Aya 133 – 135: Kwa Nini Hakuletea Ishara
Maana
Na walisema: Kwa nini hakutuletea ishara kutoka kwa Mola wake?
Umetangulia mfano wa Aya hii pamoja na tafsiri yake katika Juz. 1 (2:118). Juz. 7 (6:37) na Juz. 11 (10:20).
Je, haikuwajia dalili wazi ya yaliyomo katika vitabu vya mwanzo?
Ikiwa mnataka muujiza kweli enyi washirikina na wala sio kwa inadi, basi hii hapa Qur’an. Kwani hakika hiyo ni muujiza wa miujiza kwa namna kadhaa; miongoni mwazo ni kuwa inabainisha walioyaleta mitume na vitabu vilivyoshuka. Hapana; nyinyi hamtafuti uhakika na uongofu, wala nyinyi si watu wa kweli na wa kheri. Haya mnayoyataka ni kwa ajili ya inadi, ubabaishaji na kuvunga.
Na lau tungeliwaangamiza kwa adhabu kabla yake, wangelisema: Ewe Mola wetu! Kwa nini usituletee mtume tukazifuata ishara zako kabla hatujadhalilika na tukahizika?
Hao ni washirikina na kabla yake ni kabla ya Mtume au kabla ya Qur’an. Maana ni kuwa lau tungeliwaadhibu washirikina duniani au akhera bila ya kuwapa hoja ya kumtuma Muhammad na kuteremsha Qur’an, wangelileta hoja na kumwambia Mwenyezi Mungu: Mbona unatuadhibu kabla ya kutuletea Mtume wa kututoa kwenye ujinga na kutuzindua kwenye mghafala huu na kutuamrisha lile unalolipenda na kutukataza unalolichukia?
Lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekata nyudhuru zote baada ya kumtuma Muhammad (s.a.w) kwa ishara zilizo waziwazi.
Sema: Kila mmoja anangoja; basi ngojeni punde mtajua nani mwenye njia sawa na nani aliyeongoka.
Hili ni onyo kwamba wao wanafuata njia ya upotevu na ya maangamizi, makemeo na kiaga cha adhabu inayowangoja, lakini maonyo hayawafai watu wasioamini isipokuwa chumo lao na manufaa yao.