read

Aya 19 – 22: Na Kama Hivyo Tuliwainua.

Sehemu Ya Tatu

Tumeishiria, katika maelezo yaliyotangulia, kuwa Aya zinazofungamana na watu wa pango zinagawanyika kwenye sehemu nne. Timekwishataja mbili na sasa tunaendelea na sehemu mbili za mwisho. Katika sehemu ya tatu ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

Na kama hivyo tuliwainua ili waulizane.

Waliendelea na usingizi wao kwa muda wa miaka 309; kama itakvyoelezwa kwenye Aya ya 25. Kisha akawaamsha kutoka kwenye usingizi mrefu wa ajabu. Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu aliwaamsha ili waulizane muda wa usingizi wao, na watakapofahamu hakika, imani yao kwa Mwenyezi Mungu na ufufuo itazidi.

Unaweza kuuliza: Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema, katika Aya ya 16, kuwa lengo la kuwaamsha ni kuwa wajue muda wao wale waliozozana kabla ya kuamka. Na katika Aya hii anasema kuwa aliwaamsha ili waulizane wao wenyewe. Je kuna wajihi gani wa Aya hizi mbili?

Jibu: hakuna kugongana baina ya Aya mbili. Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwaamsha watu wa pango kwa mambo mawili: moja ameliashiria katika Aya iliyotangulia na jingine akaliashiria katika Aya hii. Kwa hiyo, maana ya Aya zote mbili ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwaamsha ili wajue wao na wengine kuwa Mwenyezi Mungu ana uwezo wa kufufua wafu hata muda ukirefuka.

Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Mola wenu ana- jua zaidi muda mliokaa.

Walipoamka walianza kuulizana, je mnajua mmekaa muda gani? Baadhi yao wakajibu kuwa tumekaa siku moja au baadhi ya siku. Kauli hii ni kuashiria kuwa hakuna kilichobadilika katika vitu vyao; si nguo wala nywele au kucha, nyuso, mili na hata rangi yao; ingawaje walikaaa muda mrefu. Lau kingebadilika kitu katika hivyo basi kingeonekana na wala asingesema msemaji miongoni mwao kuwa tumekaa siku moja au sehemu ya siku; kama asemavyo Razi.

Kisha wakasema tuachane na maswali haya, hakuna ajuae muda tuliokaa ila Mwenyezi Mungu.

Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi pesa zenu aende mjini akaangalie chakula kipi kilicho kisafi zaidi awaletee riziki katika hicho. na awe mwangalifu, wala asiwajulishe kwa yeyote. kwani wao wakiwajua watawapiga mawe au watawarudisha katika mila yao na hamtafaulu kabisa.
Pesa ilikuwa na sura ya mfalme wa wakati wao. inasemekana kuwa jina lake lilikuwa ni Dacianus na jina la mji lilikuwa ni Daqsus.

Waliamka na wakahisi njaa baada ya kukaa muda mrefu. Hivyo wakamtuma mmoja wao awanunulie chakula na wakamuusia awe na hadhari ili asitambuliwe na yeyote wasije wakauawa na mataghuti au wawafitini na dini yao. Hawajui kama wao wako kwenye zama nyingine

Sehemu Ya Nne

Na kama hivyo tuliwajulisha kwa watu wapate kujua kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli na kwamba saa haina shaka. Walipogombania jambo lao wao kwa wao, walisema: Jengeni jengo juu yao. Mola wao anawajua zaidi. Wakasema wale walioshinda katika shauri lao. Hakika tutawajengea msikiti juu yao.

‘Kama hivyo’ ni ishara ya kwamba kama tulivyozidisha uongofu na kutia nguvu kwenye nyoyo zao, tukawalaza kisha kuwaamsha, basi vile vile tuliwadhihirisha kwa watu au watu wa mji uliokuwa karibu na pango.

Waliogombania ni watu wa mji uliokuwa karibu na pango. Walihitalifiana watu wa mji huo kuwa je, watu wa pango wamelala au wamekufa? Hiyo ni baada ya kuona pesa ya zamani aliyokuwa nayo yule aliyetaka kununua chakula. Wakaenda pangoni na wakaona miili imelala chini haitingishiki wala kuzungumza.

Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘wale walioshinda’ inaonyesha kuwa watu wa mji waligawanyika, kuhusiana na watu wa pango. Kuna waliosema tuwaache kama walivyo, waliosema tulizibe pango na wale waliosema tuwajengee msikiti utakoswaliwa na watu; na hili ndilo lililoshinda.

Baada ya kubainisha makusudio ya matamko ya Aya tuanze ufafanuzi:

Ni kawaida ya Qur’an kuacha kutaja kila maneno ambayo yataweza kufahamika kutokana na mfumo wa maneno ulivyo au mambo ambayo yanalazimiana na hali ya tukio. Kwa misingi hii ndio kukawa kuna jumla nyingi hazipo kwa vile zinajulikana kutokana na mazingira yalivyo. Muhtasari wa jumla zisizokuwepo:

Mmoja wao alikwenda mjini kununua chakula na alikuwa na hadhari, kama alivyousiwa na wenzake. Lakini yeye akatokewa na jambo ambalo hakulifikiria; pale alipotoa pesa kwa muuza chakula na akasema hii ni hela ya zamani haitumiki hivi sasa ni ya mfalme Dacianus; kama ilivyosemekana. Yule mwenye hela akasema: itakuwaje jana na leo tu.

Habari zikaanza kuenea mjini. Walipomuuliza kuhusu habari yake na ya pesa aliyokuwa nayo, aliwaambia kuwa yeye na wenzake walikimbia na dini yao kutoka kwa mataghuti na wakaeleka kwenye pango. Mmoja wa waliokuwa pale akasema ndio nimesikia kuwa zamani kuna watu walikimbia na dini yao kwa kumhofia mfalme Dacianus aliyechorwa kwenye pesa hii na wakakimbilia pangoni. Inawezekana ndio hawa. Watu wakamiminika pangoni baada ya yule mwenye pesa kuwahi pangoni na kuwaeleza wenzake.

Hatimaye baada ya kugunduliwa, walinyenyekea kwa Mwenyezi Mungu; kama walivyonyenyekea mwanzo, walipoingia pangoni. Wakamtaka Mwenyezi Mungu awape rehema yake na awachagulie lile ambalo linamridhisha Yeye Mwenyezi Mungu. kabla hawajamaliza dua yao walianguka wote na roho zao takatifu zikahamia kwenye rehema ya Mola wao kwenye neema ya milele. Watu wakawajengea msikiti.

Ushahidi katika kisa hiki ni dalili yake ya hisia kwa yale aliyoyadokeza Mwenyezi Mungu (s.w.t.) “watu wapate kujua kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli na kwamba saa haina shaka” na kwamba binadamu ni wa milele akitoka kwenye nyumba hii na kuhamia nyumba nyingine. Ole wake tena ole wake yule anayeicha nyumba isiyoisha kwa nyumba inayoisha.

Watasema ni watatu na wanne wao ni mbwa wao. Na wanasema ni watano na wa sita wao ni mbwa wao, kwa kuvurumisha ya ghaibu. Na wanasema ni saba na wa nane wao ni mbwa wao.

Watu wametofautiana mahali palipokuwa na pango. Ikasemekana lilikuwa Palestina karibu na Baytul-muaqaddas. Ikasemekana lilikuwa Musel. Pia imesemekana lilikuwa Hispania upande wa Granada na kauli nyingi nyenginezo.

Vile vile wametofautiana kuhusu wakati wa tukio. Kuwa je lilikuwa kabla ya Bwana Masih au baada yake? Pia wametofautiana kuhusu chakula alichoambiwa anunue, kuwa je kilikuwa tende, zabibu au nyama? Bali hata wametofautiana katika rangi ya mbwa kuwa je alikuwa rangi ya kahawia au wa madoadoa. Na tofauti nyingi nyenginezo. Kwa hiyo si ajabu kutokea tofauti katika idadi ya watu wa pango.

Katika Tafsir ya Razi na Tabrasi imeelezwa kuwa ulipokuja ujumbe wa wakristo wa Najrani kwa Mtume (s.a.w.) yalipita mazungumzo kuhusu watu wa pango. Akasema mmoja katika wakiristo, anayeitwa Ya’qubiya: “Walikuwa watatu na wa nne wao ni mbwa wao.” Akasema Nasturiya: “Walikuwa ni watano na wa sita wao ni mbwa wao.” Wakasema waislamu: “Walikuwa ni saba na wa nane wao ni mbwa.”

Kisha Razi akaendelea kusema: Wafasiri wengi wamesema kuwa wao walikuwa saba na wa nane wao ni mbwa. Akataja njia nne za kusihi kauli hii. Tatu katika hizo ni za kuangaliwa na ya nne ina mwelekeo. Kwa ufupi kauli hiyo inasema kuwa kauli ya tatu na ya tano, Mwenyezi Mungu amesema huko ni kuvurumisha yasiyojulikana, lakini alipotaja ya saba akanyamaza, kwa hiyo inawajibisha kuwa ndiyo ya sawa.

Sema, Mola wangu ndiye anayejua zaidi idadi yao. Hawawajui isipokuwa wachache.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuishiria tofauti za watu kuhusu idadi ya watu wa pango na kwamba kauli zote au baadhi yake ni kusema tu bila ya uhakika, sasa anamwambia Mtume wake mtukufu:

Tofauti zote hizi hazina umuhimu; na kwamba ni juu ya kila mtu kumwachia Mungu, kuzingatia yale yaliyowapitia watu wa pango na kuyachukulia kuwa ni dalili ya ufufuo; sio kujadili idadi, mahali au wakati. Kwa sababu lengo la kisa hiki ni mazingatio na mawaidha; bali hili ndilo lengo la visa vyote vya Qur’an; ndilo la kwanza na la mwisho:

لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِأُولِي الْأَلْبَابِ ۗ {111}

“Kwa hakika katika simulizi zao mna mazingatio kwa wenye akili.” Juz.13 (12:111).

Basi usibishane juu yao ispokuwa mabishano ya juu juu; wala usiulize habari zao kwa yeyote yule.

Juu yao ni kuhusu hao watu wa pango. Yaani ewe Muhammad! Usiwe na haja kabisa ya kujadiliana na yeyote katika watu wa Kitab kuhusu idadi ya watu wa pango wala usimuulize ulama katika wao, kwani suala hilo sio lenyewe hasa; bali yule mwenye kubishana mwambie kwa upole tu; mfano Mungu ndiye ajuaye au mjadala huu hauna faida n.k.

وَلَا تَقُولَنَّ لِشَيْءٍ إِنِّي فَاعِلٌ ذَٰلِكَ غَدًا {23}

Wala kamwe usiseme kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifanya hilo kesho;

إِلَّا أَنْ يَشَاءَ اللَّهُ ۚ وَاذْكُرْ رَبَّكَ إِذَا نَسِيتَ وَقُلْ عَسَىٰ أَنْ يَهْدِيَنِ رَبِّي لِأَقْرَبَ مِنْ هَٰذَا رَشَدًا {24}

Isipokuwa akipenda Mwenyezi Mungu. Na mkumbuke Mola wako pale unaposahahu, na sema: Asaa Mola wangu akaniongoza kwenye uongozi ulio karibu zaidi kuliko huu.

وَلَبِثُوا فِي كَهْفِهِمْ ثَلَاثَ مِائَةٍ سِنِينَ وَازْدَادُوا تِسْعًا {25}

Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu na wakazidisha tisa.

قُلِ اللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثُوا ۖ لَهُ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ أَبْصِرْ بِهِ وَأَسْمِعْ ۚ مَا لَهُمْ مِنْ دُونِهِ مِنْ وَلِيٍّ وَلَا يُشْرِكُ فِي حُكْمِهِ أَحَدًا {26}

Sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi muda waliokaa. Ni zake siri za mbingu na za ardhi. Kuona kulikoje kwake na kusikia. Hawana mlinzi isipokuwa Yeye; wala hamshirikishi yeyote katika hukumu yake.