read

Aya 19 – 24: Masikio Yao Na Macho Yao Yatawashuhudia

Maana

Na siku watakapokusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu kwenye Moto, nao watazuiliwa.

Aya hizi tulizo nazo zinaungana na Aya iliyopita inayosema: ‘Basi wakipuuza, sema: nawahadharisha ukelele mfano ukulele wa A’di na Thamudi.’ Yaani pia waambie ewe Muhammad kuwa Malaika wa adhabu watawapeleka wakosefu kwenye Jahannam kwa nidhamu.

Atakayechelewa watamkemea na atakayejaribu kukimbia watamzuia. Makusudio ni kuwa hawana pakukimbia.

Hata watakapoufikia Moto yatawashuhudia masikio yao, na macho yao na ngozi zao kwa waliyokuwa wakiyatenda.
Hakuna kitu Siku ya Mwisho ispokuwa hisabu na malipo. Baadhi ya Aya za Qur’ani, ikiwemo hii tuliyo nayo,zinafahamisha kwamba Mwenyezi Mungu hatamwaadhibu mkosefu siku hiyo mpaka amkinaishe kuwa ana dhambi na anastahili adhabu.

Hii ni miongoni mwa tofauti zilizoko baina ya hakimu wa duniani anayetoa hukumu yake kwa hali yoyote iwayo; awe mwenye kuhukumiwa amekinai kuwa kweli amekosea au la, na hukumu ya Mwenyezi Mungu huko Akhera; ambapo Mwenyezi Mungu kesho hatatoa hukumu mpaka mhukumiwa akinai kuwa anastahili adhabu.

Kwa ajili hii ndio kutakuwa na ushahidi mwingi dhidi ya mkosefu. Wachukuzi wa dini watashuhudia kuwa walimfikishia halali ya Mwenyezi Mungu na haramu yake, Malaika watatoa ushahidi kua aliasi na akafanya jeuri na kitabu cha matendo yake kitasajili kila kauli na kitendo. Ikiwa hatatosheka, ngozi yake itashuhudia kuwa iligusa haramu, kama zina na utangulizi wake, masikio yatatoa ushahidi kuwa yalisikia haki na yakaikataa na macho nayo yatatoa ushahidi kuwa yaliona dalili za umoja wa Mungu yakazikataa na mengineyo.

Aya inaashiria maana ya ndani yakuwa sharti la shahidi ni kutopendelea. Pengine mkosefu anaweza akatuhumu kwamba wafikisha dini na Malaika wanaweza kuwa upande wa Mwenyezi Mungu kwa vile wanafanya mambo kwa amri yake. Ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akaleta ushahidi wa mtu mwenyewe binafsi ili kuondoa tuhuma hii hata kama si ya kweli.

Kuna Hadith isemayo kuwa mja kesho atamwambia Mola wake: Je, hukunikataza dhulma? Atajibiwa: ndio! Basi atasema: Mimi sitakubaliana na ushahidi ispokuwa ushahidi wa nafsi yangu. Basi hapo Mwenyezi Mungu Mtukufu ataviamuru viungo vitoe ushahidi. Mja mwenye dhambi atasema: Potoleeni mbali! Mara ngapi nimewapinga!

Na wataziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia?

Kauli yao hii inaonyesha kuwa baadhi wa wakosefu hawatakubali ushahidi wa wafikishaji dini na wa Malaika na kwamba wao watafikiria kuwa kukataa kwao huku kutawafaa, lau si Mwenyezi Mungu kuwawekea ushahidi wao wenyewe.

Zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu ambaye ametamkisha kila kitu! Na Yeye ndiye aliyewaumba mara ya kwanza, na kwake Yeye mtarejeshwa.

Viungo vyao duniani vinatamka kwa lugha ya kihali na kushuhudi hekima na mpangilio uliomo duniani kwamba Mwenyezi Mungu ndiye mwanzilishi na mrejeshaji. Na akhera vitatamka hivyo hivyo kwa uwazi kabisa. Wametofautiana wafasiri katika namna ya ushahidi wa viungo kesho.

Kuna wanaosema kuwa kutajitokeza alama za kuonyesha makosa yaliyofanyika. Wengine wakasema kuwa Mwenyezi Mungu atavitamkisha hasa kiuhakika. Hii ndio kauli iliyo wazi, kwa sababu dhahiri ya Aya inaonyesha hivyo, na akili hailikatai hilo.

Na hamkuwa wenye kujificha hata masikio yenu, na macho yenu, na ngozi zenu, zisiwashuhudie. Lakini mlidhani kwamba Mwenyezi Mungu hayajui mengi katika mliyokuwa mkiyatenda.

Makusudio ya kudhani hapa ni kuitakidi. Yaani mliamini enyi wakosefu kuwa mnafanya makosa kujificha mkihofia watu na sio kumhofia Mwenyezi Mungu, kwamba hajui mnayoyafanya kwa kujificha, na kwamba viungo vyenu havitawafichua siku ya hisabu.

Na hiyo dhana yenu mliyokuwa mkimdhania Mola wenu, ime- waangamiza; na mmekuwa miongoni mwa waliopata hasara.

Itikadi ya ubatilifu ndiyo iliyowapeleka kwenye Jahannam na ni mrejeo mabaya. Hii vile vile inalingana na wale wanaoiamini Akhera kinadharia na kuikana kimatendo; pale wanapojificha na watu na hawajifichi na Mwenyezi Mungu.
Bali hawa ni wabaya zaidi kuliko wale wanaopinga ufufuo na uweza wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu wamemuasi Mwenyezi Mungu wakiwa na uhakika kuwa yuko nao akisikia na kuona; na kwamba hakifichiki kwake chochote katika mbingu na ardhi.

Basi wakisubiri Moto ndio makazi yao. Na wakitoa udhuru hawakubaliwi.

Wakivumilia moto wakosefu basi ndio sawa na ndio makazi yao wala hawataokoka. Na wakiomba radhi kwa Mwenyezi Mungu hawaridhii.” Na wakiomba msaada watapewa maji kama mafuta yaliyotibuka yanayobabua nyuso. Kinywaji kibaya kilioje na mahali pabaya palioje pa kupumzika!” Juz. 15 (18:29).

وَقَيَّضْنَا لَهُمْ قُرَنَاءَ فَزَيَّنُوا لَهُمْ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَحَقَّ عَلَيْهِمُ الْقَوْلُ فِي أُمَمٍ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِهِمْ مِنَ الْجِنِّ وَالْإِنْسِ ۖ إِنَّهُمْ كَانُوا خَاسِرِينَ {25}

Na tukawawekea marafiki, na wakawapambia yaliyo mbele yao na nyuma yao. na ikawathibitikia kauli wawe pamoja na uma zilizopita kabla yao, miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa ni wenye kuhasirika.

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَسْمَعُوا لِهَٰذَا الْقُرْآنِ وَالْغَوْا فِيهِ لَعَلَّكُمْ تَغْلِبُونَ {26}

Na wale ambao wamekufuru walisema: Msiisikilize Qur’ani hii, na timueni zogo, huenda mkashinda.

فَلَنُذِيقَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا عَذَابًا شَدِيدًا وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَسْوَأَ الَّذِي كَانُوا يَعْمَلُونَ {27}

Basi wale ambao wamekufuru hapana shaka tutawaonjesha adhabu kali, na hapana shaka tutawalipa malipo ya mabaya zaidi waliyokuwa wakiyafanya.

ذَٰلِكَ جَزَاءُ أَعْدَاءِ اللَّهِ النَّارُ ۖ لَهُمْ فِيهَا دَارُ الْخُلْدِ ۖ جَزَاءً بِمَا كَانُوا بِآيَاتِنَا يَجْحَدُونَ {28}

Hayo ndiyo malipo ya maadui wa Mwenyezi Mungu - Moto! Humo watakuwa na nyumba ya kudumu, ndiyo malipo yao kwa sababu walikuwa wakizikataa Ishara zetu.

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا رَبَّنَا أَرِنَا اللَّذَيْنِ أَضَلَّانَا مِنَ الْجِنِّ وَالْإِنْسِ نَجْعَلْهُمَا تَحْتَ أَقْدَامِنَا لِيَكُونَا مِنَ الْأَسْفَلِينَ {29}

Na wale ambao wamekufuru watasema: Mola wetu! Tuonyeshe waliotupoteza miongoni mwa majini na tuwaweke chini ya miguu yetu, wapate kuwa miongoni mwa walio chini kabisa.