Aya 69 – 78: Mlikuwa Mkifurahi
Maana
Je, Huwaoni wale ambao wanabishana katika Ishara za Mwenyezi Mungu wanageuziwa wapi?
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamwambia Mtume wake mtukufu akipinga ubishi wa kibatili wa washirikina, kuwa umeona ewe Muhammad jinsi washirikina na wapenda anasa wanavyozifumbia macho hoja mkataa na ubainifu ulio wazi juu ya ukuu wa Mwenyezi Mungu na utume wako? Na pia vile wanavyoikimbia haki na kwenda kwenye ujinga na upotevu wa kuabudu mawe?
Ufafanuzi zaidi wa Aya hii na ufupisho wake ni kauli ya Imam Ali (a.s.): “Mwenye kukithirisha mzozo wake kwa ujinga hudumu upofu wake na haki.”
Ambao wamekadhibisha Kitabu yaani Qur’ani na yale tuliyowatuma nayo Mitume wetu. Basi watakuja jua.
Siku hiyo uhakika utadhihirika na wakosefu wataiona adhabu yao, zitakapokuwa pingu shingoni mwao na minyororo, huku wanabururwa katika maji ya moto, kisha wataunguzwa Motoni.
Wataburuzwa kupelekwa motoni wakiwa wamefungwa minyororo, kinywaji chao kitakuwa maji ya moto na mikono itafungwa shingoni na utosi utakutanishwa na nyayo:
يُعْرَفُ الْمُجْرِمُونَ بِسِيمَاهُمْ فَيُؤْخَذُ بِالنَّوَاصِي وَالْأَقْدَامِ {41}
Tena wataambiwa: Wako wapi mliokuwa mkiwashirikisha badala ya Mwenyezi Mungu na mkiwaweka akiba ya wakati wa shida? Basi waiteni wawaitikie ikiwa nyinyi ni wakweli.
Watasema: Wametupotea, wala hatuwaoni hata athari yao. bali tangu zamani hatukuwa tukiomba kitu! Kumbe walikuwa ni mangati tu.
Hivyo ndivyo Mwenyezi huwapoteza makafiri, kwa sababu wameamua kufuata njia mbaya kwa hiyari yao, baada ya kukatazwa na wakafa kwenye uovu na kufuru na hali wameamriwa kutubia na kurejea kwa Mwingi wa maghufira Mwenye kurehemu. Mwenye kuingia mlango wa uovu, ajilaumu mwenyewe tu.
Tunatafuta Dunia Kwa Dini
Haya ni kwa sababu mlikuwa mkifurahi katika ardhi pasipo haki, na kwa sababu mlikuwa mkijishaua.
Wakifurahi kwa mambo duni ya dunia yanayoisha wala hawatilii umuhimu neema za daima za akhera zinazowapita. Lakini wasifa huu hauwahusu washirikina tu; bali unatuhusu sisi pia. Tofauti ni kuwa wao wanaikabili dunia wakiwa wanikana Akhera waziwazi na kwa ndani, lakini sisi tunaikabili dunia na kuipupia kwa kutumia imani ya Mwenyezi Mungu na Siku ya mwisho. Sasa ni lipi kati haya mawili linastahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu?
Ingieni kwenye milango ya Jahannamu, mdumu humo. Basi ni maovu yaliyoje makazi ya wanaotakabari!
Ataambiwa haya mwenye kutakabari na kila mwenye kuitumia dini na nchi kujinufaisha na akachezea akili za watu wasio na hatia; ni sawa ameyafanya hayo kwa makusudi au kutojua hakika na hali halisi. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
قُلْ هَلْ نُنَبِّئُكُمْ بِالْأَخْسَرِينَ أَعْمَالًا {103}
الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا {104}
Ulama wameafikana kwa kauli moja kwamba mjinga (asiyejua) kwa uzembe hana udhuru mbele ya Mwenyezi Mungu.
Basi subiri, hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli.
Imetangulia kwa herufi zake katika Aya 55 katika sura hii tuliyo nayo.
Na ama tukikuonyesha baadhi ya yale tuliyowaahidi au tukikufisha, lakini wao watarudishwa kwetu tu.
Maneno yanelekezwa kwa Muhammad (s.a.w.) kuhusiana na washirikina. Maana ni kuwa tunaweza tukawaadhibu duniani wale wanaokukadhibisha na kukuudhi wewe ukiwaona na tunaweza tukakuhitari ukaja kwetu kabla ya hayo. Katika hali zote hizo, marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu peke yake.
Aya inashiria kwamba mumin wa kweli anatakikana afurahi kwa yale yanayomridhisha Mwenyezi Mungu, awe na yakini na dini yake na afanye juhudi kadiri atakavyoweza kupiga vita ubatilifu na upotevu, kisha malipo amwachie Mwenyezi Mungu:
وَمَا رَبُّكَ بِغَافِلٍ عَمَّا يَعْمَلُونَ {132}
Na kwa hakika tuliwatuma Mitume kabla yako. Wengine katika hao tumekusimulia na wengine hatukukusimulia.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 6 (4:164). Tazama kifungu ‘Je, mitume wote ni wa mashariki?
Na haiwi Mtume alete Ishara yoyote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Makusudio ya ishara hapa ni muujiza. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hudhihirisha muujiza mikononi mwa mitume, kulingana na inavyotaka hekima na masilahi; sio kama wanavyotaka wenye kiburi na inadi.
Basi ikija amri ya Mwenyezi Mungu huhukumiwa kwa haki, na hapo wapotofu watapata hasara.
Hapo ni hapo Siku ya Kiyama; nayo ni siku mbaya sana kwa wabatilifu na siku njema sana kwa wenye haki.
اللَّهُ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَنْعَامَ لِتَرْكَبُوا مِنْهَا وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ {79}
وَلَكُمْ فِيهَا مَنَافِعُ وَلِتَبْلُغُوا عَلَيْهَا حَاجَةً فِي صُدُورِكُمْ وَعَلَيْهَا وَعَلَى الْفُلْكِ تُحْمَلُونَ {80}
وَيُرِيكُمْ آيَاتِهِ فَأَيَّ آيَاتِ اللَّهِ تُنْكِرُونَ {81}
أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنْظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ ۚ كَانُوا أَكْثَرَ مِنْهُمْ وَأَشَدَّ قُوَّةً وَآثَارًا فِي الْأَرْضِ فَمَا أَغْنَىٰ عَنْهُمْ مَا كَانُوا يَكْسِبُونَ {82}
فَلَمَّا جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُمْ بِالْبَيِّنَاتِ فَرِحُوا بِمَا عِنْدَهُمْ مِنَ الْعِلْمِ وَحَاقَ بِهِمْ مَا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ {83}
فَلَمَّا رَأَوْا بَأْسَنَا قَالُوا آمَنَّا بِاللَّهِ وَحْدَهُ وَكَفَرْنَا بِمَا كُنَّا بِهِ مُشْرِكِينَ {84}
فَلَمْ يَكُ يَنْفَعُهُمْ إِيمَانُهُمْ لَمَّا رَأَوْا بَأْسَنَا ۖ سُنَّتَ اللَّهِ الَّتِي قَدْ خَلَتْ فِي عِبَادِهِ ۖ وَخَسِرَ هُنَالِكَ الْكَافِرُونَ {85}