Aya 75 – 82: Huwezi Kuvumilia
Maana
Juzuu ya 15, imeishia na Aya ya kuuliwa kijana na mshangao wa Musa kwa tendo hilo. Kwenye Aya hii swahibu wa Musa anamkumbusha kuhusu walivyoahidiana:
Akasema: “Sikukuambia kuwa wewe hutaweza kuvumilia kuwa pamoja nami?
Anamkumbusha tena lile sharti na Musa naye anaomba tena msamaha akasema: Nikikuuliza tena kitu baada ya haya usifuatane nami.
Hapo mwanzo yule mtu alimuwekea sharti Musa, hivi sasa Musa anajiwekea mwenyewe sharti kwamba asisuhubiane naye tena kama atamuuliza, na waumini wanalazimiana na masharti yao; sikwambii tena mitume.
Kwani umekwishapata udhuru kwangu. Sababu zote zitakuwa zimekwisha.
Basi wawili hao wakaondoka, mpaka wakawafikia watu wa mji mmoja.
Huuniushahidiwatatuwakuwaniwachachewanaovumilia.Ushahidiwa kwanza na wa pili umekwishapita kwenye Juzuu ya 15. Inasemekana mji huo walioufikia ni Antioch. Katika riwaya iliyopokewa kwa Imam Jafar As-Swadiq, inasema kuwa ni Nazarethi1.
Wakawaomba watu wake wawape chakula, lakini nao wakakataa kuwakaribisha.
Wafasiri wanasema kuwa Mwenyezi Mungu amesema walikataa kuwakaribisha, badala ya walikataa kuwapa chakula, kwa vile watu wa mji ule walikuwa wabaya sana. Kwani hakuna anayemkataa mgeni ila mtu mbaya, hasa ikiwa mgeni ni wa mbali.
Hapo wakakuta ukuta unataka kuanguka, akausimamisha.
Hapo, ni hapo kwenye mji. Aliyeusimamisha, ni yule mja mwema. Kutaka kuanguka, ni kukurubia kuanguka. Maana ni kuwa Musa na mwenzake walikuta ukuta unakaribia kuanguka, yule mwenzake akautengeneza bila ya malipo yoyote.
Ndipo Musa akastaajabu na akasema: Ungelitaka ungelichukua ujira kwa haya.
Unafanya kazi ya bure tu kwa watu waliokataa hata kutukaribisha tukiwa na shida. Kutoboa jahazi na kuua kijana ni mifano miwili yenye dhahiri ya ubaya na kusimamisha ukuta ni kinyume cha mifano hiyo miwili.
Akasema: Huku ndio kufarikiana baina yangu na wewe. Nitakueleza taawili ya yale uliyokuwa huwezi kuyavumilia.
Mja mwema alitoa sharti kwa Musa la kutoulizwa, Musa akakubali, lakini pamoja na hayo akauliza. Alipokumbushwa akaomba msamaha. Tena akauliza baada ya msamaha. Alipokumbushwa mara ya pili akajiwekea sharti yeye mwenyewe la kutofuatana naye kama atauliza tena. Lakini bado akauliza, ingawaje alikuwa na hamu sana ya kufuatana naye.
Musa hana lawama yoyote katika yote aliyoyauliza. Kwa sababu nafsi yake inaweza kuvumilia mambo ya kheri na mazuri, lakini yale anayoyaona ni mabaya, hakuweza wala hataweza kuvumilia; hata kama hilo litapelekea kuvunja masharti na maelewano. Ni kipimo gani cha masharti kinachoweza kupimwa kuacha mema na kukataza mabaya.
Imani sahihi haiwezi kuzuiwa na kitu chochote, si msukumo wa nafsi wala mengineyo. Hakuna kitu kigumu zaidi kuliko imani sahihi; na atakayeshindwa na kitu chochote katika hivyo basi hana imani sahihi; hata akiswali, kufunga na kuhiji Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu.
Huku ndio kufarikiana baina yangu na wewe, ushike njia yako nami nishike yangu. Hivyo ndivyo alivyomwambia Musa. Lakini kabla ya kutengana, yule mja mwema alimwambia Musa hekima ya yale aliyoyapinga, kama ifuatavyo:
Ama lile jahazi lilikuwa ni la maskini wafanyao kazi baharini. Nilitaka kulitia kasoro, kwani nyuma yao kulikuwa na mfalme anayenyang’anya majahazi yote.
Mwenye akili anavumilia madhara kwa ajili ya kuondoa madhara makubwa; kama anavyosema mshairi: “Nimevumilia nusu shari kihofia shari yote.”
Kuanzia hapa ndio mafaqihi wakaafikiana kuwa dhara kubwa inakingwa na dhara hafifu na yakiingiliana maovu mawili litaangaliwa lile lenye madhara zaidi kwa lile lililo na machache. Kutokana na kawaida hii wametoa hukumu nyingi, kama vile kuruhusiwa kukata kiungo ikiwa kitamletea mtu maangamizi.
Ama yule kijana wazazi wake walikuwa waumini, tukahofia asiwahangaishe kwa uasi na kufuru. Basi tulitaka Mola wao awabadilishie aliye bora zaidi kuliko huyo kwa kutakasika na aliye karibu zaidi kwa huruma.
Imepokewa riwaya kutoka kwa Imam Jafar As-Swadiq (a.s.) kuwa huyo kijana aliuawa katika rika la balehe na alikuwa kafiri. Akifanya juhudi kuwaingiza wazazi wake kwenye ukafiri, sawa na wanavyofanya baadhi ya vijana wa kileo.
Tumewahi kuwona maulama wengi wa kidini waliokuwa ni tegemeo kubwa la watu, lakini mara tu walipobalehe vijana wao, wakabomoa yote waliyojenga baba zao kwa muda mrefu.
Kuna kauli mashuhuri ya Imam Ali (a.s.): “Zubeir aliendelea kuwa nasi mpaka alipokuwa na kijana wake Abdullah”
Ahmad Amin wa Misr, katika kitabu Hayati (maisha yangu), anasema: “Hivi sasa mimi na uzee wangu ninakubali kila ambalo nilikuwa nikilikataa na huwa ninaacha misimamo niliyokuwa nayo kwa sababu ya watu na mazungumzo yao na wingi wa watoto.”
• Udogo sikutaka Hawa nafsi yangu
• Zama zikakatika kawa na mvi zangu
• Hawa zikanishika kinyume matakwa yangu
• Laitani ngezalika nao ukubwa wangu
• Udogo wa marika kupinga nafsi yangu
Na ama ukuta ulikuwa ni wa vijana wawili mayatima kule mjini, na chini yake ilikuwako hazina yao, na baba yao alikuwa ni mtu mwema. Basi Mola wako alitaka wafikie kukomaa na wajitolee hazina yao. Ni rehema itokayo kwa Mola wako. Hayo sikuyatenda kwa amri yangu. Hiyo ndiyo tafsiri ya ambayo hukaweza kuyavumilia.”
Kwa ufupi ni kuwa ukuta ulikua wa watoto wawili na chini yake kulikuwa na dafina yao. Mwenyezi Mungu akataka kuilinda mali hiyo isipotee, kwa kubakia ukuta, mpaka wawe wakubwa au wawe na akili, kisha wajitolee mali yao wao wenyewe; na mzazi wao alikuwa mtu mwema “Na wema wa mtu mumini, Mwenyezi Mungu huufanya kwa mtoto wake na mtoto wa mtoto wake.”
Funzo la kisa hiki ni kwamba mtu asijione ni yeye tu na asifanye haraka kujiamulia jambo kwa kuangalia upande mmoja, bali ni lazima aangalie pande zote kwa undani na kulinganisha kisha aangalie ulio bora zaidi; kwani masilahi huwa yanasigana na madhara.
Hakuna jambo lolote la manufaa isipokuwa lina baadhi ya madhara ndani yake; kama ambavyo hakuna jambo lolote ila lina baadhi ya manufaa. Siku zote mazingatio ni kwa lililo na wingi.
وَيَسْأَلُونَكَ عَنْ ذِي الْقَرْنَيْنِ ۖ قُلْ سَأَتْلُو عَلَيْكُمْ مِنْهُ ذِكْرًا {83}
إِنَّا مَكَّنَّا لَهُ فِي الْأَرْضِ وَآتَيْنَاهُ مِنْ كُلِّ شَيْءٍ سَبَبًا {84}
فَأَتْبَعَ سَبَبًا {85}
حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ مَغْرِبَ الشَّمْسِ وَجَدَهَا تَغْرُبُ فِي عَيْنٍ حَمِئَةٍ وَوَجَدَ عِنْدَهَا قَوْمًا ۗ قُلْنَا يَا ذَا الْقَرْنَيْنِ إِمَّا أَنْ تُعَذِّبَ وَإِمَّا أَنْ تَتَّخِذَ فِيهِمْ حُسْنًا {86}
قَالَ أَمَّا مَنْ ظَلَمَ فَسَوْفَ نُعَذِّبُهُ ثُمَّ يُرَدُّ إِلَىٰ رَبِّهِ فَيُعَذِّبُهُ عَذَابًا نُكْرًا {87}
وَأَمَّا مَنْ آمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَلَهُ جَزَاءً الْحُسْنَىٰ ۖ وَسَنَقُولُ لَهُ مِنْ أَمْرِنَا يُسْرًا {88}
ثُمَّ أَتْبَعَ سَبَبًا {89}
حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ مَطْلِعَ الشَّمْسِ وَجَدَهَا تَطْلُعُ عَلَىٰ قَوْمٍ لَمْ نَجْعَلْ لَهُمْ مِنْ دُونِهَا سِتْرًا {90}
كَذَٰلِكَ وَقَدْ أَحَطْنَا بِمَا لَدَيْهِ خُبْرًا {91}
ثُمَّ أَتْبَعَ سَبَبًا {92}
- 1. Antioch ni mji ulioko Syria na Nazareth (kwa kiarabu Naswira) uko kaskazini mwa Palestina, mji wa Bikira Maryam. Aliishi hapo Bwana Masih ndio akaitwa Mnazareth (kwa kiarabu Mnaswara) na wakristo wakawa wanaitwa Wanaswara -Mtarjumu.