read

Aya 49 -56: Ni Yupi Huyo Mola Wenu?

Maana

Akasema: Basi Mola wenu ni nani ewe Musa?

Musa na Harun walikwenda kwa Firauni kama walivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu, wakamwambia kuwa sisi ni mitume wa Mola wako, tumekujia na hoja na dalili kuthibitisha ukweli wetu. Basi ukiingia kwenye dini ya Mwenyezi Mungu utasalimika na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake; vinginevyo, utakuwa miongoni mwa watakaoangamia.

Hii ilikuwa mara ya kwanza Firauni kusikia neno ‘Mola wako’ kwa sababu yeye hakubali kuwa kuna mola; kama anavyodai kuwa yeye ndiye Mola Mtukufu. Ndio maana akauliza: Ni nani huyo Mola aliyekutuma kwangu?

Akasema: Mola wetu ni yule aliyekipa kila kitu umbo lake kisha akakiongoza

Musa alimjibu Firauni swali lake, kuwa Mola wetu ni yule aliyeumba viumbe akavipa sura na akazifanya nzuri sura zake bila ya kuwa na msaidizi kwenye hilo. Ndiye ambaye amekifanya kila kiumbe kibakie na hali yake. Amesema Imam Aliy (a.s.): “Je, hamuangalii kile kidogo jinsi Mungu alivyokiumba na akapingilia vizuri umbile lake, akakiumbia usikizi na uoni na akakifanyia mifupa na nyama.

Ni kama kwamba Musa anamwambia Firauni: Hakika Mola ni yule aliyeumba vitu kutokana na kutokuwa na chochote. Sasa wewe ni wapi na wapi na huyu? Ni kama ilivyomtokea Ibrahim na Namrud:

قَالَ إِبْرَاهِيمُ فَإِنَّ اللَّهَ يَأْتِي بِالشَّمْسِ مِنَ الْمَشْرِقِ فَأْتِ بِهَا مِنَ الْمَغْرِبِ فَبُهِتَ الَّذِي كَفَرَ ۗ {258}

Ibrahim akasema: Hakika Mwenyezi Mungu hulichomoza jua mashariki, basi wewe lichomoze magharibi. Akafedheheka yule aliyekufuru” Juz. 3 (2:258)

Akasema Firauni Nini hali ya karne za mwanzo?

Karne za mwanzo anakusudia watu wa Nuh, A’d, Thamud na wengineo ambao walikuwa wakiabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu. Firauni alitaka, kwa jawabu hili, kumrudi Musa, kwamba lau kungelikuwa na Mungu kwa sifa amabazo umezitaja, basi wangelimwabudu watu waliopita, na tunajua kuwa wao walikuwa wakiabudu masanamu.
Jawabu hili linajipinga lenyewe. Kwa sababu kutoa dalili ya kutokuweko Mungu kwa ibada ya masanamu, ni sawa na poponundu, na upofu wake, kupinga kuweko jua.

Akasema: Elimu yake iko kwa Mola wangu katika Kitabu. Mola wangu hapotei wala hasahau.

Musa alimjibu Firauni kuwa mimi sina ujuzi wa ghaibu mpaka nikupe habari za uma zilizopita. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye ujuzi wa kila kitu na ujuzi wake daima hauingiliwi na mabadiliko wala kugeuka:

يَوْمَ يَبْعَثُهُمُ اللَّهُ جَمِيعًا فَيُنَبِّئُهُمْ بِمَا عَمِلُوا ۚ أَحْصَاهُ اللَّهُ وَنَسُوهُ ۚ وَاللَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ {6}

“Siku atakapowafufua Mwenyezi Mungu awaambie yale waliyokuwa wakaiyatenda. Mwenyezi Mungu ameyadhibiti na wao wameyasahau. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kushuhudia kila kitu” (58:6).

Unaweza kuuliza kuwa Musa alikuwa na uhakika kuwa waabudu masanamu walikuwa katika upotevu, kwanini hakumwambia Firauni kuwa walikuwa kwenye upotevu na badala yake akamwambia Mwenyezi Mungu ndiye ajuye hali yao?

Jibu: Lau angelisema kuwa watu wa karne za kwanza walikuwa wapotevu, Firauni angelimtaka dalili ya kuwakinaisha waliopo au awe na hoja ambayo wasingeweza kuipinga na wakati huo Musa hakuwa nayo. Ndio maana akamjibu Firauni yale ambayo asingeyatakia dalili.

Ambaye amewafanyia ardhi kuwa tandiko.

Umekwishatangulia ufafanuzi wa kutandikwa ardhi na kufanywa kwake tandiko katika Juz.13 (13:3)

Na akawapitishia humo njia ya kufuatia matumizi yenu.

Na akateremsha kutoka mbinguni maji. Na kwayo tukatoa namna mbali mbali za mimea.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:99).

Kuleni na mchunge wanyama wenu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa wenye akili

Makusudio ya ishara ni dalili za kuweko Mwenyezi Mungu Mtukufu. Wenye akili ni wale wenye busara. Mwenyezi Mungu amewahusisha kuwataja hapa kwa sababu wao wanaipata haki wakiwa wamejiepusha na hawa na matamanio.

Kuna Hadith ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), kwamba yeye amesema: “Hakika wabora wenu ni wale wenye akili. Wakasema: Ninani hao wenye akili ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema ni wale wenye khulka njema, walio makini, wenye kuwapatiliza mafukara, mayatima na majirani, wanawalisha chakula na wanadhihirisha maamkuzi kwa watu”
Kutokana nayo tumewaumba na humo tumewarudisha na kutoka humo tutawatoa mara nyingine.

Mtu ni mtoto wa ardhi kwa mwili wake. Ndiyo mada ya kuumbwa kwake na humo mnatoka chakula chake na kinywaji chake na juu yake anakwenda na kurudi. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) anasema: “Ardhi ni mama yenu na ni mlezi wenu.”

Ni mama yetu kwa vile tumetokana nayo na ni mlezi wetu kwa vile inatulisha, kama anavyonyonyesha mama mtoto wake. Kisha tutarudi ardhini baada ya kufa, tuwe mchanga kama ilivyokuwa mwanzo, tena tuwe hai mara ya pili kwa ajili ya hisabu na malipo.

Hakika tulimwonyesha ishara zetu zote, lakini alikadhibisha na akakataa.

Aliyeonyeshwa ni Firauni. Makusudio ya ishara ni miujiza aliyoidhihirisha Mwenyezi Mungu mikononi mwa Musa na ikafahamisha waziwazi juu ya ukweli wa utume wake. Lakini itafaa wapi miujiza na maonyo yakigongana na masilahi na manufaa?

قَالَ أَجِئْتَنَا لِتُخْرِجَنَا مِنْ أَرْضِنَا بِسِحْرِكَ يَا مُوسَىٰ {57}

Akasema: Ewe Musa! Hivi umetujia kututoa katika nchi yetu kwa uchawi wako?

فَلَنَأْتِيَنَّكَ بِسِحْرٍ مِثْلِهِ فَاجْعَلْ بَيْنَنَا وَبَيْنَكَ مَوْعِدًا لَا نُخْلِفُهُ نَحْنُ وَلَا أَنْتَ مَكَانًا سُوًى {58}

Basi hakika tutakuletea uchawi kama huo. Basi weka miadi baina yetu na wewe ambayo hatutaivunja sisi wala wewe, mahali patakapokuwa sawa.

قَالَ مَوْعِدُكُمْ يَوْمُ الزِّينَةِ وَأَنْ يُحْشَرَ النَّاسُ ضُحًى {59}

Akasema: Miadi yenu ni siku ya sikukuu na watu wakusanywe kabla ya adhuhuri

فَتَوَلَّىٰ فِرْعَوْنُ فَجَمَعَ كَيْدَهُ ثُمَّ أَتَىٰ {60}

Basi Firauni akarudi na akatengeneza hila yake, kisha akaja.

قَالَ لَهُمْ مُوسَىٰ وَيْلَكُمْ لَا تَفْتَرُوا عَلَى اللَّهِ كَذِبًا فَيُسْحِتَكُمْ بِعَذَابٍ ۖ وَقَدْ خَابَ مَنِ افْتَرَىٰ {61}

Musa akawaambia: Ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu uwongo, asije akawafutilia mbali kwa adhabu, hakika ameshindwa mwenye kuzua.

فَتَنَازَعُوا أَمْرَهُمْ بَيْنَهُمْ وَأَسَرُّوا النَّجْوَىٰ {62}

Basi wakazozana kwa shauri yao wenyewe kwa wenyewe na wakanon’gona kwa siri.

قَالُوا إِنْ هَٰذَانِ لَسَاحِرَانِ يُرِيدَانِ أَنْ يُخْرِجَاكُمْ مِنْ أَرْضِكُمْ بِسِحْرِهِمَا وَيَذْهَبَا بِطَرِيقَتِكُمُ الْمُثْلَىٰ {63}

Wakasema: Hakika hawa wawili ni wachawi, wanataka kuwatoa katika nchi yenu kwa uchawi wao na waondoe njia yenu iliyo bora.

فَأَجْمِعُوا كَيْدَكُمْ ثُمَّ ائْتُوا صَفًّا ۚ وَقَدْ أَفْلَحَ الْيَوْمَ مَنِ اسْتَعْلَىٰ {64}

Kwa hiyo kusanyeni hila zenu zote, kisha mfike kwa kujipanga safu, na kwa hakika leo atafuzu atakayeshinda.