read

Aya 57 – 64: Firauni Anawakusanya Wachawi

Maana

Akasema: Ewe Musa! Hivi umetujia kututoa katika nchi yetu kwa uchawi wako?

Firauni aligongwa na hoja asizoweza kuzijibu alipokabiliana na Musa. Vipi ataweza kuzijibu nazo ni katika ishara za Mwenyezi Mungu? Firauni alikuwa akijua wazi kuwa Musa na Harun si wachawi na kwamba uchawi hauwezi kumtoa mtu nchini mwake na kwenye ufalme wake.

Kama wachawi wangelikuwa na uwezo huu basi wangelikuwa ndio watawala kila wakati na kila mahali. Lakini Firauni aliposhindwa kujibu mapigo, alikimbila hila, ujanja ujanja, uwongo na uzushi; sawa wanavyofanya leo wakoloni na vibaraka wao, wanapowaita wakombozi kuwa ni waharibifu na wenye nia safi kuwa ni wafanya fujo.

Basi hakika tutakuletea uchawi kama huo. Weka miadi baina yetu na wewe ambayo hatutaivunja sisi wala wewe, mahali patakapokuwa sawa.

Firauni alimtaka Musa apange siku ya mapambano baina yake na wachawi, yawe mahali palipo wazi kila mtu aweze kuona mapambano hayo na kuyafuatilia.

Akasema: Miadi yenu ni siku ya sikukuu na watu wakusanywe kabla ya adhuhuri

Musa alichagua siku ya sikukuu ndio iwe mapambano baina yake na wachawi, ambapo watu hawatakuwa na kazi waweze kukusanyika na akachaguwa wakati baina ya asubuhi na mchana, kwa vile ndio wakati mzuri wa kukusanyika watu; huku akiwa anataka kuidhihirisha haki na kuivunja batili.

Basi Firauni akarudi na akatengeneza hila yake, kisha akaja.

Aya hii pamoja na ufupi wake ina ubainifu mkubwana na inachukua maana nyingi. ‘Akarudi, akatengeneza, akaja’ Neno akarudi, linaelezea kuondoka Firauni kwenda kwa wasaidizi wake na kushauriana kupanga mipango.

Neno akatengeneza linaelezea kutuma wajumbe katika pembe zote za nchi kutafuta wachawi na kuwaleta. Mshauri wake alimshauri afanye hivyo; kama inavyoashiria Aya katika Juz. 9 (7:112). Na neno akaja, linaelezea kuja kwake na majigambo yake kwenye uwanja wa mapambano.

Musa akawaambia: Ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu uwongo, asije akawafutilia mbali kwa adhabu, hakika ameshindwa mwenye kuzua.

Musa alitanguliza nasaha na onyo kwa wachawi kabla ya kuanza kazi yoyote ya uchawi na akawahadharisha na kuondolewa mbali na adhabu kama wataendele kuwadanganya watu na kuwavunga; kisha akawafahamisha kuwa kadiri Firauni alivyo na nguvu ya utawala, lakini ni mdhaifu sana wa kuweza kuwadhuru au kuwanufaisha.

Basi wakazozana kwa shauri yao wenyewe kwa wenyewe na wakanon’gona kwa siri.

Waliozozana ni wachawi. Aya hii inaashiria kuwa baadhi ya wachawi waliathirika na maneno ya Musa au angalau waliingia shaka. Katika Tafsir Aya hii inaashiria kwamba baadhi ya wachawi waliathirika na maneno ya Musa (a.s). Au angalau yalitia shaka katika nafsi zao. Katika Attabariy imeelezwa kuwa wachawi walisema kutokana na tahadhari ya Musa kuwa maneno haya siyo ya mchawi.

Ni kweli kwamba maneno yakitoka kwenye moyo wa mwenye ikhlasi huchukua mkondo kuelekea kwenye moyo wa mwenye ikhlasi. Waliathirika baadhi ya wachawi kwa mawaidha ya Musa, wakaanza kupingana wenyewe. Kama kawaida yalipita majadiliano kuwa je, waendelee au wasiendelee.

Majadiliano haya yalipita kwa siri asisikie Musa wala Firauni. Lakini mwisho walioshinda ni wale waliong’ang’ania kuendelea na upinzani, kwa dalili ya alivyowasimulia Mwenyezi Mungu:

Wakasema: Hakika hawa wawili ni wachawi, wanataka kuwatoa katika nchi yenu kwa uchawi wao na waondoe njia yenu iliyo bora. Kwa hiyo kusanyeni hila zenu zote, kisha mfike kwa kujipanga safu, na kwa hakika leo atafuzu atakayeshinda.

Maneno yote haya ni ya wachawi na hawa wawili wanawakusudia Musa na Harun. Makusudio ya njia iliyo bora ni dini, kwa dalili ya Aya nyingine isemayo:

“Na Firauni akaema: Niacheni nimuuwe Musa naye amwite Mola wake, mimi nahofia asije kuwabadilishia dini yenu” (40:26).

Maana ni kuwa baadhi ya wachawi walisema kuwa Musa na Haruna ni mahodari katika fani ya uchawi kwa hiyo wanataka watushinde ili waimalize dini yetu wabakie wao ndio mabwana katika miji na wawatawale watu wawe watumwa wao.
Kwa hiyo basi hatuna budi tuwe na mshikamano dhidi yao na tutoe juhudi zetu zote ili tuwashinde, tuwe na cheo siku hii ya leo inayoshuhudiwa.

قَالُوا يَا مُوسَىٰ إِمَّا أَنْ تُلْقِيَ وَإِمَّا أَنْ نَكُونَ أَوَّلَ مَنْ أَلْقَىٰ {65}

Wakasema: Ewe Musa! Je, utatupa wewe au tutakuwa sisi wa kwanza kutupa?

قَالَ بَلْ أَلْقُوا ۖ فَإِذَا حِبَالُهُمْ وَعِصِيُّهُمْ يُخَيَّلُ إِلَيْهِ مِنْ سِحْرِهِمْ أَنَّهَا تَسْعَىٰ {66}

Akasema; bali tupeni nyinyi! Mara kamba zao na fimbo zao zikaonekana, kwa uchawi, kuwa zinakwenda mbio.

فَأَوْجَسَ فِي نَفْسِهِ خِيفَةً مُوسَىٰ {67}

Basi Musa akaingia hofu katika nafsi yake.

قُلْنَا لَا تَخَفْ إِنَّكَ أَنْتَ الْأَعْلَىٰ {68}

Tukasema; usihofu hakika wewe ndiye utakayeshinda.

وَأَلْقِ مَا فِي يَمِينِكَ تَلْقَفْ مَا صَنَعُوا ۖ إِنَّمَا صَنَعُوا كَيْدُ سَاحِرٍ ۖ وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُ حَيْثُ أَتَىٰ {69}

Na kitupe kilicho kuumeni kwako, kitavimeza walivyovitengeneza, hakika walivyovitengeneza ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote aendapo.

فَأُلْقِيَ السَّحَرَةُ سُجَّدًا قَالُوا آمَنَّا بِرَبِّ هَارُونَ وَمُوسَىٰ {70}

Basi wachawi wakaangushwa kusujudi. Wakasema:tumemwamini Mola wa Haruna na Musa!

قَالَ آمَنْتُمْ لَهُ قَبْلَ أَنْ آذَنَ لَكُمْ ۖ إِنَّهُ لَكَبِيرُكُمُ الَّذِي عَلَّمَكُمُ السِّحْرَ ۖ فَلَأُقَطِّعَنَّ أَيْدِيَكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ مِنْ خِلَافٍ وَلَأُصَلِّبَنَّكُمْ فِي جُذُوعِ النَّخْلِ وَلَتَعْلَمُنَّ أَيُّنَا أَشَدُّ عَذَابًا وَأَبْقَىٰ {71}

Akasema: Mumemwamini kabla sijawapa ruhusa! Hakika huyo ni mkubwa wenu aliyewafundisha uchawi. Nitawakata mikono yenu na miguu yenu kwa kubadilisha, kisha nitawasu- lubu kwenye vigogo vya mitende. Na hapo kwa yakini mtajua ni nani katika sisi ni mkali wa adhabu na kuiendeleza?

قَالُوا لَنْ نُؤْثِرَكَ عَلَىٰ مَا جَاءَنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالَّذِي فَطَرَنَا ۖ فَاقْضِ مَا أَنْتَ قَاضٍ ۖ إِنَّمَا تَقْضِي هَٰذِهِ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا {72}

Wakasema: Hatutaathirika nawe katika ishara waziwazi zilizotujia na yule aliyetuumba. Basi hukumu utakavyohukumu; kwani wewe unahukumu maisha haya ya duniani tu

إِنَّا آمَنَّا بِرَبِّنَا لِيَغْفِرَ لَنَا خَطَايَانَا وَمَا أَكْرَهْتَنَا عَلَيْهِ مِنَ السِّحْرِ ۗ وَاللَّهُ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ {73}

Hakika sisi tumemwamini Mola wetu ili atusamehe makosa yetu na uchawi uliotulazimisha kuufanya na Mwenyezi Mungu ndiye Mbora na mwenye kudumu zaidi.

إِنَّهُ مَنْ يَأْتِ رَبَّهُ مُجْرِمًا فَإِنَّ لَهُ جَهَنَّمَ لَا يَمُوتُ فِيهَا وَلَا يَحْيَىٰ {74}

Hakika atakayemjia Mola wake naye ni mhalifu, basi kwa hakika yake ni Jahannamu. Hafi humo wala haishi.

وَمَنْ يَأْتِهِ مُؤْمِنًا قَدْ عَمِلَ الصَّالِحَاتِ فَأُولَٰئِكَ لَهُمُ الدَّرَجَاتُ الْعُلَىٰ {75}

Na atakayemjia naye ni mumin aliyetenda mema basi hao ndio wenye daraja za juu

جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَذَٰلِكَ جَزَاءُ مَنْ تَزَكَّىٰ {76}

Bustani za milele zipitazo mito chini yake, watadumu humo milele na hayo ni malipo ya mwenye kujitakasa