read

Aya 71 – 74: Wakaondoka

Kujizuia Na Yanayotatiza

Aya hizi zinafahamisha kuwa kuna mambo amabayo dhahiri ni rehema na undani wake ni adhabu na mengine ni kinyume. Na kwamba hukumu kwenye mambo ya namna hiyo ni kungoja kuyaamulia mpaka upatikane uhakika.

Imepokewa Hadithi mutawwatir. Kutoka kwa Mtume mtukufu (s.a.w.) kuwa yeye amasema: “Halali iko wazi na haramu iko wazi na baina ya halali na haramu kuna mambo yenye kutatiza.”

Watu wengi hawajui ni halali au ni haramu. Mwenye kuyaaacha kwa kuilinda dini yake na heshima yake, atakuwa amesalimika. Na mwenye kuijingiza kwenye kitu chochote katika hivyo, basi atakuwa anakurubia kuingia katika haramu.” Hadithi nyingine inasema: “Kujizuia na yenye kutatiza ni bora kuliko kujiingiza kwenye maangamizi.”

Kuna mapokezi yanayosema kwamba Luqman, mwenye hekima, aliingia kwa Daud akamkuta anatengeneza deraya, naye alikuwa hajapata kuiona. Akataka kumuuliza, lakini akaona bora angoje. Daud alipomaliza kuitengeza, aliivaa huku akisema: nguo nzuri sana hii ya vita. Akafahamu Luqman kuwa ile nguo ni ya vita. Akasema: “Kunyamaza ni hekima.”
Ni wachache sana wanoweza kuvumilia hivyo. Yule mtu mwema ameleta mambo matatu ya ushahidi wa hakika hii, kama ifuatavyo:

1. Basi wawili hao wakaondoka, mpaka walipopanda jahazi akalitoboa.

Musa alikwenda na yule mwenzake kwenye ufuo wa bahari. Walipokuta jahazi, wakamwomba mwenyewe awachukue, akakubali.

Walipofika katikati ya bahari, yule mja mwema alilitoboa, kiasi ambacho wangeweza kuzama na kufa maji. Musa akashtuka na jambo hili baya na akasema: Unalitoboa ili uwazamishe watu wake? Hakika umefanya jambo baya kabisa. Musa akachukua nguo yake akaziba ile tundu; kama wanavyodai wafasiri.

Akasema: Sikukuambia kuwa wewe hutaweza kuvumilia kuwa pamoja nami?

Hapo anamkumbusha lile sharti la kutomuuliza kitu. Musa akaomba msamaha na akasema: Usinichukulie kwa niliyosahau. Kwa sababu kusahau hakuna neno wala usinipe uzito kwa jambo langu. Yaani usinid- hikishe kwa kusuhubiana na wewe.

2. Basi wawili hao wakaondoka, mpaka wakamkuta kijana; akamuua.

Moyo wa Musa ukafazaika kutokana na mauaji, akasema: Umemuua mtu asiye na kosa na hakuua! Hakikia umefanya jambo baya. Huyu maskini amefanya nini? Unamuua bure tu. Huu ni ubaya wa wazi.