read

Aya 40 – 44: Je, Mola Wenu Amewachagulia Wavulana?

Maana

Je, mola wenu amewachagulia waototo wa kiume na yeye akajichukulia watoto wa kike katika Malaika?

Qur’an inazingatiwa kuwa ni hoja isiyokuwa na ubishi, katika yote iliyoyasema na kuyasajili. Aya hii inaelezea vile washirikina walivyokuwa wakiitakidi kwamba Mwenyezi Mungu ana mabinti katika aina ya malaika. Vile vile walikuwa wakiitakidi kwamba mtoto wa kiume ni bora kuliko wa kike; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: “Na mmoja wao akibashiriwa msichana uso wake unasawijika naye amejaa chuki.” Juz. 14 (16: 58).

Kwa hiyo basi wao walijinasibishia ubora na uduni wakamnasibishia Mungu. Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawatahayariza na ujinga huu, akawaambia:

Hakika nyinyi mnasema kauli kubwa, kwa sababu Yeye Mwenyezi Mungu hana mshirika wala aliyeshabihiana naye. Lau angelikuwa na mtoto angelikuwa huyo mtoto wake atamrithi na kushabihiana naye, lau angelikuwa na mzazi angelikuwa mzazi wake ni mshirika wake kwenye utukufu na enzi, bali huyo mzazi angelikuwa ni mtukufu zaidi yake, kwa sababu yeye ndiyo sababu ya kupatikana kwake.
Pengine mantiki ya wajahili ni kwamba siri iliyowafanya wamnasibishie Mungu mabinti na wao watoto wa kiume, ni kuwa Mwenyezi Mungu hahofii ufukara kwa sababu ya kuwa na watoto wengi wala aibu ya kuwa na mabinti.

Hakika tumekwishabainisha katika Qur’an ili wapate kukumbuka, lakini haiwazidishii isipokuwa kuwa mbali.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameweka dalili na hoja za kupatikana kwake na umoja wake na akazifafanua kwa kupiga mifano na mifumo mbalimbali ili wafahamu na waelewe, lakini wao wameng’ang’ania njozi na kuiga. Wakazidi inadi na kuwa mbali.

Razi anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu amekithirisha kutaja dalili katika Qur’an, kwa sababu Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu alitaka washirikina wazifahamu na kuziamini. Hii inafahamisha kwamba Yeye, aliyetukuka, anafanya vitendo vyake kwa hekima na inafahamisha kuwa Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu alitaka imani kwa kila mmoja ni sawa aamini au asiamini.”

Kauli hii ya Razi inapingana na aliyoyaelezea mara kwa mara kwamba vitendo vya Mwenyezi Mungu havina sababu ya malengo, na kwamba Yeye ndiye aliyetaka kafiri awe kafiri; kama ilivyo kwa madhehebu ya Ashaira. Lakini Mwenyezi Mungu anataka kuinusuru haki na kuidhihirisha hata kwenye ulimi wa yule anayeipinga bila ya kujitambua.

Sema lau kama wangelikuwa pamoja naye miungu mingine, kama wasemavyo, basi wangelitafuta njia ya kumfikia Mwenye Arshi.

Watu wa tafsiri wametaja maana mbili za Aya hizi:

Kwanza: Ikisemwa kuwa kuna miungu wengine pamoja na Mwenyezi Mungu basi msiwahesabu hao waungu kuwa ni nyota, binadadamu, mawe au vitu vingine. Kwa sababu hivi vyote vimeumbwa na Mwenyezi Mungu, vinamwabudu na kujikurubisha kwake.

Basi mambo yakiwa hivi ni juu yenu enyi washirikiakina kumwabudu Mwenyezi Mungu; kama ambavyo vile manvyoviabudu vinamwabudu Yeye tu.

Maana au tafsiri ya pili ambayo ina nguvu zaidi ni: Lau kungelikuwa na waungu wengine, basi wangelipingana na Mwenyezi Mungu na wangelitafuta nji ya kufikia kwenye madaraka. Hakuna mwenye shaka kwamba kupingana na kuzozana viongozi kunaleta vurugu na ghasia; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

لَوْ كَانَ فِيهِمَا آلِهَةٌ إِلَّا اللَّهُ لَفَسَدَتَا ۚ فَسُبْحَانَ اللَّهِ رَبِّ الْعَرْشِ عَمَّا يَصِفُونَ {22}

“Lau wangelikuwemo humo miungu wengine isipokuwa Mwenyezi Mungu, bila shaka hizo mbingu na ardhi zingelifisidika” (21: 22).

Tumefafanua hayo katika kufasiri Juz. 5 (5:48).

Ametakasika na ametukuka juu kabisa na hayo wanayoyasema.

Amejivua Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na kauli ya madhalimu na washiriki- na kwamba Yeye ana washirika na watoto.

Kila Kitu Kinamtakasa (Kinamsabbih)

Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vilivyomo ndani yake. Na hapana kila kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake.

Ndio! Kila kitu kinamtaksa na kumsifu Mwenyezi Mungu Mtukufu, hilo halina shaka. Tasbih au utakasho wa kitu unatofautiana na kitu kingine kulingana na kilivyo hicho kitu.
Mwenye akili anamtakasa na kumsifu Mwenyezi Mungu kwa ulimi wake, vitu vingine vinamtakasa kwa lugha ya hali. Kwa maneno mengine vinamtakasa na kumsifu kwa jinsi vilivyopatikana umbile lake na mpangilio wake, kuwa yuko mpangiliaji mzuri aliyevifanya viwe hivyo vilivyo; sawa na unavyojulisha mchoro mzuri kuwa mchoraji ni hodari aliye bingwa.

Lugha ya hali ina nguvu na ni fasaha zaidi kuliko lugha ya maneno. Kwa sababu ya maneno inahitajia dalili, lakini ya hali hiyo yenyewe ni dalili inayopeleka kwenye elimu na yakini. Yamekwisha tangulia maelezo ya hayo katika kufasiri Juz. 13 (13:15).

Lakini nyinyi hamfahamu kutakasa kwake. Hakika Yeye ni Mpole Mwenye maghufira.

Hawawezi kufahamu walahidi na washirikina tasbihi zao, kwa sababu ya kujiweka mbali kwao na utukufu wa Mwenyezi Mungu katika kuumba kwake au kwa sababu ya kuzembea kuchunguza na kutambua siri na maajabu ya ulimwengu.

Anasema Ibn Arabi katika kitabu Alfutuhatil-makkiyya Juz. 4: “Mwenyezi Mungu ana ishara aina kwa aina: Kuna zile zinazotambulika kwa kutumia akili, zinazotambulika kwa usikizi na zile zinazotambulika kwa kuona. Kwa hiyo ni juu ya kila mtu kutumia vyombo hivi kuweza kujua ishara za Mwenyezi Mungu ambazo amezitaja katika kitabu chake. Akishajua na kuamini kwazo na akatenda kwa mujibu wake basi atakuwa ni miongoni mwa watu wa Qur’an na watu mahususi wa Mwenyezi Mungu.”

Kisha akaendelea kusema Ibn Arabi: “Chukua kupatikana kote kuwa ni Kitabu kinachotamka haki” Hii ni kama kauli ya mmoja wa wataalamu wa elimu ya Mwenyezi Mungu: “Hakika Mwenyezi Mungu ana vitabu viwili: kimoja kinatamka kwa lugha ya makala, hicho ni Qur’an na kingine kinatamka kwa lugha ya hali nacho ni ulimwengu.”

وَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ جَعَلْنَا بَيْنَكَ وَبَيْنَ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ حِجَابًا مَسْتُورًا {45}

Na unaposoma Qur’an tunaweka baina yako na ya wale wasioamini Akhera pazia linalowafunika.

وَجَعَلْنَا عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ أَكِنَّةً أَنْ يَفْقَهُوهُ وَفِي آذَانِهِمْ وَقْرًا ۚ وَإِذَا ذَكَرْتَ رَبَّكَ فِي الْقُرْآنِ وَحْدَهُ وَلَّوْا عَلَىٰ أَدْبَارِهِمْ نُفُورًا {46}

Na tunaweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasije wakaifahamu na tunaweka kwenye masikio yao uziwi. Na unapomtaja Mola wako peke yake katika Qur’an, basi wao hugeuka nyuma wakaenda zao.

نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَسْتَمِعُونَ بِهِ إِذْ يَسْتَمِعُونَ إِلَيْكَ وَإِذْ هُمْ نَجْوَىٰ إِذْ يَقُولُ الظَّالِمُونَ إِنْ تَتَّبِعُونَ إِلَّا رَجُلًا مَسْحُورًا {47}

Sisi tunajua vyema kabisa sababu wanayosikilizia wanapokusikiliza, na wanaponon’gona, wanaposema hao madhalimu: nyinyi hamfuati isipokuwa mtu aliyerogwa.

انْظُرْ كَيْفَ ضَرَبُوا لَكَ الْأَمْثَالَ فَضَلُّوا فَلَا يَسْتَطِيعُونَ سَبِيلًا {48}

Tazama vipi wanavyokupigia mfano. Basi wamepotea, kwa hiyo hawawezi kuipata njia.