Aya 99 – 112: Kama Hivyo Tunakusimulia
Maana
Namna hivi tunakuhadithia katika habari za yaliotangulia.
Mwenyezi Mungu anaashiria kisa cha Musa (a.s.) na habari zake. Maneno hayo anaambiwa Muhammad (s.a.w.). Neno ‘katika’ ni kuelezea baadhi; yaani tunakusimulia baadhi ya habari za umma uliotangulia, kama ulivyosikia. Nazo ni mazingatio na mawaidha kwa watu. Wakati huo huo zinafahamisha ukweli wako na utume wako. Kwa sababu ni habari za ghaibu.
Na hakika tumekuletea kutoka kwetu mawaidha.
Makusudio ya mawaidha hapa ni Qur’an. Imeitwa hivyo kwa sababu ndani yake kuna utajo wa Mwenyezi Mungu na sifa zake, mitume na habari zao, akhera na mambo yake, imani na ukafiri, kheri na shari, halali na haramu, kuumbwa mbingu na ardhi na mengineyo.
Atakayejitenga nayo basi hakika siku ya Kiyama atabeba mzigo.
Kila mwenye kuipinga Qur’an kwa kauli na vitendo au kwa vitendo bila ya kauli, basi atakuwa amejitenga nayo na atakuwa ameibebesha nafsi yake mzigo mzito. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema: “Hakuiamini Qur’an yule anayehalalisha yaliyo haramu.” Yatakuja maelezo zaidi kwenye Aya ya 124 ya Sura hii, inshaallah.
Watadumu humo.
Yaani humo mwenye mizigo. Adhabu kuiita mizigo ni katika kutumia sababu kwa msabibishi.
Ni mzigo muovu kwao kuubeba siku ya Kiyama!
Yaani mzigo wa madhambi walioubebesha nafsi zao kwa sababu ya kujtenga kwao na Qur’an.
Siku itakayopulizwa parapanda.
Hiki ni kinaya cha kufufuliwa walioko makaburini.
Na tutawakusanya wahalifu siku hiyo wakiwa buluu.
Hii pia ni kinaya cha kufazaika kwao na hali mbaya watakayokuwa nayo. Ya kushangaza ni yale niliyoyasoma katika Tafsir Al-Bahru-Muhit ya Abu Hayan Al-Andalusi, akisema: “Makusudio ya ubuluu ni ubuluu wa macho, na macho ya buluu yanachukiza sana kwa waarabu kwa sababu maadui zao waroma wana macho ya buluu.” Mfasiri huyu alikuwa karibu na wakati wa vita vya msalaba (Crusade).
Watanong’onezana wao kwa wao: ‘Hamkukaa ila siku kumi tu.’
Miongoni mwa sifa za wahalifu siku ya Kiyama nikuwa wao kutokana na vituko watakavyopambana navyo, watasahau muda wa kukaa kwao katika maisha ya dunia.
Kwa hiyo wataambiana kwa lugha ya maneno au kwa lugha ya hali kwa sauti ya chini: Hatukukaa ispokuwa siku kumi au masaa kadhaa au kitambo kidogo tu.
Unaweza kuuliza: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) katika Aya hii, amewazungumzia kuwa watasema tumekaa siku kumi, katika Sura Kahf, Aya 19 amesema, siku moja au sehemu ya siku; na katika Sura Rum, Aya 55, watasema kuwa hawakukaa ispokuwa saa moja. Je, kuna wajihi gani wa kuchanganya Aya zote hizo?
Razi amejibu kuwa baadhi ya wahalifu wataona ni siku moja wengine kumi. Tuonavyo sisi ni kuwa neno kumi, siku au saa katika Aya sio kuzungumzia kauli halisi ya wahalifu; ispokuwa ni kinaya cha vile watakavyowazia uchache wa muda na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hayo ameyaletea ibara ya kumi, mara nyingine siku na hata saa. Mwenyezi Mungu ameyaashiria haya kwa kauli yake: “Siku atakayowaita nanyi mkamwitikia kwa kumsifu. Na mkadhani kuwa hamkukaa ila muda mchache tu.” Juz.15 (17:52).
Sisi tunayajua zaidi watakayoyasema, atakaposema mbora wao kwa mwendo: ‘Nyinyi hamkukaa ila siku moja tu.’
Mbora wao kwa mwendo ni yule mwenye sera nzuri na mwenye kujua hakika ya mambo. Maana ni kuwa wakati wanapoambiana kuwa tumekaa siku kumi tu, huyo mbora wao atawaambia: Maisha mliyokuwa nayo mkishindana, si chochote ispokuwa ni kama ndoto tu, hayawezi kuhisabiwa kwa wakati wala kwa siku. Maisha ya uhakika hasa ni haya tuliyo nayo hivi sasa, ambayo hayana muda wala mwisho.
Wanakuuliza kuhusu milima. Sema: Mola wangu ataivurugavuruga. Ataiwacha tambarare iliyo sawasawa. Hutaona humo mabonde wala miinuko.
Muulizaji alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kuwa vipi milima itakavyokuwa siku ya kiyama? Mwenyezi Mungu akamwambia mtume wake Mtukufu: mjibu Aliyeuliza sawali hili kuwa Mwenyezi Mungu ataing’oa na ataigeuza kuwa ni mavumbi yatakayotawanyika angani na pale ilipokuwa patakuwa tambarare bila ya mabonde wala miinuko.
Siku hiyo watamfuata muitaji asiye na upotofu.
Siku hiyo ni siku ya Kiyama, watakofuata ni viumbe na muitaji ni yule atakayewaita viumbe kwenye mkusanyiko, hisabu na malipo. Maana ni kuwa mwito utakuwa wa haki na utaitikiwa na wote, hakuna atakayeweza kuuhalifu: “Siku atakapoita muitaji kuliendea jambo linalochusha; macho yao yatainama; watatoka makaburini kama nzige waliotawanyika; wanamkimbilia muitaji na makafiri watasema: ‘Hii ni siku ngumu.’ (54: 6-9).
Na sauti zote zitamnyenyekea Mwingi wa rehma. Basi hutasikia ila mnong’ono.
Makusudio ya sauti ni wenye sauti hizo. Na mnong’ono unafahamisha unyenyekevu.
Siku hiyo uombezi hautafaa ila wa aliyemruhusu Mwingi wa rehema na akamridhia kusema.
Hii iko katika maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Wala hawaombei ila yule Aliemridhia” (21:28). Tumeazungumzia shafaa kwa urefu katika Juz. 1 (2:97).
Anayajua yalio mbele yao na yalio nyuma yao wala wao hawawezi kumjua Yeye vilivyo.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (2:255).
Zitanyenyenyekea nyuso kwa Aliye hai, Mwangalizi Mkuu.
Makusudio ya nyuso ni walio na nyuso hizo. Maana ni kuwa viumbe wote kesho watasalimu amri mbele ya Aliye hai, asiyekufa na Msimamizi wa kila jambo wala hakuna kinachosimamiwa ila kwa ajili yake.
Na hakika ameharibikiwa mwenye kubeba dhulma.
Mwenye hasara zaidi katika watu kesho ni yule mwenye kuwadhulumu watu na akaingilia heshima na uhuru wao. Na mwenye faida mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule mwenye kufanya kwa ajili ya kheri ya binadamu na masilahi kwa njia ya kheri na ya ubinadamu.
Na mwenye kutenda mema naye ni mumin, hatahofu dhulma wala kupunjwa.
Hii ni sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni mumin tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya.” Juz. 14 (16: 97).
وَكَذَٰلِكَ أَنْزَلْنَاهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا وَصَرَّفْنَا فِيهِ مِنَ الْوَعِيدِ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ أَوْ يُحْدِثُ لَهُمْ ذِكْرًا {113}
فَتَعَالَى اللَّهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ ۗ وَلَا تَعْجَلْ بِالْقُرْآنِ مِنْ قَبْلِ أَنْ يُقْضَىٰ إِلَيْكَ وَحْيُهُ ۖ وَقُلْ رَبِّ زِدْنِي عِلْمًا {114}
وَلَقَدْ عَهِدْنَا إِلَىٰ آدَمَ مِنْ قَبْلُ فَنَسِيَ وَلَمْ نَجِدْ لَهُ عَزْمًا {115}
وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ {116}
فَقُلْنَا يَا آدَمُ إِنَّ هَٰذَا عَدُوٌّ لَكَ وَلِزَوْجِكَ فَلَا يُخْرِجَنَّكُمَا مِنَ الْجَنَّةِ فَتَشْقَىٰ {117}
إِنَّ لَكَ أَلَّا تَجُوعَ فِيهَا وَلَا تَعْرَىٰ {118}
وَأَنَّكَ لَا تَظْمَأُ فِيهَا وَلَا تَضْحَىٰ {119}
فَوَسْوَسَ إِلَيْهِ الشَّيْطَانُ قَالَ يَا آدَمُ هَلْ أَدُلُّكَ عَلَىٰ شَجَرَةِ الْخُلْدِ وَمُلْكٍ لَا يَبْلَىٰ {120}
فَأَكَلَا مِنْهَا فَبَدَتْ لَهُمَا سَوْآتُهُمَا وَطَفِقَا يَخْصِفَانِ عَلَيْهِمَا مِنْ وَرَقِ الْجَنَّةِ ۚ وَعَصَىٰ آدَمُ رَبَّهُ فَغَوَىٰ {121}
ثُمَّ اجْتَبَاهُ رَبُّهُ فَتَابَ عَلَيْهِ وَهَدَىٰ {122}