read

Aya 9 – 12: Mwenyezi Mungu Ameumba Ardhi

Maana

Sema: Hivyo nyinyi mnamkataa aliyeumba ardhi katika siku mbili, na mnamfanyia washirika? Huyo ndiye Mola wa walimwengu wote.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu hakukuwa na wakati wala mahali. Hakukuwa na kitu chochote ispokuwa Mwenyezi Mungu tu mmoja mwenye nguvu.
Kwa hiyo basi makusudio ya siku mbili yatakuwa ni mikupuo miwili au nyakati mbili, kama ilivyosemekana. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:53). Kutokana na haya, tunataja waliyosema baadhi ya wafasiri: “Hakika mfumo wa Qur’ani unatofautiana na mifumo yote.

Inapoashiria suala lolote la kielimu hailionyeshi kama wanavyolionyesha wataalamu wa sayansi kwa ulinganishi na ufafanuzi; huwa mara nyingine hulileta kwa ishara, au alama za siri (code) au kwa kudokeza kwa neno ambalo huenda likampita anayelisikia wakati ule. Lakini inajua kuwa historia na mustakbali utalifafanua neno hilo na kulithibisha kwa uwazi.”

Hakika hii ilikuja mdomoni mwa Ibn Abbas tangu karne 14 zilizopita, pale aliposema: “Msifasiri Qur’ani, zama zitaifasiri” yaani msizame sana katika Aya za kilimwengu (kisayansi), kwa sababu maendeleo ya elimu itafichua siri zake.

Na akaweka humo milima juu yake.

Mfano wakenikauliyakeMwenyeziMungu:

وَأَلْقَىٰ فِي الْأَرْضِ رَوَاسِيَ أَنْ تَمِيدَ بِكُمْ {15}

“Na akaweka katika ardhi milima ili isiyumbe nanyi.” Juz. 14 (16:15)

Na akabarikia humo na akakadiria humo chakula chake katika siku nne. Ni sawa kwa wanaouliza.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alibariki humo mimea, petroli n.k. Makusudio ya kukadiria chakula chake ni kuwa vyote vilivyo katika ardhi viko kwa kiasi cha mahitaji ya waliohai wote, kadiri idadi yao itakavyokuwa.

Kundi la wafasiri wamesema kuwa siku mbili zilizotajwa mwanzo ni kati- ka jumla ya siku nne; yaani kuumbwa ardhi na kukadiriwa chakula chake kulitimia ndani ya siku nne katika siku za Mwenyezi Mungu.

Makusudio ya wenye kuuliza hapa ni kila mwenye kuhitajia chakula. Na usawa ni kuwa Mwenyezi Mungu hakujaalia manufaa ya ardhi kwa jinsia fulani au taifa fulani tu; bali viumbe wote wako sawa katika riziki yake na fadhila yake. Akipatikana mwenye njaa basi ni kwa dhulma ya mwenye nguvu dhidi ya mnyonge. Tazama Juz. 8 (7:54-56) kifungu ‘Mwenyezi Mungu ameitengeneza ardhi na binadamu akaiharibu’

Nini Ufumbuzi Wa Tatizo La Njaa?

Kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘na akakadiria humo chakula chake,’ tutaashiria kauli ya wale waliosema kuwa sababu ya kwanza ya tatizo la njaa ulimwenguni ni wingi wa watu wanaozidi siku baada ya siku kufikia kutotosha chakula cha ardhi na heri zake; na kwamba hakiendani na ongezeko la uzazi. Kisha wakatofautiana kuhusu njia ya kutatua tatizo hili.

Kuna waliosema ufumbuzi ni vita vya maangamizi vitavyowaua watu wengi ili upatikane uwiano wa idadi ya watu na uzalishaji wa chakula. Fikra hii wameiunga mkono wenye viwanda vya silaha na walanguzi wa vyakula wanaotafuta utajiri kwa kukandamiza mailioni ya watu.

Wengine nao wakasema, kama sio vita basi kuwe na maradhi ya kuambukiza. Kisha ikaenea rai ya tatu ya kupanga uzazi. Hakuna neno kwa rai hii, kwa sababu kupanga uzazi ni haki ya kimaumbile na kisharia kwa kila mtu, kwa sharti ya kupanga kabla ya kupatikana uzazi; yaani kabla ya tone la manii halijatua kwenye mfuko wa uzazi kwa ajili ya kutengeneza mtoto.

Ama ile rai ya kwanza, inatosha tu kuwa haifai kutokana na walioitoa – wafanya biashara ya silaha na wenye mashirika ya kilanguzi kwenye mataifa masikini.

Sababu kubwa ya tatizo la njaa, inatokana na nguvu ya shari kwenye kheri za ardhi na kuzihodhi, anasa za wachache zinazotokana na kuwakandamiza wengi, kuangamiza mazao kwa ajli ya kulinda soko la kupandisha bidhaa, kutupa maelfu ya tani ya kemikali kwenye vijiji na mashamba ya Vietnam na kwengineko na kuielekeza elimu kwenye uzalishaji wa silaha.

Lau elimu ingeelekezwa kwenye uzalishaji wa usalama tu, ingelitosha kuzidi heri za ardhi kwa watu na riziki zingelikuwa kama mchanga. Jarida la UNESCO linaandika utafiti uliosema: Gharama za kombora moja tu kubwa inatosha kujenga Hospitali 75, kila hospitali moja ikiwa na vitanda 100, vikiwa na mahitaji yake yote. Au kutosha kununua majembe 50,000 ya kukokotwa, yanayoweza kulima mamilioni ya heka badala ya kulima makombora ya kuangamiza. Serikali ya Marekani imetumia $ 400, Bilioni kwenye vita vya Vietnam kabla ya kumalizika.1

Je, mabilioni yote haya si katika heri za ardhi na baraka zake? Lau yangelitumika katika kilimo si yangelitosha kulima mapori yote na hata bahari na kwenye sayari nyingine? Watu wote ardhini wangeliishi maisha ya raha.

Zaidi ya hayo, lau ingelikuwa kweli kauli ya aliyesema kuwa watu wamezidi mahitaji yao ardhini, maana yake ingelikuwa Mwenyezi Mungu hakupangilia vizuri makadirio na makisio, na kwamba Yeye anakosea mahisabu ya wakazi wa ardhini kila wakati unavyozidi kupita au kuwa Yeye anakosea kukadiria mahitaji ya chakula! Mwenyezi Mungu Mtukufu ametukuka na ametakata na wayasemayo wajinga.

Tatizo la njaa duniani haliwezi kutatuka kwa vita, maradhi ya kuambukiza wala kwa kupanga uzazi. Kutakua na faida gani ya yote haya ikiwa katika watu kuna dhalimu na mwenye kudhulumiwa na mlaji na mwenye kuliwa?

Ufumbuzi pekee wa tatizo hili ni kuondoa vikwazo baina ya mtu na nyenzo za maisha, kuitumia vizuri ardhi kuzalisha chakula na mavazi na kukidhi mahitaji ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kisha akaielekea mbingu, na ilikuwa moshi, akaiambia hiyo na ardhi: Njooni, kwa hiari au kwa nguvu! Vyote viwili vikasema: Tumekuja nasi ni watiifu.

Kusema ‘tumekuja nasi ni watiifu’ ni kinaya cha uweza wa Mwenyezi Mungu na jinsi ulimwengu unavyofuata amri yake. Aya inaashiria kuwa anga kabla ya kuumbwa nyota ilikuwa na kitu kama moshi.

Basi akazifanya mbingu saba kwa siku mbili.

Mbingu saba ni anga za aina saba za ulimwengu na wala sio nyota saba Tazama Juz. 18 (23:12-17). Kifungu ‘maana ya mbingu saba.’ Ama kuhusu siku mbili ni mikupuo miwili au nyakati mbili, kama ilivyosemekana.

Na akaipangia kila mbingu mambo yake.

Yaani ameumba katika kila mbingu nyota na vinginevyo ambavyo anayevijua ni Yeye ti.

Na tukaipamba mbingu ya dunia kwa mataa.

Ambayo ni sayari zinazoangaza kama taa.

Na kwa ulinzi.

Mwenyezi Mungu anazihifadhi sayari katika kuendelea kwake na mfumo mmoja.

Hayo ndio makadirio ya Mwenyezi nguvu, Mwenye Kujua.

‘Hayo’ ni hayo yaliyotangulia ya kuumbwa ardhi na manufaa yake, kuumbwa mbingu na kupambwa kwake na kuhifadhiwa kwake. Hayo hayawi ispokuwa kutoka kwa mwenye uweza anayepangilia vizuri mambo na mwenye ujuzi.

Haya ndio tuliyo nayo katika fahamu na elimu ya kufasiri Aya hizi. Tunayataja kwa kujichunga tukiwa na imani na Mwenyezi Mungu na uweza wake na kwa kila ghaibu aliyoiashiria katika Kitabu chake kwa tamko tusilolijua maana yake kwenye njia yake wala kutambua uhakika wa siri yake.

Kama tukitaka ziada ya maarifa hatupati ispokuwa kunakili kutoka katika vitabu vya wataalamu, ambapo wao hawaleti dalili za kuthibitisha au kukanusha ispokuwa mara chache.

Anayetaka maelezo zaidi ya kauli zao na arejee kwenye kitabu Alkawnul-a’jib (ulimwengu wa ajabu) cha Hafidh Twawqan, Maallah fis samai (Pamoja na Mwenyezi Mungu katika mbingu) cha Ahmad Zakiy na vinginevyo.

فَإِنْ أَعْرَضُوا فَقُلْ أَنْذَرْتُكُمْ صَاعِقَةً مِثْلَ صَاعِقَةِ عَادٍ وَثَمُودَ {13}

Basi wakipuuza, sema: Nawahadharisha ukelele mfano ukelele wa A’di na Thamudi.

إِذْ جَاءَتْهُمُ الرُّسُلُ مِنْ بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا اللَّهَ ۖ قَالُوا لَوْ شَاءَ رَبُّنَا لَأَنْزَلَ مَلَائِكَةً فَإِنَّا بِمَا أُرْسِلْتُمْ بِهِ كَافِرُونَ {14}

Walipowafikia Mitume mbele yao na nyuma yao wakawaambia: Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu! Wakasema: Angelitaka Mola wetu bila ya shaka angeliwateremsha Malaika. Basi sisi hakika tunayakataa hayo mliyotumwa.

فَأَمَّا عَادٌ فَاسْتَكْبَرُوا فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَقَالُوا مَنْ أَشَدُّ مِنَّا قُوَّةً ۖ أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّهَ الَّذِي خَلَقَهُمْ هُوَ أَشَدُّ مِنْهُمْ قُوَّةً ۖ وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يَجْحَدُونَ {15}

Ama kinaA’di walitakabari katika ardhi bila ya haki, na wakasema: Nani aliye na nguvu zaidi kuliko sisi? Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi Mungu ambaye amewaumba ni Mwenye nguvu zaidi kuliko wao? Na wao wakawa wanazikataa Ishara zetu!

فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا صَرْصَرًا فِي أَيَّامٍ نَحِسَاتٍ لِنُذِيقَهُمْ عَذَابَ الْخِزْيِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَخْزَىٰ ۖ وَهُمْ لَا يُنْصَرُونَ {16}

Basi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku za nuhusi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwahizi katika uhai wa duniani, na bila ya shaka adhabu ya Akhera ina hizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa.

وَأَمَّا ثَمُودُ فَهَدَيْنَاهُمْ فَاسْتَحَبُّوا الْعَمَىٰ عَلَى الْهُدَىٰ فَأَخَذَتْهُمْ صَاعِقَةُ الْعَذَابِ الْهُونِ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ {17}

Na ama Thamudi tuliwaongoza, lakini walistahabu upofu kuliko uwongofu. Basi uliwachukua ukelele wa adhabu ya kuwafedhehi kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma

وَنَجَّيْنَا الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ {18}

Na tukawaokoa wale ambao wameamini na wakawa na takua.
  • 1. Haya ni katika miaka ya 70. Je hivi sasa Marekani imetumia Matirilioni mangapi ya dola huko Afghanistan na Iraq? Mtarjum