe kwa hali yoyote.
Na haviwi vitimbi vya makafiri ila katika upotovu.
Yaani: “Na vitimbi viovu havimpati ila mwenyewe. Basi hawangoji ila desturi ya wa zamani.” Juz. 22 (35:43).
Na Firauni akasema: Niachieni nimuuwe Musa, naye amwite Mola wake!
Hii inaashiria kuwa badhi ya watu wa Firauni walimshauri asimuue Musa kwa kuhofia Mola wake atalipiza kisasi.
Firauni aliendelea kusema: “Hakika Mimi nachelea asije kubadilisha dini yenu, au akadhihirisha uharibifu katika nchi.
Firauni ni mzuri kwa vile yeye anasema, mimi ndiye mola wenu mkuu na mimi simjui Mungu mwingine kwenu zaidi yangu. Na Musa ni mharibifu kwa vile yeye ana mwito wa kuwakomboa watu kwenye utumwa wa watu wengine! Haya siyo mageni. Ndio mantiki ya viongozi wa mabavu kila wakati na kila mahali.
Na Musa akasema: Hakika Mimi najikinga kwa Mola wangu na Mola wenu anilinde na kila mwenye kiburi asiyeiamini Siku ya Hisabu.
Musa anajilinda kwa Mwenyezi Mungu asiwe na kiburi na kutomwogopa Mwenyezi Mungu na hisabu yake na adhabu yake. Kwa sababu mtu duni zaidi ni yule aliye na mambo haya mawili.
Na akasema mtu mmoja Muumini, katika watu wa Firauni, anayeficha Imani yake: Mtamuuwa mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Mwenyezi Mungu? Na hali amewajia na hoja zilizo wazi?
Haki huwa haikosi mtetezi, ijapokuwa ni kwaneno la ikhlasi linaloelekezwa kwa watu wa batili na upotevu. Huyu hapa mtu katika watu wa Firauni, aliyemwamini Mwenyezi Mungu kwa ukweli na yakini, lakini alificha imani yake, kwa kuhofia kuuliwa.
Firauni alipotaka kumfanyia shari Musa, imani halisi iliugusa moyo wake, kiasi cha kulipinga hilo na kulihadharisha, lakini kwa mfumo wa kiakili na kihekima, akasema: Amekosa nini mtu huyu mpaka akastahiki kuuliwa? Ni kwa vile tu amesema: Mola wangu ni Mwenyezi Mungu, akiwa na hoja mkataa zilizowaziba mdomo na kuwashinda; kama vile mkono mweupe na fimbo iliyomeza mliyokuwa mkiyazua?
Sheikh Maraghi, katika tafsiri yake, anasema, ninamnukuu: “Mtu mmoja mumin ni binamu yake Firauni, mrithi wake na mkuu wa polisi. Huyu aliokoka pamoja na Musa. Na ndiye aliyekusudiwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu:
وَجَاءَ مِنْ أَقْصَى الْمَدِينَةِ رَجُلٌ يَسْعَىٰ قَالَ يَا قَوْمِ اتَّبِعُوا الْمُرْسَلِينَ {20}
Ikumbukwe kwamba Sheikh Maraghi alipokuwa akifasiri sura Yasin alisema kuwa mtu huyu aliyekuja mbio kutoka mjini alikuwa katika zama za Isa; kama walivyosema hivyo wafasiri wengineo. Sasa ni nani aliyemfufua wakati wa Musa, ambapo kati yake na Isa kuna zaidi ya miaka 1200; kama walivyosema wanahistoria? Lakini wasiokosea ni wale maasum (waliohifadhiwa na makosa).
Na akiwa ni mwongo basi uwongo wake ni juu yake mwenyewe, mwacheni na uwongo wake na akiwa ni mkweli yatawafika baadhi ya hayo anayowaahidi; iwe mtamuua au mtamuacha. Alisema baadhi ya anayowaahidi na wala hakusema yote anayowaahidi, kwa sababu baadhi yanatosha kuangamiza.
Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi apindukiaye mipaka, mwongo mkubwa.
Mmedai kuwa yeye ni mwongo, basi mwacheni apate malipo ya uwongo. Hapa kuna ishara kuwa wasifu huu ni wa Firauni na kwamba yeye atapambana na malipo ya uwongo wake na kupaetuka kwake mipaka tu.
Enyi watu wangu! Leo mna ufalme, mmeshinda katika nchi; basi ni nani atakaye tusaidia kutuokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu kama ikitufikia?
Bado maneno yanatoka kwa mumin kuwaambia watu wake, watu wa Firauni. Maana yake ni kuwa, nyinyi hivi sasa mko katika amani na mnao ufalme ulioshinda. Basi neema hii aliyowaneemesha Mwenyezi Mungu, msiiondoe kwa kumuua anayesema Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu. Basi ni nani atakayetuokoa na uovu wake akitujia usiku au mchana?
Kwa ufupi ni kuwa mumin alimkinga Musa kwa njia nzuri na akawajadili maadui wa Mungu kwa hekima na mawaidha mazuri; kwanza alimwepusha Musa na makosa. Pili akawatishia maadui zake kwa hatari na madhara. Tatu akawakumbusha neema ya Mwenyezi Mungu kwao na akawahadhrisha wasiibadilishe na kufuru.
Kwa mfumo huu aliweza kubadilisha azma ya taghuti na kushikilia kwake kumuua Musa, mpaka Firauni akasema:
Siwapi rai ila ile niliyoiona, wala siwaongozi ila kwenye njia ya uwongofu.
Kauli hii ya Firauni inafanana na kuomba msamaha kutokana na yale aliyoyaazimia, kumuua Musa. Na hiyo ni kutokana na nasaha za mumin. Maana ni kuwa mimi sikutoa shauri ya kumuua Musa ila baada ya kufikiria vizuri; na sikutaka haya ila kwa masilahi yenu.
وَقَالَ الَّذِي آمَنَ يَا قَوْمِ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ مِثْلَ يَوْمِ الْأَحْزَابِ {30}
مِثْلَ دَأْبِ قَوْمِ نُوحٍ وَعَادٍ وَثَمُودَ وَالَّذِينَ مِنْ بَعْدِهِمْ ۚ وَمَا اللَّهُ يُرِيدُ ظُلْمًا لِلْعِبَادِ {31}
وَيَا قَوْمِ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ يَوْمَ التَّنَادِ {32}
يَوْمَ تُوَلُّونَ مُدْبِرِينَ مَا لَكُمْ مِنَ اللَّهِ مِنْ عَاصِمٍ ۗ وَمَنْ يُضْلِلِ اللَّهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ {33}
وَلَقَدْ جَاءَكُمْ يُوسُفُ مِنْ قَبْلُ بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا زِلْتُمْ فِي شَكٍّ مِمَّا جَاءَكُمْ بِهِ ۖ حَتَّىٰ إِذَا هَلَكَ قُلْتُمْ لَنْ يَبْعَثَ اللَّهُ مِنْ بَعْدِهِ رَسُولًا ۚ كَذَٰلِكَ يُضِلُّ اللَّهُ مَنْ هُوَ مُسْرِفٌ مُرْتَابٌ {34}
الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِ اللَّهِ بِغَيْرِ سُلْطَانٍ أَتَاهُمْ ۖ كَبُرَ مَقْتًا عِنْدَ اللَّهِ وَعِنْدَ الَّذِينَ آمَنُوا ۚ كَذَٰلِكَ يَطْبَعُ اللَّهُ عَلَىٰ كُلِّ قَلْبِ مُتَكَبِّرٍ جَبَّارٍ {35}