read

Aya 86- 89: Tungelipenda Tungeliondoa

Maana

Na tungelipenda, tungeliyaondoa tuliyokupa wahyi.

Razi anasema, katika kufasiri Aya hii, kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baada ya kubainisha, katika Aya iliyotangulia, kuwa yeye amewapa elimu kidogo tu, hapa anabainisha kwamba yeye lau angelitaka kuwaondolea hiki kidogo, angeliweza. Na hilo ni kwa kufuta kuhifadhika kwake moyoni na maandishi yake ya vitabuni.

Kisha usingelipata wakili wa haya juu yetu, utakayemtegemea akutetee kukurudishia tulichokichukua kwako. Isipokuwa rehema itokayo kwa Mola wako. Hiyo pekee ndiyo inayoweza kukurudishia ambacho tungekichukua kwako.

Hakika fadhila yake kwako ni kubwa kutokana na elimu aliyokupa na ubwana juu ya watu wote.

Sema: lau wangelikusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur’an, basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao.
Umepita mfano wake katika Juz 1 (2: 23).

Hakika tumewaeleza watu katika hii Qur’an kwa kila mfano, katika yanayohusiana na itikadi, sharia na maadili. Na tukaweka hoja mkataa na dalili wazi, lakini watu wengi wamekataa isipokuwa kukanusha tu, na kuwa mbali na haki. Kwa sababu iko chungu na ni nzito, hawawezi kuivumilia isipokuwa wenye takua.

وَقَالُوا لَنْ نُؤْمِنَ لَكَ حَتَّىٰ تَفْجُرَ لَنَا مِنَ الْأَرْضِ يَنْبُوعًا {90}

Na walisema: hatutakuamini mpaka utuchimbulie katika ardhi hii chemchemi.

أَوْ تَكُونَ لَكَ جَنَّةٌ مِنْ نَخِيلٍ وَعِنَبٍ فَتُفَجِّرَ الْأَنْهَارَ خِلَالَهَا تَفْجِيرًا {91}

Au uwe na kitalu cha mitende na mizabibu na utupitishie mito kati yake ikimiminika.

أَوْ تُسْقِطَ السَّمَاءَ كَمَا زَعَمْتَ عَلَيْنَا كِسَفًا أَوْ تَأْتِيَ بِاللَّهِ وَالْمَلَائِكَةِ قَبِيلًا {92}

Au utuangushie mbingu vipande vipande, kama ulivyodai, au utuletee Mwenyezi Mungu na Malaika ana kwa ana.

أَوْ يَكُونَ لَكَ بَيْتٌ مِنْ زُخْرُفٍ أَوْ تَرْقَىٰ فِي السَّمَاءِ وَلَنْ نُؤْمِنَ لِرُقِيِّكَ حَتَّىٰ تُنَزِّلَ عَلَيْنَا كِتَابًا نَقْرَؤُهُ ۗ قُلْ سُبْحَانَ رَبِّي هَلْ كُنْتُ إِلَّا بَشَرًا رَسُولًا {93}

Au uwe na nyumba ya dhahabu au upae mbinguni. Na hatutaamini kupaa kwako mpaka ututeremshie Kitabu tukisome. Sema: ametakasika Mola wangu! Kwani mimi ni nani, isipokuwa ni mwanadamu Mtume?

وَمَا مَنَعَ النَّاسَ أَنْ يُؤْمِنُوا إِذْ جَاءَهُمُ الْهُدَىٰ إِلَّا أَنْ قَالُوا أَبَعَثَ اللَّهُ بَشَرًا رَسُولًا {94}

Na nini kilichowazuia watu kuamini ulipowajia utume, isipokuwa walisema: je, Mwenyezi Mungu hupeleka mwanadamu kuwa Mtume?

قُلْ لَوْ كَانَ فِي الْأَرْضِ مَلَائِكَةٌ يَمْشُونَ مُطْمَئِنِّينَ لَنَزَّلْنَا عَلَيْهِمْ مِنَ السَّمَاءِ مَلَكًا رَسُولًا {95}

Sema: Lau ingelikuwa duniani kuna Malaika wanaotembea kwa utulivu, basi bila ya shaka tungeliwateremshia Malaika kuwa Mtume wao.

قُلْ كَفَىٰ بِاللَّهِ شَهِيدًا بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ ۚ إِنَّهُ كَانَ بِعِبَادِهِ خَبِيرًا بَصِيرًا {96}

Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona.