Aya 73 -77: Je Mtume Anahadaika Na Dini Yake
Maana
Na hakika walikaribia kukufitini uache tuliyokupa wahyi ili utuzulie mengine. Na hapo wangelikufanya rafiki.
Waliokaribia ni washirikina. Walijaribu washirikiane na Mtume (s.a.w.) kwa kumtaka awakubalie matakwa yao na wamfanye kuwa ni kiongozi na rafiki. Miongoni mwa hayo ni kuigusa miungu yao au angalau aache kuikashifu, lakini Mtume hakuwakubalia matakwa yao washirikina, kwa sababu yeye ni maasum na maasum hawezi kuchangia dini yake na risala yake na mambo mengine.
Unaweza kuuliza: Kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘walikaribia kukufitini’ inafahamisha kuwa yeye Mtume alikaribia kuwakubalia matakwa yao?
Jibu: Aya hii inafungamana moja kwa moja na Aya inayofuatia.
Lau sikukuweka imara ungelikurubia kuwaelekea kidogo.
Kwa hiyo maana ni kuwa, hakika wewe Muhammad lau si ulinzi wetu kwako kwa kukupa isma (kuhifadhika) ya dhambi, basi ungelikaribia kuwaelekea washirikina na kuwatikia maombi yao. Isma ndiyo iliyokuzuia kuwakubalia. Ni sawa na kusema: ‘Lau si fulani ungeliangamia’ Umetangulia mfano wake katika Juz. 12 (12: 24).
Zaidi ya hayo, kufikiria kufanya kitu ni jambo jingine na kukifanya ni jambo jingine. Kuna Hadith mutawatir kutoka kwa Mtume kwamba yeye amesema: “Umeondolewa umma wangu yale yanayozungumzwa na nafsi zao madamu hawakufanya au kuzungumza,” yaani kujizungumzia mtu mwenyewe nafsini mwake, hakuna athari. Kuna mapokezi yanayosema, kuwa washirikina walipomwambia Mtume alinyamaza, hakuwajibu.
Hapo basi, tungelikuonjesha maradufu ya uhai na maradufu ya mauti.
Maana ni kuwa, ewe Muhammad! Lau ungeliwaelekea washirikina tungelikuadhibu mara mbili zaidi ya mwengine, duniani na Akhera. Kwa sababu adhabu ya wakuuu inakua kulingana na ukuu wao na cheo chao. Hii ni kiasi cha kukadiria tu, na ‘kukadiria muhali sio muhali.’
Kisha usingelipata wa kukunusuru nasi, kukukinga na adhabu.
Katika Nahju-lbalagha imeelezwa: “Siku ya Kiyama ataletwa kiongozi mkandamizaji, akiwa hana wa kumsaidi wala wa kumtolea udhuru, atatupwa katika Jahannam, azunguke humo kama pia, kisha afungwe kwenye shimo lake.”
Na kwa hakika walikaribia kukukera katika nchi ili wakutoe humo; na hapo wasingelibakia nyuma yako ila muda mchache.
Waliposhindwa washirikina na Mtume walijaribu kumkera kwa kila njia ili atoke Makka. Lau wangelimtoa, basi Mwenyezi Mungu angeliwangamiza muda kidogo baada ya kutoka kwake.
Unaweza kuuliza kuwa si walifanya hivyo washirikina pale walipoafikiana kumuua Mtume, mpaka akalazimika kutoka kwenda Makka kwa kuhofia, kama ilivyoelezwa katika Juz. 9 (8:30).
Jibu: makusudio ni kuwa lau washirikina wangelimtoa wao kwa nguvu na kua ni mkimbizi aliyefukuzwa asiyejua pa kwenda, basi Mwenyezi Mungu angeliwangamiza haraka sana. Lakini Mtume alitoka Makka kwa amri ya Mwenyezi Mungu kwenda kwa watu ambao walijitolea kwake kwa hali na mali na familia.
Ndio desturi ya wale tuliowatuma kabla yako wala hutapata mabadiliko katika desturi yetu.
Yametangulia maelezo kuhusu hukumu ya Mwenyezi Mungu na kadha yake, kwamba kaumu yoyote itakayomtoa Mtume wao kwa nguvu, Mwenyezi Mungu anaiangamiza haraka. Na hii ndio desturi katika viumbe vyake, haibadiliki wala haigeuki, inaendela wakati wote na mahali kote.
أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ إِلَىٰ غَسَقِ اللَّيْلِ وَقُرْآنَ الْفَجْرِ ۖ إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا {78}
وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَكَ عَسَىٰ أَنْ يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَحْمُودًا {79}
وَقُلْ رَبِّ أَدْخِلْنِي مُدْخَلَ صِدْقٍ وَأَخْرِجْنِي مُخْرَجَ صِدْقٍ وَاجْعَلْ لِي مِنْ لَدُنْكَ سُلْطَانًا نَصِيرًا {80}
وَقُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ ۚ إِنَّ الْبَاطِلَ كَانَ زَهُوقًا {81}