read

Aya 82-85: Qur’ani Ni Ponyo

Maana

Na tunateremsha katika Qur’an ambayo ni ponyo na rehema.

Qur’an ni rehema kwa yule anayeitakia nafsi yake rehema na ni ponyo la ukafiri, ulahidi, ujinga, ufisadi na kila uchafu, kwa yule mwenye kumfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu na haki.

Imam Ali (a.s.) katika kuisifu Qur’an ansema: “Hakika hiyo ni kamba imara, nuru inayobainisha, ni dawa yenye kuleta nafuu, ni kichujio cha takataka, ni hifadhi kwa mwenye kushikamana nayo na ni uokovu kwa mwenye kufungamana nayo.” Mwenye kuhalifu hukumu miongoni mwa hukumu za Qur’an atakuwa miongoni mwa madhalimu na waliohasirika.

Wala haiwazidishii madhalimu isipokuwa hasara.

Qur’an ni rehema kwa waumini na nakama kwa madhalimu na wafisadi, kwa sababu kila wanapoasi hukumu miongoni mwa hukumu zake, wanazidi dhambi na adhabu.

Na tunapomneemesha mtu hugeuka na kujitenga kando na inapomgusa shari hukata tamaa.

Maana ya Aya hii yanafupilizwa na kauli ya Imam Ali (a.s.) katika wasifu wa mtu: “Akijitosheleza huchangamka na kushawishika na anapofukarika hukata tamaa na kubweteka. Umepita mfano wake katika Juz . 11 (10:12) na Juz. 12 (11: 9).

Sema: kila mmoja anafanya kwa namna yake. Na Mola wenu anajua aliyeongoka katika njia.

Wafasiri wamesema: “Namna, ni njia. Na maana ya Aya ni kuwa kila mmoja kati ya mumin na kafiri anafanya kwa njia yake na maumbile yake” lakini sisi tutaifafanua, kama tulivyoifahamu, katika hali zifuatazo:

1. Neno kila mmoja linafahamisha kuenea kwa mtu mmoja mmoja; kwa mfano ukisema: kila mtu analifahamu hili, ni kama umesema: Zayd analifahamu na Bakari, Hindu n.k. (yaani kila mmoja ana namna yake ya kulifahamu) Lakini ukisema: watu wote wanalifahamu, itakuwa kadhia ni moja na hukumu itakuwa imewaenea kwa ujumla sio kwa mtu mmoja mmoja. Kwa hiyo maana ya Aya ni kuwa kila mmoja katika watu ana namna yake inayomuhusu yeye peke yake; kama vile alama za vidole, kila mmoja ana zake.

2. Imepokewa Hadith kutoka kwa Ja’far As-swadiq (a.s.) kwamba yeye amefasiri namna kwa maana ya nia. Usahihi wa tafsiri hii unafahamika kutoka na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na Mola wenu anajua aliyeongoka katika njia’ iliyokuja moja kwa moja bila ya kuweko kiunganishi kingine.” Yaani Mwenyezi Mungu anamjua anayetaka kuongoka na kufu- ata njia yake bila ya makusudio mengine yoyote isipokuwa dhati yake Aliye Mtukufu.

Kwa hiyo maana ya Aya yatakuwa: Kila mtu anafanya kulingana na nia yake na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atapambana naye kulingana na nia yake; ikiwa kheri basi ni kheri na ikiwa ni shari basi itakuwa ni shari.

Mwenye kudhihirisha kheri mbele ya watu ili awahadae watu na kumbe ana malengo ya shari, basi huyo mbele ya Mwenyezi Mungu ni mshari. Na mwenye kuiba mkate ili ajisitiri njaa baada ya kukosa budi, akiwa hana njia nyingine, basi huyo mbele ya Mwenyezi Mungu hastahiki adhabu.

Roho Inatokana Na Amri Ya Mola Wangu

Wanakuuliza kuhusu roho. Sema: roho inatokana na amri ya Mola wangu. Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.

Roho ina maana nyingi. Makusudio yake hapa ni uhai. Mtume (s.a.w.) aliulizwa kuhusu roho, Mwenyezi Mungu akamwamrisha amwambie muulizaji kuwa roho ni katika vitu vinavyopatikana kwa amri ya Mungu ambayo ni kusema ‘Kuwa na ikawa.’

Kwa ufafanuzi zaidi ni kuwa vitu viko aina mbili: Aina ya kwanza, Mwenyezi Mungu anavileta kupitia sababu za kimaumbile kutokana na maada; kama mwili wa binadamu.

Aina ya pili ni ile inayopatikana kwa kiasi cha amri tu; ambayo ni neno ‘kuwa’ Na roho ni katika aina hiyo. Aya imeliweka wazi hilo. Kwa sababu neno: ‘roho inatokana na amri ya Mola wangu,’ ni ishara ya neno ‘amri’ lilioko katika kauli yake nyingine Mwenyezi Mungu:

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَنْ يَقُولَ لَهُ كُنْ فَيَكُونُ {82}

“Hakika amri yake anapotaka kitu ni kukiambia kuwa! Na kikawa.” (36:82).

Majaribio yamethibitisha hakika hii na wakaiamini wale waliobobea na kumaliza miaka mingi kwenye utafiti wa asili ya uhai. Waliamni hakika hii baada ya kubainika kwamba sababu ya moja kwa moja ya uhai haina muungano wowote wa kuishia kwenye maada. Lau ingelikuwa inaishia kwenye maada, wangeliweza kumtengeneza binadamu kwenye viwanda vyao na maabara yao.

Wamejaribu wakashindwa: “Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu.” Yaani kadiri viwanda vyenu vinavyotengeneza vitu vya ajabu, lakini si chochote kulingana na chembe hai za nzi, sikwambii nzi mwenyewe: “Enyi watu! Umepigwa mfano, basi usikilizeni. Hakika wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, hawataumba hata nzi, wajapojumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kutoka kwake.

ضَعُفَ الطَّالِبُ وَالْمَطْلُوبُ {73}

Amedhoofika huyo mwenye kutaka na mwenye kutakiwa.”(22:73)

Umepita mfano wake katika Juz.9 ( 6:95).

Mwenyezi Mungu Na Elimu Ya Chembe Hai

Imetokea sadfa, wakati nikifasiri Aya hii, nikasoma makala katika gazeti Ruzil Yusuf la Misri1 toleo la April 1969 likiwa na maelzo haya:

“Mwili wa mtu una mamilioni ya chembe hai ambazo haziwezi kuonekana isipokuwa kwa darubini. Katika miaka ya karibuni ilikuwa ni vigumu kuweka elimu ya chembe kwa sababu wataalamu walikuwa hawawezi kuz- ifungua hizo chembe au kuzidunga sindano. Kwa vile kazi ilikuwa inahi- taji chombo kidogo kuliko milimita elfu moja, basi sindano nayo ingelihi- tajika iwe na ncha ndogo kuliko milimita milioni moja.

Hatimae walifanikiwa wataalamu kuzifungua chembe hizo kupitia mwanga, sawa na tunavyowasha sigara kutokana na mwanga wa jua kupitia kioo. Ni njia pekee iliyowawezesha wataalamu kuzifungua chembe hai na kugundua kuwa ni mkusanyiko uliosheheni makumi ya viumbe mbalimbali, kila kimoja kikiwa na sifa yake maalum na kazi yake na mfungamano ulionacho pamoja na wakazi wengine wa chembe hizo.

Kuweza kufahamu kazi hizo na mifungamano hiyo, kutahitajia miaka ya utafiti kama sio vizazi. Ndio ikaanza elimu ya chembe hai na tukawa sasa tunajua kwamba chembe hai zina mwili na viungo, utando, nyuzi na mengineyo ya kushangaza akili.

Imedhihirika kwamba chembe hai za damu ni mkusanyiko wa chembe zinazoelea. Idadi yake ni mara kumi zaidi ya watu wote. Mkusanyiko huo unatengeneza chembe nyingine kila baada ya miezi mine na kuhifadhi idadi ya chembe nyingine, kiasi ambacho zile zinazokuja hazipungui wala kuzidi zile zilizoondoka. Wala hazina matatizo ya makazi kwa sababu ya wingi, kama ilivyo kwa watu.

Hapa ndio kuna maajabu! Ubongo wa mifupa uzalishe mikondo ya damu ya aina na iliyo na kazi tofauti tofauti yenye chembe nyekundu na nyeupe zinazoua na zinazokinga. Vipi basi jinsi moja ilete jinsi nyingi tofauti tofauti? Kwani ngamia anaweza kuzaa ndovu, tena azae mamba, kisha azae kicheche? Lakini kwenye damu linapatikana hilo. Haya ni maajabu kweli! Kwa ufupi kabisa ni kwamba chembe hai hivi sasa zimekuwa ndio gumzo kubwa la utafiti wa kisayansi na njia yake mpya; pengine ni njia pekee ya kufahamu siri za uhai.”

Umeona maajabu haya! Kiumbe kidogo ambacho hakiwezi kuonekana isipokuwa kwa kukuzwa mara elfu, tena hakiwezi kupasuliwa ila kwa mwangaza. unywele kwake ni kama ndovu aliye kwenye chungu chungu.
Pamoja na yote haya, kiumbe hiki kina viungo, mishipa, utando na mengineyo; kama mwanadamu. Kisha viumbe hivi, vya ajabu, vinafanya maskani yake ndani ya mwili wa mtu, vikiwa ni mamilioni, kwa kiasi cha miezi mine kisha vinakuja vingine kwa idadi ile ile ya vile vilivyoondoka bila ya kuzidi wala kupungua; kisha vingine na vingine na kuendelea.

Je, hii yote ni sadfa? Je, sadfa inaweza kukaririka mara bilioni. Je, viungo vyote hivyo, utando na nyuzi zilizofumwa kwa nidhamu na mpangilio ni sadfa?

Je sadfa inaweza kuzalisha vitu vya aina mbali mbali kutoka katika aina moja? Maswali yote haya na mengineyo yanataka jawabu.

Hapana! Tena hapana kabisa! Hakuna tafsiri ila kuweko Mjuzi mwenye uweza wa kuumba ulimwengu na uhai kwa neno ‘Kuwa’ na ikawa.

Baada ya hayo, kila sayansi inavyozidi kupiga hatua, ndio dalili na ushahi- di wa kuweko Muumba mwenye amri, unazidi. Ametukuka Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu, aliyesema: “Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu”.

وَلَئِنْ شِئْنَا لَنَذْهَبَنَّ بِالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ ثُمَّ لَا تَجِدُ لَكَ بِهِ عَلَيْنَا وَكِيلًا {86}

Na tungelipenda, tungeliyaondoa tuliyokupa wahyi; kisha usingelipata wakili wa haya juu yetu.

إِلَّا رَحْمَةً مِنْ رَبِّكَ ۚ إِنَّ فَضْلَهُ كَانَ عَلَيْكَ كَبِيرًا {87}

Isipokuwa rehema itokayo kwa Mola wako. Hakika fadhila yake kwako ni kubwa.

قُلْ لَئِنِ اجْتَمَعَتِ الْإِنْسُ وَالْجِنُّ عَلَىٰ أَنْ يَأْتُوا بِمِثْلِ هَٰذَا الْقُرْآنِ لَا يَأْتُونَ بِمِثْلِهِ وَلَوْ كَانَ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ ظَهِيرًا {88}

Sema: Lau wangelikusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur’an, basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao.

وَلَقَدْ صَرَّفْنَا لِلنَّاسِ فِي هَٰذَا الْقُرْآنِ مِنْ كُلِّ مَثَلٍ فَأَبَىٰ أَكْثَرُ النَّاسِ إِلَّا كُفُورًا {89}

Na hakika tumewaeleza watu katika hii Qur’an kwa kila mfano, lakini watu wengi wamekataa isipokuwa kukanusha tu.
  • 1. Nimeupanga wakati wangu kwa namna hii ifuatayo: Saa nzima na nusu, kabla ya adhuhuri ni ya kununua mahitaji ya nyumbani na kusoma magazeti. Saa nzima na nusu usiku ni ya kusoma utafiti mpya wa kielimu na kijamii, mbali ya kazi nyingine za utungaji.