read

Aya 66-69: Anawaendeshea Majahazi

Maana

Mola wenu ndiye anayewaendeshea majahazi, ili mtafute katika fad- hila zake. Hakika Yeye ni Mwenye kuwarehemu.

Jahazi inatembea kwenye uso wa bahari kwa sababu za kimaumbile, hilo halina shaka, lakini sababu hizi zote zinaishia kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa sababu yeye ni muumba wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake.

Ni kwa sababu hii ndio ikafaa kutegemeza kuendesha kwake Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hekima ya hilo ni kuwa mtu daima awe katika fikra ya kuwa Mwenyezi Mungu ndiye mtendaji mkuu wa vilivyomo ulimwenguni na wala sio maumbile. Ama lengo la jahazi ni kurahisisha mawasiliano.

Na inapowagusa dhara katika bahari, hao mnaowaomba wanapotea, isipokuwa Yeye tu. Anapowaokoa mkafika nchi kavu mnageuka.

Na mtu amekuwa mwingi wa kukanusha.

Umepita mfano wake katika Juz. 11 (10:22).

Je, mmeaminisha kuwa hataweza kuwadidimiza upande wa nchi kavu au kuwaletea tufani la kokoto, kisha msipate wa kutegemea?

Watu wote wako mikononi mwa Mungu, popote pale walipo, hata wakiwa kwenye ngome zilizo na nguvu. Wakiwa baharini anaweza kuwangamiza kwa kufa maji, wakiwa nchi kavu anaweza kuwadidimiza ardhini au kunyweshewa na mvua ya mawe na wakiwa kwenye ngome imara anivunjilia mbali. Hawezi kujiaminisha ila mjinga.

Au mmeaminisha kuwa hatawarudisha humo mara nyingine awapelekee kimbunga cha upepo awazamishe kwa mlivyokufuru, kisha msipate wa kutufuatilia.

Humo ni baharini. Maana ni kuwa hakuna njia nyingine ya kuangamia isipokuwa baharini, basi Mwenyezi Mungu ana uwezo wa kuwarudisha humo, awazamishe kwa kimbunga na asipatikane wa kumfuatilia Mungu kwa aliyowafanyia.

Ufupi wa Aya hizo ni kuwa mjinga humhofia Mwenyezi Mungu anapokuwa na shida, lakini shida ikimuondokea anamgeuka; pamoja na kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni muweza wa kunufaisha na kudhuru. Ama mumin mwenye akili anapata mawaidha kwa shida na raha, anahofia haya na kutaraji msaada kwa yale.

وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُمْ مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَىٰ كَثِيرٍ مِمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلًا {70}

Hakika tumewatukuza wanaadamu na tumewabeba nchi kavu na baharini na tumewaruzuku vitu vizuri na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tuliowaumba.

يَوْمَ نَدْعُو كُلَّ أُنَاسٍ بِإِمَامِهِمْ ۖ فَمَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَأُولَٰئِكَ يَقْرَءُونَ كِتَابَهُمْ وَلَا يُظْلَمُونَ فَتِيلًا {71}

Siku tutakapowaita watu kwa Imam wao. Basi atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kuume, basi hao watasoma kitabu chao wala hawatadhulumiwa hata chembe.

وَمَنْ كَانَ فِي هَٰذِهِ أَعْمَىٰ فَهُوَ فِي الْآخِرَةِ أَعْمَىٰ وَأَضَلُّ سَبِيلًا {72}

Na aliyekuwa kipofu katika hii, basi Akhera atakuwa kipofu na aliyepotea zaidi njia.