read

Aya 78-81: Simamisha Swala Linapopinduka Jua

Maana

Aya ya kwanza na ya pili ni miongoni mwa Aya za hukumu, zilizoshuka kwa ajili ya kubainisha nyakati za Swala. Wana-Fiqh wana kauli kadhaa, kama zifuatavyo:

1. Simamisha Swala linpopinduka jua mpaka giza la usiku.

Wametofautiana katika makusudio ya kupinduka jua. Imesemekana ni wakati wa kutua jua na ikasemkena ni kupinduka nusu ya mzingo wa mbingu (meridian), na hiyo ndiyo kauli ya wengi.
Imepokewa kutoka kwa Imam Ja’far As-swadiq (a.s.) kwamba giza la usiku ni nusu ya usiku.

Katika tafsiri za kisunni na kishia imeelezwa kuwa Aya hii imekusanya nyakati zote za Swala tano: Adhuhuri na Alasiri zinaingia katika kupinduka jua. Magharibi na Isha zinaingia katika giza la usiku na Asubuhi katika Qur’an ya alfajiri.

Katika Shia amesema Tabrasi kwenye Majmau-bayan: “Aya hii imeku- sanya Swala tano: Swala ya adhuhuri na alasiri zinaingia katika kupinduka jua, swala ya magharibi na isha zinaingia katika giza la usiku na makusudio ya Qur’an ya alfajiri ni swala ya alfajiri. Hizi ndizo Swala tano.”

Katika sunni amesema Razi: “Simamisha Swala, yaani idumishe kuanzia wakati wa kupinduka jua mpaka giza la usiku, inaingia swala ya adhuhuri, alasiri magharibi na isha” Kisha akaendela kusema: “wamekongamana kuwa makusudio ya Qur’an ya alfajiri ni Swala ya asubuhi.”

Ilivyo ni kwamba mafaqihi, katika vitabu vyao, wanaanza maneno kwa Swala ya adhuhuri kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘linapopinduka jua’ ambapo ameanzia Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kwa kutaja wakati wake.

Kuongezea mapokezi ya Hadith zinazoelezea kuwa adhuhuri ndiyo ya kwanza kufaradhishwa, kisha zikafuatia nyingine kwa utaratibu ulivyo. Hilo lilikuwa Makka usiku wa Israi, mwaka mmoja kabla ya Hijra (kuhamia Madina).

Madhehebu za kiislamu zimeafikiana kuwa haifai Swala kabla ya kuingia wakati wake na kwamba jua likipinduka ndio umeingia wakati wa Adhuhri, lakini wametofautiana kwenye kiwango cha muda huu, unaisha wakati gani?

Shia Imamiya wamesema kuwa mara tu bada ya kupinduka jua unahusika wakati wa Swala ya adhuhuri kwa kiasi cha kuswaliwa kwake na kiasi cha kuweza kuswaliwa swala ya alsiri mwisho wa mchana kinahusika na Swala ya alasiri. Baina ya wakati wa kwanza na wa mwisho ni wa ushirikano wa Swala mbili; yaani inaweza kuswalia adhuhuri na alasiri.

Dhahiri ya Aya iko pamoja nao: ‘linpopinduka jua mpaka giza la usiku’ wala Mwenyezi Mungu hakutenganisha; kama ilivyo kwenye madhehebu nyingine.

Wengineo wamesema kuwa wakati wa adhuhuri unaanza linapopinduka jua mpaka kuwa kivuli cha kila kitu mfano wake, ikizidi hapo wakati wa adhuhuri utakuwa umekwisha na utakuwa wakati wa alasiri umeingia. Ufafanuzi uko katika kitabu chetu: Al-fiqh ala madhahib al-khamsa (Fiqh kwenye madhehebu matano).

2. Na Qur’an ya alfajiri. Hakika Qur’an ya alfajiri imekuwa ni yenye kushuhudiwa.

Wameafikiana kwamba makusudio ya Qur’an ya alfajiri ni ile inayosomwa katika Swala ya alfajiri, yaani ya asubuhi. Vil vile wameafikiana kwamba wakati wake unaanzia kutokeza alfajiri ya kweli mpaka kutoka jua (mawiyo); isipokuwa Maliki anasema kuwa asubuhi ina nyakati mbili: Ya hiyari, inaanzia alfajiri hadi kujuana nyuso. Na wakati wa dharura unaoanzia kujuana nyuso hadi kutoka jua. Kauli ya kushangaza ni ile ya masufi wanaosema kuwa makusudio ya alfajiri ni kupasuka moyo.

Wamekongamana mafaqihi, kwa ushahidi wa Tabrasi na Razi, kwamba makusudio ya yenye kushuhudiwa, ni kwamba Malaika wa usiku na mchana wanakusanyika ili washuhudie Swala. Wametegemea riwaya aliyoipokea Bukhari kutoka kwa Abu Hurayra, katika Sahih Bukhari Juzuu ya

6 mlango wa sura Bani Israil. Sisi tunaishuku riwaya hii. Na tunafasiri yenye kushuhudiwa, kuwa ni kuhudhuria hisiya. Kwa sababu mtu wakati wa asubuhi hisia zake zinakuwa zipo baada ya kupumzika na usingizi. Ndio maana ikasemwa ‘usingizi unabeba maazimio ya siku’

3. Na katika usiku amka kwayo ni ziada kwa ajili yako.

Kwayo ni hiyo Qur’an. Kwa ajili yako ni kumuhusisha yeye tu. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amekufaradhishia wewe Muhammad swala nyingine, zaidi ya zile tano ambazo ni zako na wengine, uiswali usiku. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

يَا أَيُّهَا الْمُزَّمِّلُ {1}

قُمِ اللَّيْلَ إِلَّا قَلِيلًا {2}

“ Ewe mwenye kujifunika nguo! Simama usiku isipokuwa kidogo.”(73:1-2)

وَمِنَ اللَّيْلِ فَاسْجُدْ لَهُ وَسَبِّحْهُ لَيْلًا طَوِيلًا {26}

“ Na usiku umsujudie Yeye na umtakase usiku mrefu.” (76:26).

Swala hii inaitwa Swala ya usiku (swalatu-llayl). wakati wake ni kuanzia nusu ya usiku hadi alfajiri. Ni wajibu kwa Mtume (s.a.w.), kama tulivyoeleza mwanzo na ni sunna kwa mwenginewe.

Huenda Mola wako akakuinua cheo kinachosifika.

Huenda ni neno la kutarajia ikiwa linatoka kwa kiumbe na ni la mkato ikiwa linatoka kwa muumbaji. Hapa anaambiwa Muhammad (s.a.w.).

Hakuna kitu zaidi ya Muhammad wala cheo zaidi ya Muhammad na kizazi zaidi ya kizazi cha Muhammad; isipokuwa yule ambaye hakuna mfano wake kitu chochote. Kuna Hadithi isemayo kuwa Mtume (s.a.w.) alifasiri cheo chenye kusifika katika Aya hii kuwa ni cheo atakachowaombea umma wake kesho.

Na sema: Mola wangu! Niingize muuingizo mwema na nitoe kutoka kwema.

Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake mtukufu kuomba dua hii. Kuingia kwema na kutoka kwema ni fumbo la haki na ikhlsi katika itikadi, makusudio, vitendo, harakati zote na kupumzika. Hakuna shaka kuwa mwenye kuwa na silaha ya haki na akamfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu peke yake, basi atamuimarisha kwa kauli thabiti, atampa hoja imara na umakini wa moyo ulio mwema na safi.

Na unipe madaraka kutoka kwako ya ushindi.

Kuna ushindi na madaraka yanayozidi kutajwa Mtume mtukufu pamoja na jina la Mwenyezi Mungu mara tano kwa siku, katika adhana na katika swala za wajibu na sunna? Kuna nguvu gani na heshima adhimu kuliko ile aliyompa Muhammad, aliposema:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانْتَهُوا ۚ {7}

“Anachowapa Mtume kichukueni na anachowakataza kiacheni.” (59:7).

Na sema haki imefika na batili imetoweka. Hakika batili ni yenyekutoweka.

Haki ni risala ya Muhammad, itikadi na sharia. Vinginevyo ni batili, kiuhalisi na mbele ya Mwenyezi Mungu; hata kama vitaaminiwa na watu wa ardhini wote. Wafasiri wamesema kuwa makusudio ya batili hapa ni ushirikina na kwamba Mtume (s.a.w.) alipoikomboa Makka aliingia Al- ka’ba na mlikuwa na masanamu 360, akawa anazisukuma huku akisema: “Haki imefika na batili imetoweka. Hakika batili ni yenye kutoweka.”

Nguvu Ya Haki Na Nguvu Ya Batili

Unaweza kuuliza: Mara nyingi tunaona na kushuhudia watu wa batili wakishinda na watu wa haki wakishindwa. Hii si inapingana na kauli ya Mwenyezi Mungu ‘Hakika batili ni yenye kutoweka’ ?
Jibu, Hakika haki ina nguvu za dhati zisizoepukana nazo kwa hali yoyote; nazo zinatenda kazi na kuathiri kwenye nyoyo safi zilizo takatifu. Mara nyingi athari hii inafikia kiwango ambacho hakuna nguvu yote yote inayoweza kuisimamisha; si mapanga ya wachinjaji wala unyongaji wa mataghuti.

Historia inatusimilia jinsi mashahidi wa itikadi walivyojitolea kuwa mashahidi kwa nyuso za kutabasamu na nafsi zilizo radhi; bali hayo yametokea wakati wetu huu huko Vietnam, Korea, Palestina na kwengineko.

Ndio! Ni kweli hawa ni wachache; kama ilivyo kawaida ya kila jambo tukufu lenye thamani. Lakini wangelikuwa wengi kwa idadi au wengi kwa viwango vya asilimia, basi dunia ingelijaa uadilifu, na dhulma na jeuri isengelikuwa na athari yoyote. Sisi hatuna shaka ubinadamu utakwenda na njia hii; hata kama muda utakuwa mrefu.

Ama batili, haina nguvu wala urefu, isipokuwa kuweko kwake kunategema rushwa, dhulma, ukandamizaji, kuwafukuza watu njama n.k.

Haya yote yataondoka kadiri siku zinavyokwenda na hali kubadilika. Ama nguvu ya haki huwa inakwenda na wakati, inabakia hivyo hivyo tu wakati wote. Kwa sababu inategema hiyo haki yenyewe, kama ilivyo. Kwa ajili hii ndio tunasema tena: Sisi tuna imani isiyokuwa na shaka kwamba mwisho ni wa haki na neno la juu litakuwa la haki peke yake.

وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِلْمُؤْمِنِينَ ۙ وَلَا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَارًا {82}

Na tunateremsha katika Qur’an ambayo ni ponyo na rehema. Wala haiwazidishii madhalimu isipokuwa hasara.

وَإِذَا أَنْعَمْنَا عَلَى الْإِنْسَانِ أَعْرَضَ وَنَأَىٰ بِجَانِبِهِ ۖ وَإِذَا مَسَّهُ الشَّرُّ كَانَ يَئُوسًا {83}

Na tunapomneemesha mtu hugeuka na kujitenga kando na inapomgusa shari hukata tamaa.

قُلْ كُلٌّ يَعْمَلُ عَلَىٰ شَاكِلَتِهِ فَرَبُّكُمْ أَعْلَمُ بِمَنْ هُوَ أَهْدَىٰ سَبِيلًا {84}

Sema: kila mmoja anafanya kwa namna yake. Na Mola wenu anajua aliyeongoka katika njia.

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ ۖ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُمْ مِنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا {85}

Wanakuuliza kuhusu roho. Sema: roho inatokana na amri ya Mola wangu. Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.