read

Aya 61-65: Wakasujudu

Maana

Na tulipowaambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipokuwa Iblis, alisema: Je, nimsujudie uliyemuumba kwa udongo?

Umepita mfano wake katika Juz. 1 (2:35) na Juz. 8 (7:11).

Kumtanguliza Aliyezidi Juu Ya Aliyezidiwa

Akasema: Unaona! Huyu ndiye uliyemtukuza zaidi kuliko mimi?

Iblisi anahoji kwa majisifu na ufedhuli akimwambia, aliyemtukufu na kutukuka, kuwa ni nani huyo ambaye umemfadhilisha kuliko mimi? Na ni kitu gani kimemfanya awe na heshima hiyo na ukamilifu? Naona ni kinyume na hivyo:

قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِنْهُ خَلَقْتَنِي مِنْ نَارٍ وَخَلَقْتَهُ مِنْ طِينٍ {12}

“Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye, umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo.” Juz. 8 (7:12).

Habithi huyu alijitia ubora kwa kutetea mantiki yake, kuwa yeye ni bora na mkamilifu. Kwa hiyo yeye hafai kumsujudia aliyemzidi.

Ibilisi amekosea katika mantiki yake haya. Kwa sabau yeye si bora kabisa kuliko Adam, bali ni kinyume. Kwahiyo Mwenyezi Mungu hakumtanguliza aliyezidiwa juu ya aliyezidi; kama alivyodai Ibilisi. Ni akili gani inayoruhusu kuwa Mwenyezi Mungu amkurubishe aliye baidi na ambaidishe aliye karibu? Lakini hakika hii imefichika kwa Ashaira1 na Mu’tazila, waliposema kuwa inafaa kutangulizwa aliyezidiwa juu ya aliyemzidi. Tazama kitabu Al-mawqif Juzuu ya nane Uk. 373.

Wanasema Ashaira; Akili inakubali kuwa Mwenyezi Mungu atamwadhibu mtiifu na kumpa thawabu muasi, kwa sababu, kwa Mwenyezi Mungu hakuna uovu wala hana wajibu wowote. Tazama kitabu hicho hicho Uk. 195. Shia Imamiya wanasema akili haikubali kuwa Mwenyezi Mungu amwadhibu aliyefanya wema, lakini inakubali kuwa anaweza kuwasamehe waovu; sawa na mwenye haki yake, anaweza akasamehe yote au baadhi.

Wakaendelea kusema kuwa haikubaliki kiakili kutangulizwa aliyezidiwa juu ya aliyemzidi kwa sababu ni daraja ya juu na ya chini kulingana na utaratibu wa kimaumbile. Kumfanya aliyejuu kuwa yuko chini na aliye chini kuwa yuko juu ni kinyume na mantiki ya kiakili na kimaumbile.

Kama utaniahirisha mpaka siku ya kiyama, bila shaka nitakiburuza kizazi chake isipokuwa wachache tu.

Ibilisi anatishia kuchukua kisasi kwa kizazi cha Adamu; si kwa jambo lolote ila ni kwa sababu Mwenyezi Mungu amemtukuza Adamu. Anachukua kisasi kwa kuwaburuza kwenye maasi, kama vile anavyokokotwa mnyama; isipokuwa wachache tu ambao ni wale wenye ikhlasi.

Kisha Ibilisi anataka apewe muda katika maisha yake ili apoteze watu na afanye ufisadi; Mwenyezi Mungu akamkubalia maombi yake, akasema: ondoka! Atakayekufuata katika wao, basi Jahannam itakuwa ndio malipo yenu, malipo yenye kutimia.

Ibilisi alipotishia kuwapoteza wanadamu, Mwenyezi Mungu naye akamkemea yeye na wale atakaowapoteza na kumwambia: fanya utakavyo, atakufuata kwenye upotevu yule atakayetaka, kwani mimi si mlazimishi yeyote kwenye twaa na maasi. Wote ninawapa uwezo, akili na utashi na ninawabainishia njia ya kheri na njia ya shari. Ninakataza hili na kuamuru lile. Mwenye kufuata na akatii, basi pepo ni makazi yake na mwenye kuwa jeuri na akaasi basi jahannam ndio makazi ya waasi; watal- ipwa humo malipo wanayostahiki kwa ukamilifu bila ya upungufu.

Na uwachochee uwawezao katika wao kwa sauti yako na wakusanyie jeshi lako la wapandao farasi na wendao kwa miguu.

Hakuna jeshi la hakika hasa la iblisi lililo na farasi au bila ya farasi; isipokuwa ni fumbo la wafisadi, yaani watu wanaofuata hawaa, wahaini na vibaraka.

Amesema Imam Ali katika Nahjul-balagha: “Tahadharini asije aka-chochea -shetani- kwa mwito wake na kuwakusanya kwenye jeshi lake la wapanda farasi na wanaokwenda kwa miguu.” Sheikh Muhammad Abduh naye akaongezea kwa kusema: ”Anawachochea mfanye lile alitakalo, mkichelewa atawakusanyia jeshi lake la wapanda farasi na waendao kwa miguu, yaani wasaidizi wake.”

Umepita mfano wake katika Juz. 8 (7:18). Huko tumejibu maswali matatu: kuwa je, alizungumza moja kwa moja na Mwenyezi Mungu au kwa kupitia kitu kingine? Je, upotevu unatokana na Mwenyezi Mungu au na Ibilisi? Kwanini Mwenyezi Mungu akampa muda Ibilisi ili apoteze watu? Rudia huko.

Na shirikiana nao katika mali na watoto.

Kushirkiana katika mali ni fumbo la kila mali iliyopatikana kwa njia isiyokuwa ya haki; kama vile uporaji, riba, utapeli, hiyana na kuwa kibaraka. Au kuitumia isivyostahiki; kama vile kufanya israfu, kuitumia kwenye pombe, kamari na kwenye mambo ya kujionyesha. Ama kushirikiana katika watoto ni fumbo la zina, kuua watoto kwa kuhofia ufukara na aibu na kuwalea malezi ya ufisadi.

Na uwaahidi na shetani hawapi ahadi ila ya udanganyifu.

Ahadi ya udanganyifu ni kuivisha batili nguo ya haki na makosa kuyavika nguo ya usawa; kwa mfano shetani kumtia wasiwasi anayeamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, kuwa usihofie kumuasi Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu ni karimu Mwingi wa maghufira, na wewe bado una umri, utatubia kesho na kuomba maghufira.

Kuna baadhi ya mapokezi yanayosema kuwa Ibilisi alimtia wasiwasi mfanya ibada mmoja katika waisrail, afanye dhambi kisha atubie ili ibada yake iwe na nguvu.

Hakika waja wangu hutakuwa na mamlaka nao, na Mola wako anatosha kuwa ni wa kutegemewa.

UmepitamfanowakekatikaJuz.14(15:42).

رَبُّكُمُ الَّذِي يُزْجِي لَكُمُ الْفُلْكَ فِي الْبَحْرِ لِتَبْتَغُوا مِنْ فَضْلِهِ ۚ إِنَّهُ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا {66}

Mola wenu ndiye anayewaendeshea majahazi, ili mtafute katika fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwenye kuwarehemu.

وَإِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فِي الْبَحْرِ ضَلَّ مَنْ تَدْعُونَ إِلَّا إِيَّاهُ ۖ فَلَمَّا نَجَّاكُمْ إِلَى الْبَرِّ أَعْرَضْتُمْ ۚ وَكَانَ الْإِنْسَانُ كَفُورًا {67}

Na inapowagusa dhara katika bahari, hao mnaowaomba wanapotea, isipokuwa Yeye tu. Anapowaokoa mkafika nchi kavu mnageuka. Na Mtu amekuwa mwingi wa kukanusha.

أَفَأَمِنْتُمْ أَنْ يَخْسِفَ بِكُمْ جَانِبَ الْبَرِّ أَوْ يُرْسِلَ عَلَيْكُمْ حَاصِبًا ثُمَّ لَا تَجِدُوا لَكُمْ وَكِيلًا {68}

Je, mmeaminisha kuwa hataweza kuwadidimiza upande wa nchi kavu au kuwaletea tufani la kokoto, kisha msipate wa kutegemea?

أَمْ أَمِنْتُمْ أَنْ يُعِيدَكُمْ فِيهِ تَارَةً أُخْرَىٰ فَيُرْسِلَ عَلَيْكُمْ قَاصِفًا مِنَ الرِّيحِ فَيُغْرِقَكُمْ بِمَا كَفَرْتُمْ ۙ ثُمَّ لَا تَجِدُوا لَكُمْ عَلَيْنَا بِهِ تَبِيعًا {69}

Au mmeaminisha kuwa hatawarudisha humo mara nyingine awapelekee kimbunga cha upepo awazamishe kwa mlivyokufuru, kisha msipate wa kutufuatilia.
  • 1. Madhehebu ya kiitikadi yanayofuatwa na masunni wengi. Muasisi wake ni Abul Hassan Al-ash'ariy aliyekufa mwaka 324 AH (936 AD) -Mtarjumu.