Aya 93 – 100: Juju Na Majuju
Maana
Kisha akafuata sababu
Dhul-qarnaini alirejea mji wa tatu ulioko katika Bahari nyeusi, unaokaliwa na Slaves1 -kama ilivyosemekana - ambao Mwenyezi Mungu ameuashiria kwa kauli yake:
Hata alipofikia baina ya milima miwili, alikuta nyuma yake watu ambao takriban hawakuwa wakifahamu kauli.
Watu aliowakuta huko walikuwa hawafahamu lugha yake wala hakufaamu lugha yao, lakini walielewana kwa ishara au kwa mkalimani; kama anavyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Wakasema: “Ewe Dhul-qar-nain! Hakika Juju na Majuju wanafanya ufisadi katika nchi. Basi je, tukulipe ujira ili utujengee baina yetu na wao ngome?
Sheikh Maraghi anasema katika Tafsir yake: “Juju ni wa Tatars, na Majuju ni wa Mongoli. Asili yao wanatokana na baba mmoja anayeitwa Turk. Miji yao inaanzia Tibet na China hadi kwenye Bahri iliyoganda. Miongoni mwao ni Changez Khan na Halako.
Kisha akanukuu Maraghi Jarida la Al-Muqtatif la mwaka 1888, kwamba jengo la ukuta wa Dhul-qarnain liko nyuma ya Amou–Daria sehemu za Balkh. Jina lake hivi sasa ni mlango wa chuma na liko karibu na mji wa Tirmidh.
Mtaalamu mmoja wa kijerumani Cyllid Burger, amelitaja katika safari zake zilizokuwa mwanzoni mwa karne ya 15. Vilevile amelitaja mwana historia wa Kihispania Clavijo katika safari zake za mwaka 1402 A.D.
Vyovyote iwavyo ni kwamba watu walimtaka Dhul-qarnain awajengee ngome itakayowakinga na Juju na Majuju waliokuwa wakiishambulia nchi yao, wakiwapa adhabu mbaya ya kuwaua, kuwateka na kupora. Wakajiwekea sharti la kumlipa katika mali zao ikiwa atawajenega ngome.
Akasema: Yale Mola wangu aliyoniwezesha na akanipa utawala na mali ni bora kuliko yale aliyowapa Mwenyezi Mungu. Nyinyi wenyewe mna haja kubwa ya mali yenu, basi itumieni kwenye masilahi yenu.
Lakini nisaidieni kwa nguvu nijenge kizuizi baina yenu na wao.
Makusudio ya nguvu hapa ni wafanyikazi na vifaa vya ujenzi.
Nileteeni vipande vya chuma. Hata alipojaza baina ya nafasi iliyo kati ya milima miwili.
Yaani alipoletewa vyuma alivipanga mpaka vikajaza nafasi iliyo baina ya milima miwili, kisha wakamletea kuni akawasha moto akaweka mifuo akasema: Vuvieni. Hata alipokifanya (chuma) moto akasema: Nileteeni shaba iliyoyeyuka niimwagie.
Wakamletea, akamwagia kwenye vyuma vilivyo moto, vikashikana, ukawa mlima wa chuma.
Hawakuweza kuukwea hao Juju na Majuju, kutokana na urefu na kuteleza wala hawakuweza kuutoboa kutokana na ugumu wake na maki yake.
Akasema: Hii ni rehema itokayo kwa Mola wangu.
Aliyesema ni Dhul-qarnain, akimshukuru Mola wake (s.w.t.) kwa rehema na neema hii aliyoitimiza mikononi mwake. Hivi ndivyo anavyokuwa mumin mwenye ikhlasi. Anamnyenyekea Mwenyezi Mungu na kushukuru kila zinapokuwa neema za Mwenyezi Mungu kupitia kwake.
Kujengwa kwa ngome hii ni usadikisho wa mfano kuwa katika historia ya binadamu kulikuwa na kusaidiana baina ya mataifa makubwa na yale madogo yanayoendelea; baina ya taifa lililo na nyenzo za maendeleo na lile lisilokuwa nazo.
Nguvu za Amerika zinafanana sana na nguvu za Dhul-qarnaini, kwa vile haziwezi kukabiliwa na yoyote, lakini kuna tofauti kubwa ya matokeo na natija. Wakati nguvu zote za Dhul-qarnain zilkuwa ni utawala wa kheri ya ubinadamu na ufanisi wake, lakini nguvu za Amerika ni za kuhami uovu wa uzayuni na kutawala nyenzo zote, masoko yote kwa masilahi ya ukoloni na kuwadumaza watu kwa kila namna.
Ushahidi wa hayo hauna idadi. Kuanzia kuusaidia uzayuni dhidi ya waarabu na ubaguzi wa rangi ndani ya Amerika hadi Rhodesia,2 mapinduzi ya kijeshi katika nchi za kiafrika3 na kuwapiga vita wapigania ukombozi huko Kongo na kila mahali. Ama huko Vietnam ndio haisemeki. Wamekusanya majeshi na kutumia kila walicho nacho, lakini ukakamavu wa wananchi wa Vietnam umetoa somo kwa Amerika, ambalo hawatalisahau maisha.
Kwa hiyo kila ushindi wanaoupata Amerika wajue huo ni wa muda tu, utaondoka kwa upinzani wa wananchi ambao unazidi siku baada ya siku.
Itakapofika ahadi ya Mola wangu atauvunja vunja.
Yaani huo mlima atauvunja vunja. Maana ni kuwa utakapokurubia wakati wa kutokea Juju na Mjuju nyuma ya ukuta, Mwenyezi Mungu ataleta sababu za kuvunjika kwake.
Na ahadi ya Mola wangu ni kweli haina shaka.
Shekh Maraghi anasema: “Ahadi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ilifika kwa kutoka Changez Khan wakafanya ufisadi katika ardhi”.
Katika Tafsir Ar-Razi imeelezwa kuwa maana ya ahadi hapa ni siku ya Kiyama. Katika Tafsir At-Twabariy imeelezwa ni baada ya kuuliwa Dajjal.
Ama sisi tunapondokea kwenye kauli ya Maraghi, kwa sababu iko karibu na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Na siku hiyo tutawaacha wakisongana wao kwa wao.
Kwani tunafahamu kuwa Juju na Majuju wataenea katika ardhi baada ya kuharibika ngome na wataharibu maisha ya watu. Mwenyezi Mungu anasema:
حَتَّىٰ إِذَا فُتِحَتْ يَأْجُوجُ وَمَأْجُوجُ وَهُمْ مِنْ كُلِّ حَدَبٍ يَنْسِلُونَ {96}
Zaidi ya hayo ni kwamba lau ingelikuwa makusudio ya ahadi yake ni Kiyama au baada ya kufa Dajjal, ingelikuwa ngome bado ipo; na kama ipo basi ingelionekana, hasa kwa kuzingatia kuwa elimu imefanya dunia hivi sasa, pamoja na wakazi wake, ni kama familia moja inayoishi kwenye nyumba moja.
Na parapanda itapuziwa na wote watakusanywa pamoja.
Hii ndiyo siku ya mwisho kwa wale wa mwanzo na wa mwisho. Katika Tafsir Attwabariy imeelezwa kuwa Mtume (s.a.w.) aliulizwa kuhusu Parapanda, akasema ni pembe itakayopuziwa.
Baada ya hayo yote, tunapenda kujulisha kuwa tuliyoyaeleza au kuyanukuu kutoka kwa wengine kuhusiana na Juju na Majuju, ni kwa njia ya kuleta karibu ufahamisho sio uhakika hasa.
Kwa vile hatukupata rejea za kutegemewa. Kwa sababu hiyo basi tutuatosheka na dhahiri ya Qur’an Tukufu na kuwaachia ufafanuzi wenzetu wengine.
الَّذِينَ كَانَتْ أَعْيُنُهُمْ فِي غِطَاءٍ عَنْ ذِكْرِي وَكَانُوا لَا يَسْتَطِيعُونَ سَمْعًا {101}
أَفَحَسِبَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَنْ يَتَّخِذُوا عِبَادِي مِنْ دُونِي أَوْلِيَاءَ ۚ إِنَّا أَعْتَدْنَا جَهَنَّمَ لِلْكَافِرِينَ نُزُلًا {102}
قُلْ هَلْ نُنَبِّئُكُمْ بِالْأَخْسَرِينَ أَعْمَالًا {103}
الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا {104}
أُولَٰئِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ وَلِقَائِهِ فَحَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فَلَا نُقِيمُ لَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَزْنًا {105}
ذَٰلِكَ جَزَاؤُهُمْ جَهَنَّمُ بِمَا كَفَرُوا وَاتَّخَذُوا آيَاتِي وَرُسُلِي هُزُوًا {106}