Aya 79 – 85: Mwenyezi Mungu Amewajaalia Wanyamahowa
Maana
Mwenyezi Mungu ndiye ambaye amewajaalia wanyamahowa ili muwapande baadhi yao na wengine muwale.
Wanyamahowa ni ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewatumikisha kwa ajili ya manufaa ya binadamu; kama vile kula na kupanda.
Amewahusu kuwataja, pamoja na kuwa neema zake hazina idadi, kwa kuungana kwake na maisha ya waarabu wakati huo, na mpaka sasa bado wana mahitaji mengi sana katika baadhi ya miji.
Na katika hao mna manufaa mengine; kama vile kunufaika na manyoya yake na ngozi zake. Na manapata kwao haja zilizo vifuani mwenu; kama vile kubeba mizigo mizito na bidhaa mbalimbali kutoka mji mmoja hadi mwingine. Na mnachukuliwa juu yao na juu ya majahazi.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6:142) na Juz. 14 (16:66).
Na anawaonyesha ishara zake, basi ni ipi katika ishara za Mwenyezi Mungu mtaikataa?
Yaani mtaikataa pamoja na hoja na dalili? Ndio walikata kwa vitendo ishara za Mwenyezi Mungu na hukumu zake. Kwa sababu mema kwao ni maovu na maovu kwao ni mema.
Je, hawatembei katika ardhi wakaona ulivyokuwa mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? Walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko wao na wakilima ardhi.
Historia ya watu wa ardhi imejaa mazingatio na mawaidha kwa mwenye kuzingatia na kupata somo. Ni uma ngapi zilifikia ukomo wa starehe na maendeleo, lakini walipopetuka mipaka, Mwenyezi Mungu aliwakamata kwa dhulma zao kwa mshiko wa Mwenye nguvu na uweza. Basi hayakufaa waliyokuwa wakiyachuma; kama vile utawala, mali na makasri na ngome walizozijenga. Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (12:109), Juz. 17 (22:46) na Juz 21 (30:9).
Basi walipowajia Mitume wao kwa dalili zilizo wazi wakifurahia elimu waliyokuwa nayo.
Makusudio ya furaha hapa ni kughurika. Na makusudio ya elimu ni sababu za utajiri, yaani elimu ya kuzalisha chakula na mavazi. Hilo linaashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko wao na wakilima ardhi.’ Qarun naye alipoambiwa: “Na utafute kwa aliyokupa Mwenyezi Mungu makazi ya Akhera” Alijibu: “Nimepewa haya kwa sababu ya elimu” Juz 20 (28:77-78)
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwatuma mitume, kwa hoja mkataa, wakati uliopita kwenye umma zilizokuwa na utajiri; kama vile viwanda n.k. Wakaghurika kwa sababu hizi au kwa elimu na wakawafanyia maskhara manabii wa Mwenyezi Mungu na vitabu; sawa na mashirika ya leo yanayohodhi kila kitu ambayo yanaikataa haki na ubinadamu na kudharau thamani yake na amani ya mataifa
Na yakawazunguka waliyokuwa wakiyafanyia stihzai.
Mwenyezi Mungu aliwaadhibu kwa kupituka kwao mipaka na yakawasibu yale waliyokuwa wakiyadharau. Huu ndio mwisho wa kila mwenye kupituka mipaka na kuasi, hata kama muda utarefuka kiasi gani.
Walipoiona adhabu yetu wakasema: Tumemwamini Mwenyezi Mungu peke yake na tumekataa tuliyokuwa tukimshirikisha naye.
Walipokuwa katika amani ya Mwenyezi Mungu walimkufuru, lakini walipoiona adhabu yetu wakasema tumeamini, lakini imani yao haikuwa ni yenye kuwafaa walipoiona adhabu yetu. Kwa sababu hii sio imani yoyote ispokuwa ni kukimbia adhabu, lakini watakimbia wapi?
Ni desturi ya Mwenyezi Mungu iliyopita kwa waja wake, ambayo ni kuwa Mwenyezi Mungu anasikiliza toba na kuzikubali katika nyumba ya taklifa na matendo sio katika nyumba ya hisabu na malipo.
Na hapo waliokufuru watapata hasara.
Kila mkosefu ni mwenye hasara na mtupu.