Aya 25 – 29: Waliokufuru Walisema Msisikilize Qur’ani
Maana
Na tukawawekea marafiki, na wakawapambia yaliyo mbele yao na nyuma yao.
Makusudio ya yaliyo mbele yao ni dunia na balaa yake, na ya nyuma yao ni Akhera ambayo kwa wapinzani ni uzushi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewaandalia mataghuti marafiki wabaya wanaowavutia na maovu na kuwaweka mbali na mema.
Unaweza kuuliza: ikiwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyewapangia watakaowahadaa kwenye upotevu na maasi, basi si itakuwa ni dhulma kuwaadhibu na kusema: ‘Basi ikiwathibitikia kauli;’ yaani adhabu.
Jibu: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewafanyia hivyo baada ya wao wenyewe, kwa uchaguzi wao mbaya, kufuata njia ya upotevu. Hilo amelifafanua Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliposema:
وَمَنْ يَعْشُ عَنْ ذِكْرِ الرَّحْمَٰنِ نُقَيِّضْ لَهُ شَيْطَانًا فَهُوَ لَهُ قَرِينٌ {36}
Pia akasema:
فَلَمَّا زَاغُوا أَزَاغَ اللَّهُ قُلُوبَهُمْ ۚ{5}
Hayo yamekwishaelezwa huko nyuma mara kadhaa.
Na ikawathibitikia kauli wawe pamoja na uma zilizopita kabla yao, miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa ni wenye kuhasirika.
Waliasi na wakafanya uovu, wakastahili adhabu, sawa na walivyostahili mfano wao katika umma zilizopita. Aya hii inafahamisha kuwa majini wana umma na vizazi, wana mitume na manabii; na miongoni mwao kuna wema na wengine waovu, sawa na watu.
Na wale ambao wamekufuru walisema: Msiisikilize Qur’ani hii, na timueni zogo, huenda mkashinda.
Mataghuti walishangaa walipoona athari ya Qur’ani na inavyoatwala kwenye nafsi za watu; wakawa wamedangana hawajui wafanye nini baada ya kushindwa kukabili hoja kwa hoja. Kisha wakaafikiana waipige vita kwa mambo yasiyosawa – waipe sifa ya uchawi na vigano na waifanyie vurugu. Wakaona kuwa hiyo ndiyo njia iliyobaki ya kuishinda.
Hii ya kufanya vurugu inafahamisha kukubali kwao kushindwa, na kwamba Qur’ani ni ngome ya Mwenyezi Mungu iliyoshinda fikra zote za bianadamu, wakati wote.
Basi wale ambao wamekufuru hapana shaka tutawaonjesha adhabu kali, na hapana shaka tutawalipa malipo ya mabaya zaidi waliyokuwa wakiyafanya.
Makosa yanagawanyika sehemu mbili: Kuna yale mabaya na yale yaliyo mabaya zaidi. Vile vile malipo kwa sababu:
مَنْ عَمِلَ سَيِّئَةً فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا ۖ {40}
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja mabaya zaidi waliyoyafanya ili kubainisha kuwa malipo nayo yatakuwa mabaya zaidi, sawa na matendo yao.
Hayo ndiyo malipo ya maadui wa Mwenyezi Mungu - Moto! Humo watakuwa na nyumba ya kudumu, ndiyo malipo yao kwa sababu walikuwa wakizikataa Ishara zetu.
Hayo ni ishara ya hayo malipo ya mtendo mabaya zaidi ambayo ni kudumu katika moto wa Jahannam. Kudumu huku, Mwenyezi Mungu amekufanya ni malipo ya kila mpinzani mwenye inadi na mshirikina, mambo ambayo hayana udhuru wowote kabisa.
Ujinga unaweza kuwa ni udhuru, lakini sio katika shirki na kupinga. Kwa sababu dalili za umoja wa Mwenyezi Mungu na utukufu wake hazikujificha, ziko waziwazi. Kuzijua kunahitaji kuangalia kusikokuwa kwa kuiga au kufuata mapenzi ya moyo.
Na wale ambao wamekufuru katika wadhaifu watasema: Mola wetu! Tuonyeshe waliotupoteza miongoni mwa majini na watu katika wale waliofuatwa, tuwaweke chini ya miguu yetu, wapate kuwa miongoni mwa walio chini kabisa.
Walimuomba Mwenyezi Mungu awaletee wale waliowapoteza katika mashetani watu na majini ili wawakanyage na wawe sehemu ya ndani kabisa ya Jahannam, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekwishawafanyia mabaya na mabaya zaidi.pale alipomkamata kila mmoja kwa dhambi yake
إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنْتُمْ تُوعَدُونَ {30}
نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنْفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ {31}
نُزُلًا مِنْ غَفُورٍ رَحِيمٍ {32}
وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِمَّنْ دَعَا إِلَى اللَّهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ {33}
وَلَا تَسْتَوِي الْحَسَنَةُ وَلَا السَّيِّئَةُ ۚ ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِي بَيْنَكَ وَبَيْنَهُ عَدَاوَةٌ كَأَنَّهُ وَلِيٌّ حَمِيمٌ {34}
وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ {35}
وَإِمَّا يَنْزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّهِ ۖ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ {36}