read

Aya 16 -21: Tunawaamrisha Wapenda Anasa Wake

Lugha

Neno ‘mutraf,’ambalo tumelifasiri kwa neno wapenda anasa, lina maana ya wale ambao wanastarehe watakavyo.

Maana

Nilipofikia kufasiri Aya hii (tunawaamrisha watanasi wake), nilikumbuka swali nililoulizwa na mmoja wa mahatibu wa Iraq akisema: Kwa nini unawatukana wapenda anasa kwenye vitabu vyako? Nami nikamuuliza: Kwanini wewe unawatetea? Je, wewe ni mmoja wao? Au ni kwa vile wao ni mawalii wa neema zako? Basi akarudi nyuma na swali lake na akaomba msamaha. Hili limenifanya niieleze Aya hii kwa mfumo ufuatao:

1. Mbali ya neno ‘utajiri,’ neno ‘wapenda anasa’ pamoja na mnyumbuliko wake limekuja mara nane katika Qur’an; kama ilivyoelezwa katika Murshid. Katika Nahjulbalagha neno hili limeelezwa mara nyingi. Halikutajwa neno wapenda anasa ila pamoja na shutuma.

2. Watu wa Lugha wamesema: Neno Taraf katika mnyumbuliko wake linatumika hivi: Amejitanaasi mtu, kwa maana ya kujineemesha. Ameitanasi mali, kwa maana ya kuifuja. Pia neno hilo linakuwa kwa maana ya uovu na kiburi. Haya ndio maelezo yake kilugha. Ama sifa yake iliyotajwa katika Qur’an na kwengineko ni: Kughafilika na Mwenyezi Mungu, kuwafanyia uovu waja wa Mwenyezi Mungu, kuifanyia kiburi amri ya Mwenyezi Mungu na kuwapiga vita mawalii wa Mwenyezi Mungu. Vile vile kujifaharisha kwa wingi, kujiona, unyanyapaa na mengine mengi ya shutuma; isipokuwa yule aliyehurumiwa na Mungu na akajihurumia mwenyewe.

3. Tunapotaka kuangamiza mji, huwaamrisha wapenda anasa wake, lakini hufanya maovu humo; basi hapo kauli huakikika katika mji huo na tukauangamiza maangamizo makubwa.

Linaoamriwa ni uadilifu na twaa; yaani tunawamrisha uadilifu na utiifu. Wafasiri wametaja njia nne katika maana ya Aya hii. Yenye nguvu zaidi ni ile inayosema kuwa Mwenyezi Mungu amelitumia neno wapenda anasa kwa watu wote wa mji, katika mtindo wa kutumia sehemu kwa maana ya yote.

Mfano huu katika maneno ya waarabu unatumika sana, ikiwa hiyo sehemu ni muhimu zaidi; kama jicho katika mwili, wamelitumia kwa mstari wa mbele katika jeshi; kwa sababu jicho ni kiungo muhimu katika mwili1
Kwa kuwa wapenda raha ni wepesi zaidi na wajasiri wa kufanya maasi kuliko wengine, ndio ikafaa kulitumia neno hilo kwa watu wote wa mji; kama linavyotumika jicho kwa mtu.

Kwa hiyo basi maana ya Aya yanakuwa kwamba Mwenyezi Mungu hawaangamizi watu wa mji ila wakistahili hilo baada ya kuwekewa hoja kwa kutumwa mtume awaamrishe kheri, kuwakataza uovu, kuwahadharisha na uhalifu na maasi. Wakifanya uovu na kutoka kwenye utiifu, basi linahakika neno la adhabu juu yao na Mwenyezi Mungu huwateremshia maangamizi.

Ni kweli maana haya yanawafikiana na matamshi ya Aya, wala hayakataliwi na akili, lakini sisi tutaifasiri kwa njia njingine; kama ifuatavyo: Jamii yoyote iliyo na wapenda anasa, kwa maana tuliyoyataja, basi ni jamii inayoishi kwenye nidhmu ya ufisadi na dhulma. Kwani kuweko kwao ni sawa kabisa na kuweko saratani katika mwili.

Wa kulaumiwa kwanza kabisa kwa kupatikana wafisadi ni jamii yenyewe; kwa vile haikusimama kidete kuwapinga au angalu kutowaunga mkono; bali wanawabatiza majina ya waheshimiwa, kuwatukuza, kuwapa kura na kuwapa uongozi.

Hapa ndio inakuwa jamii yenyewe ni mshiriki kamili wa wapenda anasa na wafisadi katika makosa na madhambi yao yote na wanastahiki maangamivu; sawa na wapenda anasa.

Kuna Hadith isemayo: “Mwenye kuridhia dhulma ni kama mwenye kuifanya” “Mwenye kuinyamazia haki ni kama shetani bubu” Ikiwa mambo ni hayo itakuwaje kwa yule mwenye kuiridhia batili?

Anasema Seyyid Afghani: “Ewe mkulima unayechimba ardhi kwa jembe lako kwa nini usilitumie jembe hilo kuuchimba moyo wa anayekufanya mtumwa?” Tazama Juz. 13 (13:11).

Kwa hakika maangamizi yako aina nyingi. Yanaweza kuwa tufani tetemeko la ardhi, vimondo n.k. Vile vile yanaweza kuwa kwa udhalili na kusalitiwa shari.

Aina hii ni mbaya na ya kufedhesha zaidi. Wameadhibiwa nayo umma wa Muhammad (s.a.w.) pale walipoacha jihadi, wakawafumbia jicho wafisadi na washari na wakaukubali udhalili na unyonge.

Imam Ali (a.s.) anasema: “Hakika kwenye utawala wa kiislamu kuna hifadhi ya mambo yenu, basi upeni utiifu wenu... Wallahi ni lazima mfanye hivyo au Mwenyezi Mungu atauondoa kwenu utawala wa kiislamu kisha usirudi kwenu kabisa mpaka mambo yarudie kwa wengine wasiokuwa nyinyi.”

Yaani tukiutii Uislamu tutaishi kwenye ngome imara tukiwa na hadhi na heshima; vinginevyo utawala utahama kwenda kwa maadui zetu, kisha usirudi kwetu. Kila ninaposoma onyo hili basi hujisikia natetema.

Na karne ngapi tumeziangamiza baada ya Nuh?

Makusudio ya karne hapa ni watu. Hii ni hadhari na ahadi kwa wale wanaomkadhibisha Muhammad (s.a.w.) kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni muweza wa kuwafanya kama alivyowafanya wale waliowakadhibisha Mitume waliokuwa kwenye karne zilizopita; kama vile Ad na Thamud:

أَفَأَمِنُوا مَكْرَ اللَّهِ ۚ فَلَا يَأْمَنُ مَكْرَ اللَّهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْخَاسِرُونَ {99}

“Je,wamejiaminisha na hila ya Mwenyezi Mungu? Hawaaminishi hila ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye hasara.” Juz. 9 (7:99).

Imam Ali (a.s.) amesema: “Hakika radhi ya Mwenyezi Mungu kwa waliobaki ni moja na uchukivu wa Mwenyezi Mungu kwa waliobaki ni mmoja. Jueni kuwa Yeye hataridhia chochote alichokichukia kwa waliokuwa kabla yenu wala hatachukia chochote alichowaridhia waliokuwa kabla yenu.”

Na Mola wako anatosha kuwa ni mwenye habari na mwenye kuona dhambi za waja wake.

Kwa hiyo atamwadhibu anavyostahiki. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alisema kumwambia Abu dharr: “Hakika mumin anaziona dhambi ni jiwe kubwa analohofia kumwangukia na kwamba kafiri anaona dhambi zake ni kama nzi tu anayepita puani mwake.”

Anayetaka ya upesi upesi (dunia) tutamharakishia humo tunayoyataka kwa tunayemtaka.

Sio kuwa kila alitakalo mtu anapewa na Mungu, Kwani sisi huwa tunataka mambo mengi na hayawi. Ispokuwa makusudio ya Aya ni kuwa mwenye kufanya kwa ajili ya dunia tu, bila ya kuamini chochote isipokuwa manufaa yake, basi atapata matunda ya kazi yake na juhudi yake kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu, kwani mja hawezi kufikia jambo lolote kama Mungu akikataa, hata kama atafanya kazi usiku na mchana. Hakika Mwenyezi Mungu hatupi tunayoyataka ila kwa kutaka kwake. Hayo ndio makusudio ya ‘tunayoyataka kwa tunayemtaka’

Kisha tunamwekea Jahannam; ataiingia hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa mwenye kufurushwa.

Kwa vile yeye anaamini masilahi yake tu na haoni umuhimu wowote isipokuwa nafsi yake, wala hafanyi lolote isipokuwa kwa ajili yake.

Na mwenye kutaka ya mwisho (Akhera) na akayahangaikia kwa mahangaikio yake huku akiwa ni mumin, basi hao mahangaikio yao yatakuwa ni yenye kushukuriwa.

Makusidio ya kuyahangaikia kwa mahangaikio yake ni kutaka kheri na kuifanya na kuiamini si kwa chochote isipokuwa kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na kheri. Anayefanya hivi ndiye anayestahiki daraja na cheo mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya watu.

Ama anayefanya kwa ajili ya faida na biashara basi yake ni Jahannam. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) anasemama: “Ambaye Hijra yake (kuhama kwake) ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi Hijra yake ni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na ambaye hijra yake ni kwa ajili ya kuipata dunia au mwanamke amuoe, basi Hijra yake ni kwa lile alilololi- hajiria.

Muhtasari wa yote haya ni kuwa Uislamu ni njia inayomuelekeza mtu kufanya kheri na kuiacha shari hiyo yenyewe. Kwa hiyo itakuwa ni lazima kusema ukweli kwa kuwa ni lazima kufanya hivyo na ni lazima kujiepusha na uongo kwa kuwa ni lazima kujiepusha. Mtume (s.a.w.) ameutolea ibara mwelekeo huu kwa kusema: “Hakika nimetumwa kutimiza tabia njema.” Ilivyo hasa ni kuwa tabia njema haiwi ila ikiwa imetakata na kila uchafu.

Wote hao tunawasaidia, hawa na hao,

Hiyo ni ishara ya makundi yote mawili: wale wanaotenda kwa ajili ya dunia na wale wanaotenda kwa ajili ya akhera.

Katika atia za Mola wako; na atia za Mola wako hazizuiliki.

Atia (vipawa) za Mwenyezi Mungu kwa mtu zinaanzia tangu kuumbwa kwake na kuweko kwake ambako hakupatikani ila kwake tu; kisha sababu za kubakia kwake na kukua kwake. Atia hizi zinamhusu mwema na muovu. Ama atia zake katika akhera zitawahusu wema wanaomcha Mungu tu.

Angalia jinsi tulivyowafadhilisha baadhi yao kuliko wengine.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hawagawanyi watu kwenye tabaka, wala kuto- fautiana katika haki za kibinadamu kwa mtu binafsi au makundi. Vipi iwe hivyo na hali yeye ndiye aliyesema:

إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِنْدَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ ۚ{13}

“Hakika mtukufu wenu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule mwenye takua zaidi katika nyinyi” (49:13).

Kwa hiyo basi kuzidiana watu katika dunia, katika isiyokuwa haki ya kibinadamu, inafaa; kama vile afya, umri, riziki kupitia kufanya kazi, kurithi au njia nyingine yoyote aliyoihalalisha Mungu. Lakini utajiri unaokuja kwa ulanguzi, hila na uporaji unatokana na shetani, wala haifai kuunasibisha na Mwenyezi Mungu.

Na akhera ni yenye daraja kubwa zaidi na fadhila kubwa zaidi.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja kuwa watu wanatofautiana katika dunia, sasa anasema kuwa huko Akhera pia itakuwako tofauti, lakini huko tofauti ni kubwa sana. Kwani sifa zinazowatofautisha hapa ni utajiri na ufukara, elimu na ujinga, maradhi na siha na umri mrefu na mfupi; kisha wote wanaishia kwenye mauti kwa usawa, hata wema na waovu. Ama sifa watakazotofautiana huko Akhera, ni kuungua katika moto na kuwa kwenye neema na furaha. Wapi na wapi tofauti hii na ile.

لَا تَجْعَلْ مَعَ اللَّهِ إِلَٰهًا آخَرَ فَتَقْعُدَ مَذْمُومًا مَخْذُولًا {22}

Usimfanye mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, usije ukabaki ni mwenye kukalaumiwa uliyetupwa.

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِنْدَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُلْ لَهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُلْ لَهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا {23}

Na Mola wako amepitisha kuwa msimwabudu yoyote ila Yeye tu na kuwatendea wema wazazi wawili. Mmoja wao akifikia uzee naye yuko kwako au wote wawili, basi usiwaambie Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa heshima.

وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُلْ رَبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا {24}

Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma na useme: Mola wangu! Warehemu kama walivyonilea utotoni.

رَبُّكُمْ أَعْلَمُ بِمَا فِي نُفُوسِكُمْ ۚ إِنْ تَكُونُوا صَالِحِينَ فَإِنَّهُ كَانَ لِلْأَوَّابِينَ غَفُورًا {25}

Mola wenu ni Mjuzi zaidi wa yaliyo katika nafsi zenu, ikiwa nyinyi mtakuwa wema. Hakika Yeye ni Mwenye kughufiria wanaorejea kwake.
  • 1. Hata Waswahili pia hutumia mfumo huu; kwa mfano wanasema: 'huyu ndiye jicho letu' kwa maana ya mtu muhimu.