Aya 101 – 104: Tulimpa Musa Ishara Tisa
Maana
Hakika tulimpa Musa ishara tisa zilizo wazi.
Yamewishatangulia maelezo, katika Aya kadhaa, kuhusu Musa (a.s.) na watu wake na miujiza yake na pia kuhusu Firauni na wakuu wake na utaghuti wake.
Inawezekana kuwa mnasaba wa kutajwa miujiza ya Musa hapa, ni kuwa Mwenyezi Mungu alipotaja mapendekezo ya washirikina kwa Muhammad (s.a.w.), alifuatishia kuonyesha mapendekzo ya Firauni kwa Musa na matokeo yake yakawa ni balaa kwake; kwamba itatokea hivyo hivyo, lau Mwenyezi Mungu atajibu mapendekezo ya washirikina kwa Muhammad (s.a.w.).
Kwa sababu wao watayakataa yatakapowajia; sawa na walivyofanya watu wa Firauni na wangeliangamia kama alivyoangamia Firauni. Kwa hiyo kukosa kujibiwa ni heri kwao na Mwenyezi Mungu anajua yanayowafaa waja na yale ya kuwaharibia.
Musa ana ishara na miujiza mingi, ikiwemo ile ya kuifanya risala yake iwe nyepesi; kama vile kuondoka mifundo ya ulimi wake, kuneemeshwa na kufadhilishwa wana wa Israil kwa kutolewa maji katika jiwe, kuteremshiwa manna na salwa au kuhofishwa kwa kufunikwa na mlima. Mingine ni ya kumpa fundishoFirauni na watu wake ili waweze kuamini au malipo ya inadi yao.
Hiyo ndiyo miujiza tisa iliyoashiriwa na Aya. Iliyo dhahiri zaidi ni kugeuka fimbo kuwa nyoka, mkono kuwa mweupe na kuangamizwa makafiri baharini. Ama sita iliyobakia, mitano yake imeashiriwa na Aya hii:
فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمُ الطُّوفَانَ وَالْجَرَادَ وَالْقُمَّلَ وَالضَّفَادِعَ وَالدَّمَ آيَاتٍ مُفَصَّلَاتٍ فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا مُجْرِمِينَ {133}
Na wa sita ni kuangamizwa mali zao: “Na Musa akasema: Mola wetu! Hakika wewe umempa Firauni na wakuu wake mapambo na mali nyingi katika maisha ya dunia. Mola wetu! Hivyo wanawapoteza watu na njia yako.
Mola wetu! Ziangamize mali zao na zitie shida nyoyo zao. Na hawataamini mpaka waione adhabu yenye kuumiza. Akasema Mwenyezi Mungu, maombi yenu yamekubaliwa. Basi muwe na msimamo wala msifuate njia ya wale wasiojua.” Juz 11 (10: 88-89).
Waulize wana wa Israil
Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad (s.a.w.). Makusudio ya wana wa israili ni wale walioamini; kama vile Abdullah bin Salam na maswahiba zake. Lengo la swali hili na jawabu ni kuwadhihirishia mayahudi na wasiokuwa mayahudi ukweli wa Mtume mtukufu kwa kila alilowaletea kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Alipowajia na Firauni akamwambia: Hakika mimi nakuona wewe umerogwa.
Yaani umchawi, kwa maana ya kuwa umepewa elimu ya uchawi, kwa dalili ya Aya nyingine isemayo: “Wakasema wakuu wa watu wa Firauni: Hakika huyu ni mchawi mjuzi.” Juz.9 (7:109). Walisema hivyo baada ya kushuhudia fimbo inageuka kuwa nyoka mkubwa na mkono rangi ya maji ya kunde kuwa mweupe bila ya ubaya.
Akasema; hakika umekwishajua kuwa hakuziteremsha hizi isipokuwa Mola wa mbingu na Ardhi, kuwa ni dalili. Hakika mimi nakuona, ewe firauni, umeangamia.
Makusudio ya ‘hizi’ ni ishara tisa.
Firauni alipomwambia Musa, mimi nakuona u mchawi, Musa alimjibu kuwa unajua kwa hakika ukweli wa ishara na niliyokuletea na kwamba hizo ni dalili wazi kutoka kwa Mwenyezi Mungu zinazokuonyesha wewe na watu wote kuwa mimi ni mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini wewe unafanya inadi na kiburi kwa ajili ya kupupia cheo chako.
Ikiwa wewe unaniona kuwa mimi ni mchawi basi mimi ninakuona wewe umeangamia; na hayo ni malipo ya kukadhibisha kwako haki na atakayekuwako ataona. Kila mwenye kuipinga haki na akaona uzito kuambiwa basi huyo ni mwanachama wa Firauni na mila yake.
Na akataka kuwahamisha katika ardhi.
Aliyetaka kuwatoa ni Firauni, na waliotakiwa kutolewa ni Musa na watu wake. Maana ni kuwa Firauni alitaka ardhi ya Misri isikaliwe na Wana wa israil kwa kuwaua, kuwachukua mateka na kuwafukuza. Lakini janga likamgeukia yeye, kama inavyokuwa kwa kila taghuti.
Tukamzamisha yeye na waliokuwa pamoja naye wote.
Mwenyezi Mungu aliwangamiza baada ya kuwapatia hoja na dalili wazi, lakini wakakataa isipokuwa ukafiri na kupetuka mipaka.
Na tukawaambia, baada yake, wana wa Israil: kaeni katika ardhi.
Ardhi iliwakunjukia wana wa Israil, baada ya kupata amani kwa kuangamia Firauni. Mwenyezi Mungu akawapa hiyari ya kukaaa popote katika nchi. Ilitakikana washukuru Mungu kwa neema hii, lakini wao wakapetuka mipaka na wakafanya uovu:
Wakaabudu ndama badala ya Mwenyezi Mungu, wakasema: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumbwa na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu ni fukara na wao ni matajiri, wakawaua mitume, wakala haramu na riba, wakaipotoa Tawrat, wakajaribu kumuua Bwana Masih, na kumzulia mama yake uovu na mengineyo aliyoyasajili Mwenyezi Mungu katika Tawrat, Injili na Qur’an na watu wakayasajili katika vitabu vya historia na vya Hadith vya zamani na vya sasa. Uzayuni unatosha kuwa ni ushahidi wa hakika ya kikundi hiki kiovu na kwamba hicho ni shari na balaa kwa ubinadamu.
Na itakapokuja ahadi ya Akhera tutawaleta nyote pamoja.
Maneno hapa wanaambiwa wana wa Israil na akhera ni Siku ya Kiyama, kuletwa pamoja ni mkusanyiko wa wanaotofautiana. Makusudio ni kutoa hadhari na kiaga kwa wale watakokuja katika wana wa Israil kuleteta fitina na ufisadi katika nchi.
Hii ndio dhahiri ya tamko la Aya. Lau ingelikuwa inafaa kufasiri Qur’an kwa maoni yetu, basi tungelisema kuwa neno ‘kuletwa pamoja’ linaashiria kujumuika mayahudi na uzayuni, kutoka huko na huko, katika ardhi ya Palestina na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atawasalitia uovu mkali na itakuwa ni ahadi itakayotimizwa. Usawa ni tuliyoyaelezea katika Aya ya 4 ya sura hii, rudia huko.
وَبِالْحَقِّ أَنْزَلْنَاهُ وَبِالْحَقِّ نَزَلَ ۗ وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا مُبَشِّرًا وَنَذِيرًا {105}
وَقُرْآنًا فَرَقْنَاهُ لِتَقْرَأَهُ عَلَى النَّاسِ عَلَىٰ مُكْثٍ وَنَزَّلْنَاهُ تَنْزِيلًا {106}
قُلْ آمِنُوا بِهِ أَوْ لَا تُؤْمِنُوا ۚ إِنَّ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ مِنْ قَبْلِهِ إِذَا يُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ يَخِرُّونَ لِلْأَذْقَانِ سُجَّدًا {107}
وَيَقُولُونَ سُبْحَانَ رَبِّنَا إِنْ كَانَ وَعْدُ رَبِّنَا لَمَفْعُولًا {108}
وَيَخِرُّونَ لِلْأَذْقَانِ يَبْكُونَ وَيَزِيدُهُمْ خُشُوعًا ۩ {109}
قُلِ ادْعُوا اللَّهَ أَوِ ادْعُوا الرَّحْمَٰنَ ۖ أَيًّا مَا تَدْعُوا فَلَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ۚ وَلَا تَجْهَرْ بِصَلَاتِكَ وَلَا تُخَافِتْ بِهَا وَابْتَغِ بَيْنَ ذَٰلِكَ سَبِيلًا {110}
وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي لَمْ يَتَّخِذْ وَلَدًا وَلَمْ يَكُنْ لَهُ شَرِيكٌ فِي الْمُلْكِ وَلَمْ يَكُنْ لَهُ وَلِيٌّ مِنَ الذُّلِّ ۖ وَكَبِّرْهُ تَكْبِيرًا {111}