Aya 45 – 48: Unaposoma Qur’an
Maana
Na unaposoma Qur’an tunaweka baina yako na ya wale wasioamini Akhera pazia linalowafunika.
Kuna kauli nyingi katika kufasir Aya hii. Yenye nguvu zaidi ni ile isemayo kuwa jamaa katika washirikina walikuwa – Muhammad anaposoma Qur’an – wanajaribu kumzuia kwa kumuudhi, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akamwambia endelea kusoma Qur’an na kutoa mwito wa Mwenyezi Mungu wala usichoke.
Na tunaweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasije wakaifahamu na tunaweka kwenye masikio yao uziwi.
Hili ni fumbo la inadi ya washirikina. Ama kunasibisha vifuniko na uziwi kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.), tumekuzungumzia kwa ufafanuzi katika kufasiri Juz. 7 (6:25). Hiyo ni mfano wa Aya hii kinukuu na kimaana.
Na unapomtaja Mola wako peke yake katika Qur’an, basi wao hugeuka nyuma wakaenda zao.
Walikuwa washirikina, inaposomwa Qur’an, wanapomsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema: Lailaha illallah (hapana Mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu) basi wanaachana naye na kwenda zao huku wakisema:
أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ {5}
وَانْطَلَقَ الْمَلَأُ مِنْهُمْ أَنِ امْشُوا وَاصْبِرُوا عَلَىٰ آلِهَتِكُمْ ۖ {6}
Sio siri kuwa upinzani huu ni kwa vile tu tamko la tawhid linakusanya msingi wa kusema: “Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu ni yule mwenye takua zaidi” (49: 13). Sio utabaka na ubaguzi.
Sisi tunajua vyema kabisa sababu wanayosikilizia wanapokusikiliza, na wanaponon’gona, wanaposema hao madhalimu: Nyinyi hamfuati isipokuwa mtu aliyerogwa.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kusema: ‘na tunaweka kwenye masikio yao uziwi’ sasa anasema: Sisi tunajua vizuri kwamba wewe wakati unaposoma Qur’an washirikina hawakusikilizi kwa moyo safi, bali wanakusikiliza kwa kwa roho ya chuki, inadi na kiburi, kisha wanaambiana na pia kuwaambia wengine, kuwa Muhammad ni mchawi ameingiwa na jini linalozungumza hekima na ufasaha huu kwenye ulimi wake; itakuwaje azungumze hivi naye hajui kusoma wala kuandika, tena hana hazina ya dhahabu au fedha wala hana shamba la mitende na mizabibu.
Hii ndio fikra yao ya kitabaka, kwamba mwenye mali tu ndio anayeweza kuwa na cheo kitukufu kiwe cha dini au cha kawaida: “Na walisema: kwa nini hii Qur’an haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili hii” (43:31) Ama akili, ukweli na uaminfu kwao hauna maana.
Tazama vipi wanavyokupigia mfano.
Walizidi mno kwa Muhammad (s.a.w.) kwa vile kuwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na kutamka maneno ya Mwenyezi Mungu; mara wakamwita mwendawazimu, mara mchawi, mara kuhani na mara nyingine wakamwita mshairi.
Muhammad ambaye ametumwa kukamilisha tabia njema, amekuwa mchawi na mwendawazimu? Kwa nini amekuwa hivyo? Kwa vile yeye anatamka haki na kuitolea mwito na wala hakukubaliana na matamanio ya wabatilifu na wafisadi. Zaidi ya hayo hana farasi wala mali.
Kwa ufupi ni kwamba watu wa matamanio na matakwa, hisia zao ziko upande mmoja tu, matamanio na masilahi yao binafsi. Hawasikii wala hawaoni isipokuwa kwayo tu; kiasi cha kuhalalisha yote kwenye hawa zao na matamanio. Kwa hali hii ndio tunapata tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao; na juu ya macho yao pana kifuniko” Juz. 1 (2:7) na tafsiri ya kila Aya iliyo na maana haya katika maneno ya Mtukufu Aliyetukuka.
Basi wamepotea, kwa hiyo hawawezi kuipata njia, ya kuwakadhibisha wenye haki, isipokuwa uzushi, upotevu, ulaghaii, uadui, njama na rushwa.
وَقَالُوا أَإِذَا كُنَّا عِظَامًا وَرُفَاتًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ خَلْقًا جَدِيدًا {49}
قُلْ كُونُوا حِجَارَةً أَوْ حَدِيدًا {50}
أَوْ خَلْقًا مِمَّا يَكْبُرُ فِي صُدُورِكُمْ ۚ فَسَيَقُولُونَ مَنْ يُعِيدُنَا ۖ قُلِ الَّذِي فَطَرَكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ ۚ فَسَيُنْغِضُونَ إِلَيْكَ رُءُوسَهُمْ وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هُوَ ۖ قُلْ عَسَىٰ أَنْ يَكُونَ قَرِيبًا {51}
يَوْمَ يَدْعُوكُمْ فَتَسْتَجِيبُونَ بِحَمْدِهِ وَتَظُنُّونَ إِنْ لَبِثْتُمْ إِلَّا قَلِيلًا {52}