Utangulizi
Amesema Allah Mtukufu: “Na sikuumba majini na watu ila wapate kuniabudu.”1
Ustaarabu wa Kiislamu umetokana na mafunzo mazuri ya dini ya Kiislamu na umesaidia kuratibu maswala ya dini na dunia, hivyo Uislamu ni dini ya imani na sharia. Ni dini ya maendeleo na mafanikio kwa kila aina zake.
Mizizi Ya Dini:
Dini ni mkusanyiko wa imani na majukumu ya kivitendo yaliyoletwa na Manabii kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili kuwaelekeza na kuwaongoza wanadamu. Hivyo nafsi kujengeka katika msingi wa imani hizi huku ikitekeleza majukumu haya ya kivitendo ndiyo sababu ya mwanadamu kufanikiwa kwa wema ndani ya maisha haya ya Dunia na Akhera, hivyo mizizi hiyo ya dini ni mitano:
I. Tawhidi:
Ni kuamini kuwa ulimwengu una Mungu aliyeuumba na kuufanya uwepo baada ya kuwa haukuwapo, na kwamba huyo Muumba wa ulimwengu ni Mmoja Mpekee asiyekuwa na mshirika.
II.Uadilifu:
Ni kuamini kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mwadilifu, hamdhulumu yeyote, na kwamba matendo Yake yana hekima, hivyo, hatendi chochote isipokuwa kina masilahi kwa viumbe.
III. Utume:
Ni kuamini kuwa Mwenyezi Mungu hawaachi viumbe wake bila mwongozo, hivyo aliwatuma manabii ili wawaite watu kwenye njia iliyonyooka. Na Nabii wa kwanza ni Nabii Adam (a.s) na wa mwisho ni Nabii Muhammad (s.a.w.w), na kwamba dini ikubaliwayo kwa Mwenyezi Mungu ni Uislamu na ndio dini kamili.
IV. Uimamu:
Ni kuamini kuwa, kama ambavyo Mwenyezi Mungu aliteua Manabii na mitume, vivyo hivyo aliteua warithi wa Mitume yake. Ili kuendeleza kazi ya unabii wa bwana wetu Muhammad (s.a.w.w.) aliwateua Maimamu, warithi na Makhalifa kumi na wawili, wa kwanza wao ni Ali bin Abi Twalib (a.s) na wa mwisho ni Imam Al-Mahdi (a.t.f.s).
V. Marejeo:
Ni kuamini kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu atawafufua watu baada ya kifo ili kumlipa mtiifu kwa wema na kumwadhibu aliyeasi, ili awape malipo ya kudumu.
Matawi Ya Dini:
Ni hukumu alizoziweka Allah Mtukufu kupitia Qur’an na Sunna tukufu kwa masilahi ya waja wake, na ambazo Mtume (s.a.w.w.) ametulingania kuzifuata, na akatuamuru kuzitekeleza, zikiwa na lengo la kuzitoharisha nafsi na kuimarisha utumishi wake kwa Allah Mtukufu. Matawi ya dini yaliyo muhimu zaidi ni:
1. Swala
2. Saumu
3. Zaka
4. Hijja
5. Khumsi
6. Jihadi
7. Kuamrisha mema na kukataza maovu
8. Kumtawalisha Mtume (s.a.w.w.) na Ahlul-Bayti wake watoharifu (a.s) na kujiepusha na adui zao.
- 1. Sura Adh-Dhariyyat: 51.