Aya 47 -49: Tutawafufua Wala Hatutamuacha Yeyote
Maana
Na siku tutakayoipitisha milima na utaiona ardhi i wazi.
Ardhi hii tunayoishi leo, Mwenyezi Mungu ameitaja katika Aya nyingi, miongoni mwazo ni hii tuliyo nayo. Hapa Mwenyezi Mungu ameisifu kwa sifa mbili:
Kwanza, kuwa Mwenyezi Mungu ataing’oa milima mahali ilipo na aipeleke kama mawingu. Sifa ya pili, kwamba ardhi yote kuanzia pembe hadi pembe itakuwa wazi bila ya kuweko kizuizi chochote. Hapo ndio itakuwa ufufuo ambao Mungu ameuashiria kwa kusema:
Na tutawafufua wala hatutamuacha yeyote katika wao.
Mwenyezi Mungu atawafufua wote, kuanzia wa kwanza hadi wa mwisho, kwa ajili ya hisabu.
Na watahudhurishwa mbele ya Mola wako kwa safu.
Huko nyuma tumetaja kuwa hisabu na malipo ni kweli isiyokuwa na shaka. Tumelithibitisha hilo kwa dalili mkataa, katika kufasiri Aya zinazoonyesha hivyo; miogoni mwazo ni, Juz. 11 (10:4) kifungu cha ‘Hisabu na malipo ni lazima’.
Aya tuliyo nayo inasema kuwa viumbe watahudhurishwa kwa Mungu kesho wakiwa wamepiga safu. Makusudio ya kuhudhurishwa hapa ni kusimama kwa Mungu kwa ajili ya hisabu.
Ama kuhusu neno safu, wafasiri wametofautiana; wengine wameliacha neno na dhahiri yake, wengine wakaleta sarufi na kulichukulia tamko yale yasiyowezekana. Tuonavyo sisi ni kuwa safu ni fumbo la utaratibu na nidhamu, kwamba viumbe watahudhurishwa kwa mola wao kwa mpangilio madhubuti.
Hakika mmetufikia kama tulivyowaumba mara ya kwanza; bali mlidai kuwa hatutawawekea miadi.
Hivi ndivyo atakavyoanza Mwenyezi Mungu kuwahukumu wale waliokuwa wakipinga ufufuo: Tuliwatoa matumboni mwa mama zetu mkiwa uchi hamna chochote; vilevile leo tumewatoa makaburini mwenu. Hakuna tofauti isipokuwa pale mwanzo mlikuwa hamuulizwi chochote na leo mmetolewa ili muulizwe yale mliyokuwa mkiyafanya, kuyaamini na kuyasema. Miongoni mwayo ni kusema kwenu kuwa ufufuo ni uzushi na vigano. Je, mmeona leo?
Na kitabu kitawekwa ndipo utawaona waovu wakiogopa kwa sababu ya yale yaliyomo.
Hii ndiyo Siku ya Ufufuo mliyokuwa mkiikadhibisha. Kila mmoja atapewa daftari la matendo yake na aambiwe:
اقْرَأْ كِتَابَكَ كَفَىٰ بِنَفْسِكَ الْيَوْمَ عَلَيْكَ حَسِيبًا {14}
Yaani soma daftari la matendo yako na ujipigie mahisabu wewe mwenyewe. Atasoma huku akitetemeka kwa hofu isiyokuwa na matumini yoyote wala matarajio ya kuokoka. Lau angeliogopa adhabu tangu mwanzo na kajiepusha na njia yake, angelikuwa leo yuko kwenye amani na sala- ma. Lakini alijiaminisha huko na anahofu hapa.
Na watasema: ole wetu! Kina nini kitabu hiki hakiachi dogo wala kubwa ila kinalihesabu?
Hapo mwanzo walikuwa wakisema hakuna kitabu wala hisabu.
Na watakuta waliyoyafanya yamehudhurishwa, bila ya kuzidi wala kupungua. Kwanini isiwe hivyo na Mola wako hadhulumu yoyote? Si kwenye thawabu wala adhabu; bali huwa zikaongezwa thawabu kwa mwenye kufanya wema na kusamehewa mwenye kufanya uovu.
وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ فَفَسَقَ عَنْ أَمْرِ رَبِّهِ ۗ أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاءَ مِنْ دُونِي وَهُمْ لَكُمْ عَدُوٌّ ۚ بِئْسَ لِلظَّالِمِينَ بَدَلًا {50}
مَا أَشْهَدْتُهُمْ خَلْقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلَا خَلْقَ أَنْفُسِهِمْ وَمَا كُنْتُ مُتَّخِذَ الْمُضِلِّينَ عَضُدًا {51}
وَيَوْمَ يَقُولُ نَادُوا شُرَكَائِيَ الَّذِينَ زَعَمْتُمْ فَدَعَوْهُمْ فَلَمْ يَسْتَجِيبُوا لَهُمْ وَجَعَلْنَا بَيْنَهُمْ مَوْبِقًا {52}
وَرَأَى الْمُجْرِمُونَ النَّارَ فَظَنُّوا أَنَّهُمْ مُوَاقِعُوهَا وَلَمْ يَجِدُوا عَنْهَا مَصْرِفًا {53}