read

Aya 30 – 35: Mwenyezi Mungu Hadhulumu Waja

Maana

Na akasema yule aliyeamini: Enyi watu wangu! Hakika mimi nawahofia mfano wa siku za makundi. Mfano wa hali ya watu wa Nuh na A’di na Thamudi na wale wa baada yao.

Makusudio ya makundi hapa ni watu waliounda vikundi dhidi ya mitume wao; kwa dalili ya kauli yake: “Mfano wa hali ya watu wa Nuh na A’di na Thamudi na wale wa baada yao.”

Aliposema Firauni: ‘Wala siwaongozi ila kwenye njia ya uongofu’ yule mumin naye akasema: ‘mimi vile vile si kusema niliyowaambia ila kwa kuhofia yasiwapate maangamizi kama yalivyowapata wa mwanzo, pale walipowakadhibisha manabii wao.

Na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu waja, lakini wao wenyewe wanajidhulumu kwa kuwakadhibisha mitume na kuifanyia jeuri amri ya Mwenyezi Mungu.

Baada ya yule mumin kuwahadharisha na adhabu ya dunia, aliwahadharisha na adhabu ya Akhera kwa kusema:

Na enyi watu wangu! Hakika mimi nawahofia Siku ya kunadi.

Siku ya kunadi ni Siku ya Kiyama, ambapo watu watanadiwa kwa ukulele; kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

يَوْمَ يُنَادِ الْمُنَادِ مِنْ مَكَانٍ قَرِيبٍ {41}

“Siku atakaponadi mwenye kunadi kutoka mahali karibu” (50:41).

Siku mtakapogeuka kurudi nyuma mkijaribu kukimbia adhabu ya moto, lakini wapi! Hamtakuwa na wa kuwalinda kwa Mwenyezi Mungu.

Vipi mtaweza kumkimbia na hali yeye ndiye mwenye nguvu, kwenye jambo lake, hapingwi wala hazuiwi.

Na ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza, basi huyo hana wa kumwongoa.
Yaani atakayefuata njia ya upotevu basi Mwenyezi Mungu atampoteza; kama vile anayekunywa sumu, Mwenyezi Mungu atamuua tu, wala hutap- ata atakayemponesha na kumpa uhai.

Na alikwishawajia Yusuf zamani kwa dalili zilizo wazi, lakini nyinyi mliendelea katika shaka kwa yale aliyowaletea.

Yaani enyi wamisr! Yusuf aliwajia mababa zenu, wakatia shaka utume wake; kama hivyo nanyi mnatia shaka utume wa Musa. Katika Kamusi ya Kitabu kitakatifu, imeelezwa kuwa Yusuf ni jina la kiibrania (Hebrew) lenye maana ya anayezidisha. Mama yake alimwita hivyo, ili apate ziada ya mtoto mwingine. Naye alikufa akiwa na miaka 110

Mpaka alipokufa mkasema: Mwenyezi Mungu hataleta tena Mtume baada yake.

Hii inaashiria kuwa wao walifurahi kwa kufa Yusuf, kwa vile watakuwa huru na taklifa za Mwenyezi Mungu. Wakasema bila ya kujali, kwa msukumo wa matamanio kwamba Mwenyezi Mungu hatapeleka tena Mtume baada ya Yusuf mpaka Siku ya Mwisho.

Kama hivyo Mwenyezi Mungu humpoteza yule aliyepita kiasi mwenye shaka kuhusu Mwenyezi Mungu na haki. Mwenyezi Mungu anampoteza mwenye kupita kiasi, kwa sababu ametoka katika uongofu na akaingia kwenye upotevu kwa uchaguzi wake mbaya na upofu.

Wale ambao wanajadiliana katika Ishara za Mwenyezi Mungu bila ya dalili yoyote iliyowafikia.

Makusudio ya wale wanaojadiliana ni wale wenye kupita kiasi wenye shaka. Ishara za Mwenyezi Mungu ni dalili za umoja wake, unabii wa mananbii wake na hoja wazi. Maana ni kuwa wakosefu wanajibu hoja za Mwenyezi Mungu kwa matamanio yao na kuiga mababa zao.

Ni chukizo kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya walioamini kujadili wakosefu bila ya ujuzi wala mwongozo au kitabu.

Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu apigavyo chapa juu ya kila moyo wa jeuri anayejivuna.

Kiburi na kujidai ndio sababu hasa ya kupigwa chapa moyoni. Hilo limetegemezwa kwa Mwenyezi Mungu kwa vile Yeye ndiye aliyejaalia kiburi kuwa ndio sababu ya upofu wa moyo; sawa na alivyoujaalia ujinga kuwa ndio sababu ya kudangana na kuwa mbali na haki na akajaalia kusoma na kufanya utafiti ni sababu ya elimu na mwamko.

وَقَالَ فِرْعَوْنُ يَا هَامَانُ ابْنِ لِي صَرْحًا لَعَلِّي أَبْلُغُ الْأَسْبَابَ {36}

Na Firauni akasema: Ewe Hamana! Nijengee mnara ili nipate kuzifikia njia.

أَسْبَابَ السَّمَاوَاتِ فَأَطَّلِعَ إِلَىٰ إِلَٰهِ مُوسَىٰ وَإِنِّي لَأَظُنُّهُ كَاذِبًا ۚ وَكَذَٰلِكَ زُيِّنَ لِفِرْعَوْنَ سُوءُ عَمَلِهِ وَصُدَّ عَنِ السَّبِيلِ ۚ وَمَا كَيْدُ فِرْعَوْنَ إِلَّا فِي تَبَابٍ {37}

Njia za mbinguni ili nikamwone Mungu wa Musa. Na kwa hakika mimi bila ya shaka namjua kuwa ni mwongo tu. Na hivi ndivyo Firauni alivyopambiwa ubaya wa vitendo vyake, na akazuiliwa Njia. Na vitimbi vya Firauni havikuwa ila katika kuangamia tu.

وَقَالَ الَّذِي آمَنَ يَا قَوْمِ اتَّبِعُونِ أَهْدِكُمْ سَبِيلَ الرَّشَادِ {38}

Na yule ambaye aliamini alisema: Enyi watu wangu! Nifuateni, nitawaongoza njia ya uongofu.

يَا قَوْمِ إِنَّمَا هَٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا مَتَاعٌ وَإِنَّ الْآخِرَةَ هِيَ دَارُ الْقَرَارِ {39}

Enyi watu wangu! Hakika maisha haya ya dunia ni starehe yenye kupita tu, na hakika Akhera ndiyo nyumba ya daima.

مَنْ عَمِلَ سَيِّئَةً فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا ۖ وَمَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِنْ ذَكَرٍ أَوْ أُنْثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَٰئِكَ يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ يُرْزَقُونَ فِيهَا بِغَيْرِ حِسَابٍ {40}

Mwenye kutenda uovu hatalipwa ila sawa na huo, na mwenye kutenda wema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi, waruzukiwe humo bila ya hisabu.