read

Aya 108 – 110: Walioamni Na Wakatenda Mema

Maana

Hakika wale ambao wameamini wakatenda mema, mashukio yao yatakuwa kwenye Pepo za Firdausi.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwahidi makafiri moto, sasa anatoa ahadi ya Pepo kwa waumini. Firdausi ni katika Pepo ya daraja ya juu. Mtume Mtukufu (s.a.w.) amesema: “Mkimuomba Mwenyezi Mungu muombeni Firdausi.”

Watadumu humo; hawatataka kuondoka.

Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atawalipa wema yale ambayo hawatataka mengine, tosha kabisa! Yanatosheleza yote wanayoyataka. Aya inaashiria kuwa hakuna tamaa huko Akhera; vinginevyo ingelikuwa hakuna kutosheka. Kwani mwenye tamaa hatosheki.

Sema: Lau bahari ingelikuwa ndio wino kwa maneno ya Mola wangu, basi bahari ingemalizika kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu, hata tungeleta mfano wake kuongezea.

Bahari ni jina la jinsi, linaenea kwenye bahari zote. Makusudio ya kabla ya kumalizika maneno, ni kuwa hayamaliziki na mfano wake ni mfano wa bahari. Maana ni kuwa lau tuchukulie kuwa bahari zote ni wino wa kuandika maneno ya Mwenyezi Mungu zisingetosha na maneno ya Mwenyezi Mungu yangelibakia bila ya kikomo.

Aya nyingine yenye maana hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na lau miti yote iliyomo ardhini ikawa ni kalamu na bahari (ikawa wino) na ikaongezewa bahari nyingine saba, maneno ya Mwenyezi Mungu yasingelimalizika.” (31:27).

Makusudio ya maneno ya Mwenyezi Mungu hapa sio matamshi yanayotokana na herufi wala si amri ya kitendo inayotokana na ibara ya ‘kuwa na kikawa,’ kwa sababu amri hii haiingii kwenye mahisabu: “Na amri haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho.” (54:51).

Isipokuwa makusudio ya maneno yake hapa, ni kuweza kuvileta vitu vyote, wakati wowote atakao; ni sawa iwe ni kwa kuviambia kuwa na vikawa au aviambie muda ujao, wa karibu au mbali. Uwezo huu hauna kikomo wala mwisho, lakini bahari, miti na mifano yake ina kikomo; na kila chenye kikomo kinakwisha.

Kwa maneno mengine ni kuwa kila kitu kilichopo kitakwisha na kukoma, isipokuwa uwezo wa Mwenyezi Mungu wa kukifanya hicho kitu utabakia.

Tutaifafanua zaidi fikra hii kwa mfano huu: Mtu akiwa na maarifa ya kilimo, maarifa yake haya atakuwa nayo tu wakati wote atakaokuwa hai, lakini kile atakochokilima kitaisha. Uweza wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hauishi kwa vile hauna kikomo ni wa milele, lakini viumbe vyake vimepatikana na kila chenye kupatikana kina mwisho.

Sema: Hakika mimi ni binadamu kama nyinyi tu, sina tofauti na nyinyi isipokuwa nimeletewa wahyi kwamba Mungu wenu ni Mungu mmoja.

Ibn Abbas anasema: “Mwenyezi Mungu, kwa Aya hii, amemfundisha Mtume wake unyenyekevu, akamwamrisha aseme yeye mwenyewe kuwa ni binadamu kama wengine, isipokuwa Mwenyezi Mungu amemtukuza kwa wahyi.”

Nasi tunaongezea kauli ya Ibn Abbas: Na ili waislamu wasimfanye Muhammad (s.a.w.) kama wanaswara (wakristo) walivyomfanya Isa (a.s.).

Mwenye kutarajia kukutana na Mola wake, kwa hisabu, thawabu na adhabu, basi na atende matendo mema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake.

Kila mwenye kufanya amali kwa ajili ya mwengine atakuwa amemshirikisha Mwenyezi Mungu kwenye ibada; ni sawa aseme waungu ni wengi au asiseme.

Tofauti ni kuwa kauli ni shirki ya waziwazi na riya ni shirki ya kificho. Kuna Hadith inayosema:

“Mwenye kuswali kwa riya amefanya shirki na mwenye kufunga kwa riya amefanya shirk”

Fananisha mengine kwenye swala na saumu.