read

Aya 23-26: Inshaallah

Maana

Wala kamwe usiseme kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifaya hilo kesho; isipokuwa akipenda Mwenyezi Mungu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kumwambia usibishane, alimwamrisha afungamanishe kila jambo lake na matakwa ya Mungu.

Mtu anaweza kupitiwa akafanya lile aliloliazimia kuliacha au akaacha lile aliloliazimia kulifanya. Hili linaweza kumtokea hata maasumu, maadamu sio la kumwasi Mungu. kwa sababu isma haiwezi kuwa pamoja na maasi kwa hali yoyote ile; sawa na ambavyo elimu haiwezi kuwa pamoja na ujinga.

Utashi Mkuu

Mazingira yana athari, hilo halina shaka, lakini sio kila kitu kwa binadamu. Ni mtu gani ambaye kila analolitaka analipata? Hata awe na uwezo au cheo kiasi gani! Ni nani ambaye ameweza kumfanya mkewe au mwanawe vile anavyotaka awe kiumbo na kitabia? Ongezea mifano mingine kadiri unavyotaka. Hakuna yeyote ambaye amenyookewa na kila analolitaka; hata katika mazungumzo na usingizi.

Kwa hiyo utashi wa mtu upo na una athari yake, lakini utashi huu unahukumiwa na utashi wa Mwenyezi Mungu ambaye anasema: ukitaka jambo litafute kwa sababu zake na njia zake za kimaumbile ambazo nimeziweka, lakini angalia usinisahau. Kwani wewe unatembea kwenye njia yangu. Mimi ndiye niliyekuumba, nikakutengenezea njia na nikakupa mwongozo wa njia hiyo, tena nikakuamrisha uifuate.

Vilevileusisahaukuwanjianiliyokutengenezahaiwezikukufikisha,kwa hali yoyote ile, kwenye matakwa yako; hata ukijitahidi kiasi gani. Kwa sababu mimi vile vile nimetengeneza vikwazo kwenye njia hiyo. Si wewe wala mwingine mwenye uwezo navyo. Kwa sababu viko mikononi mwangu. Ni mimi ndiye ninayevizuia na ni mimi ndiye ninayeviachia. Usikate kabisa kuwa wewe utafika kila unapotaka; isipokuwa kwa matakwa ya juu. Tazama kifungu cha ‘Siri na matukio ya ghafla’ katika Juz.2 (2:210).

Na mkumbuke Mola wako pale unaposahahu.

Kila mtu hutokewa na kusahau; hasa akiwa ametingwa na shughuli na huzuni. Hata imesemekana neno la kiarabu insan lililo na maana ya mtu, linatokana na neno nasiya lenye maana ya mwenye kusahau.

Mwenyezi Mungu ametuamrisha tumkumbuke tunaposahau na akatu- fundisha namna ya kukumbuka pale aliposema: na sema: Asaa Mola wangu akaniongoza kwenye uongozi ulio karibu zaidi kuliko huu.
Yaani kama Mwenyezi Mungu hatanikumbusha yale niliyoyasahau. Basi yeye atanikumbusha yaliyo na masilahi na manufaa zaidi kuliko haya. Na kusahau baadhi ya mambo kuna faida zake nyingi.

Kwa mnasaba wa Aya hii tutaje kisa ambacho ni nadra kutokea cha kuhusudiana watu wa elimu ya dini; kama wanavyohusudiana wafanyakazi na wafanyabiashara:

Imepokewa riwaya kwamba Mansur alikuwa akimfadhilisha sana Abu Hanifa kuliko wanafiqh wengine. Muhammad bin Is-haq akamuonea wivu. Siku moja wakakutana wote mbele ya Mansur. Muhamad akamuuliza Abu Hanifa akikusudia kumshinda na kumnyamazisha, kama ifuatavyo:-

Muhammad: Unasemaje kuhusu mtu aliyeapa akanyamaza kwa muda, kisha akasema inshaallah.

Abu Hanifa: Kiapo chake kitafaa na atalazimiana nacho, kwa sababu kauli yake ya inshaallah imetengana na kiapo, lau haikutengana basi kiapo hak itafaa.

Muhammad: Vipi na babu wa Amir Al-muminin – akimkusudia Mansur – hasemi hivyo?

Mansur akamgeukia Abu Hanifa: Eti ni kweli babu alisema hivi?

Au Hanifa: Ndio

Mansur: Sasa unampinga babu yangu ewe Abu hanifa?

Abu Hanifa: Kauli ya babu yako ni sahihi lakina kuna taawili, inayoitoa kwenye ushahihi. Huyu Muhammad na wenzake hawakuoni kuwa wewe unastahiki ukhalifa. Kwa sababu wao wanakubai, kisha wakitoka wanasema inshaallah. Maana yake ni kuwa katika madhehebu yao wao hawakukubali kuwa wewe ni khalifa kwa kuzingatia kuwa Mwenyezi Mungu hakutaka wewe uwe khalifa.

Basi Mansur akakasirika sana akawaambia maaskari wake mchukueni huyu, akimwashiria Muhammad bin Is-haq. Basi ule mtandio wake wakauweka shingoni mwake wakamburura hadi korokoni.

Kwa mnasaba huu tunadokeza kuwa mtu akisema: nimekuuzia kitu, inshaallah au mke wangu nimemtaliki inshaallah au pia kusema: wallahi sitafanya hivi inshaalllah n.k. Basi akisema hivyo ataangaliwa: ikiwa alikusudia kutabaruku na jina tu la Mwenyezi Mungu, basi atalazimiana na aliyoyasema. Itakuwa bei yake, talaka au kiapo chake kimefungika. Ama ikiwa amekusudia kuwa hilo ni sharti basi hatalazimika na kitu kwa sababu hilo sharti litakuwa limevunja alichokisema.

Unaweza kuuliza: Je, tutajuaje alichokikusudia?

Jibu: hilo litategema msemaje yeye mwenye. Kwa sababu makusudio hayakujulikana isipokuwa kwa yule aliyekusudiwa; na kadhi atachukua kauli yake.

Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu na wakazidisha tisa.

Baada ya kutoka nje kidogo Mwenyezi Mungu amerudia kisa cha watu wa pango na kubainisha kuwa wao walibaki kwenye usingizi kwa muda wa miaka 309.

Unaweza kuuliza: Kwa nini akasema na wakazidisha tisa badala ya kusema moja kwa moja, mia tatu na tisa?

Jibu: Baadhi ya wafasiri wamejibu kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema miaka 300 kwa hisabu ya miaka ya jua na 309 kwa miaka ya mwezi. Kwa sababu tofauti kati yake ni miaka mitatu kwa kila mia.

Sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi muda waliokaa. Ni zake siri za mbingu na za ardhi.

Ndio anajua. Kwa sababu Yeye ndiye aliyewaumba, akawaongoza, akawalaza na akawaua. Na ametoa habari kuwa walikaa miaka 309. Kauli yake ni haki.

Kuona kulikoje kwake na kusikia.

Yaani anaona sana kila linaloonwa na anasikia sana kila linalosikiwa. Makusudio ni kuwa hakifichiki kwake kitu chochote.

Hawana mlinzi isipokuwa Yeye; wala hamshirikishi yeyote katika hukumu yake.

Viumbe hawana mlinzi yeyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Maana ni kuwa hakuna wa kumsaidia aliyedhalilishwa na Mungu na hakuna wa kumdhalilisha aliyesaidiwa na Mungu na wala hakuna wa kuzuia alichokitoa na kutoa alichokizuia. Kwa sababu Yeye yuko peke yake hana mshirika. Ufalme uko mikononi mwake na Yeye ni muweza wa kila kitu.

وَاتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنْ كِتَابِ رَبِّكَ ۖ لَا مُبَدِّلَ لِكَلِمَاتِهِ وَلَنْ تَجِدَ مِنْ دُونِهِ مُلْتَحَدًا {27}

Na soma uliyopewa wahyi katika kitabu cha Mola wako. Hapana wa kubadilisha maneno yake. Wala hutapata makimbilio isipokuwa kwake.

وَاصْبِرْ نَفْسَكَ مَعَ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ ۖ وَلَا تَعْدُ عَيْنَاكَ عَنْهُمْ تُرِيدُ زِينَةَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَا تُطِعْ مَنْ أَغْفَلْنَا قَلْبَهُ عَنْ ذِكْرِنَا وَاتَّبَعَ هَوَاهُ وَكَانَ أَمْرُهُ فُرُطًا {28}

Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanaomuomba Mola wao asubuhi na jioni, wakitaka radhi yake; wala macho yako yasiwaruke kwa kutaka mapambo ya maisha ya dunia; wala usimtii tuliyemghafishilisha moyo wake asitukumbuke na akafuata matamanio yake na mambo yake yakawa yamepita kiasi.

وَقُلِ الْحَقُّ مِنْ رَبِّكُمْ ۖ فَمَنْ شَاءَ فَلْيُؤْمِنْ وَمَنْ شَاءَ فَلْيَكْفُرْ ۚ إِنَّا أَعْتَدْنَا لِلظَّالِمِينَ نَارًا أَحَاطَ بِهِمْ سُرَادِقُهَا ۚ وَإِنْ يَسْتَغِيثُوا يُغَاثُوا بِمَاءٍ كَالْمُهْلِ يَشْوِي الْوُجُوهَ ۚ بِئْسَ الشَّرَابُ وَسَاءَتْ مُرْتَفَقًا {29}

Sema hii ni kweli itokayo kwa Mola wenu, basi atakaye aamini na atakaye akufuru. Hakika sisi tumewaandalia wenye kudhulumu moto ambao hema lake litawazunguka. Na wakiomba msaada watapewa maji kama mafuta yaliyotibuka yanayobabua nyuso. Kinywaji kibaya kilioje na mahali pabaya palioje pa kupumzika!