read

Aya 45 – 46: Pambo La Maisha Ya Dunia

Maana

Na wapigie mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tuliyoyateremsha kutoka mbinguni yakachanganyika na mimea ya ardhi ikawa majani makavu yaliyokatikakatika yanayopepeprushwa na upepo.

Dunia ni nzuri yenye mandhari ya kijani ya kupendeza, lakini ina ghururi na madhara. Haina kheri katika akiba yake isipokuwa takua; kama alivyosema Imam Ali (a.s.).

Haya ndiyo maana ya Aya; ambapo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameifananisha dunia, katika uzuri wake, na mvua iliyonyesha kwenye ardhi ikairutubisha na ikaota miti ya kila aina, lakini mara inageuka na kuwa kame, majani yakawa makavu yanayopukusika yakirushwa na upepo. Hivi ndivyo yalivyo maisha ya dunia, ni mazuri lakini yameficha ubaya.

Na Mwenyezi Mungu ana uwezo juu ya kila kitu.

Anaweza kuuondoa ulimwengu na kuumaliza kabisa; kama alivyoweza kuumba na kuuleta. Anasema Ibnul Arabi katika kitabu Futahitl-Makkiyya “Mwenyezi Mungu ni muweza wa mambo na ana uwezo wa kuumba” Anakusudia kuwa Mwenyezi Mungu anasifika kuwa ni muweza pale anapotaka kitu kuwa kikawa, ni sawa aseme au asieme na anasifika kuwa ana uweza pale anaposema na kitu kikawa vilevile.

Mali Na Watoto Ni Pambo La Maisha Ya Dunia

Mali na watoto ni pambo la maisha ya dunia.

Pambolamaishalikoainambili:Laummanalakibinafsi.Laummani kama vile kujenga njia za mawasiliano; mfano barabara n.k. Au taasisi; mfano kujenga vyuo vikuu, vituo vya malezi ya watoto viwanda n.k.

Na la kibinafsi ni kama nyumba, gari, mtoto mtiifu aliyefaulu, viwanda, umaarufu katika jamii n.k. Vipambo hivi sio haramu. Vitakuwaje haramu na hali Yeye ndiye aliyesema:

“Sema: Ni nani aliyeharamisha pambo la Mwenyezi Mungu ambalo amewatolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki?” Juz. 8 (7:32).

Lakini pambo binafsi halistahili mtu kujitukuza na kujifaharisha nalo. Kwa sababu kipimo cha kutukuzwa pambo ni kwa manufaa ya umma na kubakia vizazi na vizazi. Hili ndilo alilolikusudia Mwenyezi Mungu pale aliposema:

Na vibakiavyo vizuri ndivyo bora mbele ya Mola wako na kwa malipo na tumaini bora.

Kwa sababu mwenye kutekeleza atapata huko Akhera yale aliyoyatumai, mbali ya kupata heshima na kuendelea kutajika katika maisha haya ya dunia.

Kwa ufupi ni kuwa mali ni nyenzo sio lengo. Inapimwa na kukadiriwa kwa natija yake na athari yake. Ikiwa ni kheri itakuwa kheri na ikiwa ni shari basi itakuwa shari. Ikitumika kwa njia ya shari na ufisadi, kama vile mashindano ya silaha, basi itakuwa mali ni shari na ikitumika katika kutekeleza mahitaji, basi mali itkuwa ni kheri.

Na kheri hiyo iko aina mbili: Ikiwa itamletea manufaa mwenye nayo au kumkinga na madhara basi itakuwa ya binafsi na itaisha kwa kuisha. Lakini ikiwa manufaa yake ni kwa umma basi itakuwa ni katika vibakiavyo vizuri.

وَيَوْمَ نُسَيِّرُ الْجِبَالَ وَتَرَى الْأَرْضَ بَارِزَةً وَحَشَرْنَاهُمْ فَلَمْ نُغَادِرْ مِنْهُمْ أَحَدًا {47}

Na siku tutakayoipitisha milima na utaiona ardhi iwazi. tutawafufua wala hatuta- muacha yeyote katika wao.

وَعُرِضُوا عَلَىٰ رَبِّكَ صَفًّا لَقَدْ جِئْتُمُونَا كَمَا خَلَقْنَاكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ ۚ بَلْ زَعَمْتُمْ أَلَّنْ نَجْعَلَ لَكُمْ مَوْعِدًا {48}

Na watahudhurishwa mbele ya Mola wako kwa safu. Hakika mmetufikia kama tulivyowaumba mara ya kwanza; bali mlidai kuwa hatutawawekea miadi.

وَوُضِعَ الْكِتَابُ فَتَرَى الْمُجْرِمِينَ مُشْفِقِينَ مِمَّا فِيهِ وَيَقُولُونَ يَا وَيْلَتَنَا مَالِ هَٰذَا الْكِتَابِ لَا يُغَادِرُ صَغِيرَةً وَلَا كَبِيرَةً إِلَّا أَحْصَاهَا ۚ وَوَجَدُوا مَا عَمِلُوا حَاضِرًا ۗ وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا {49}

Na kitabu kitawekwa ndipo utawaona waovu wakiogopa kwa sababu ya yale yaliyomo. Na watasema: “Ole wetu! Kina nini kitabu hiki hakiachi dogo wala kubwa ila kinalihesabu? Na watakuta waliyoyafanya yamehudhurishwa. Na Mola wako hadhulumu yoyote.