read

Udhu

Mwenyezi Mungu amesema: “Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swala, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu na miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba, basi ogeni. Na mkiwa wagonjwa au safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmeingiliana na wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni mchanga ulio safi na mpake nyuso zenu na mikono yenu Mwenyezi Mungu hapendi kukutieni katika taabu, lakini anataka kukutakaseni na kutimiza neema Yake juu yenu ili mpate kushukuru.”1

Ni Wakati Gani Tunawajibika Kisharia Kuwa Na Udhu?

i. Ni lazima kuchukua udhu kwa ajili ya kila Swala ya faradhi au ya sunna isipokuwa sala ya kumsalia maiti, kwani si lazima kuchukuwa udhu kwa ajili yake.

ii. Kwa ajili ya kuizunguka Al-Kaaba wakati wa ibada ya Hijja na Umra.

iii. Kwa ajili ya kugusa maandishi ya Qur’an Tukufu.

Masharti Ya Kusihi Kwa Udhu

i. Nia ya kujikurubisha kwa Allah Mtukufu

ii. Maji yawe tohara

iii. Yawe maji halisia: Yaani yasiwe maji ya matunda au yaliyokamuliwa toka kwenye mmea wowote ule (Kama vile maji ya waridi), au yaliyochanganywa na mada yoyote ile (kama vile maji ya sabuni, maji ya iriki au soda).

iv. Yawe maji ya halali: Yaani yasiwe maji ya wizi, na unyang’anyi au yatokanayo na kipato kisicho cha halali kisharia.

v. Chombo cha udhu kiwe cha halali: Yaani kisiwe cha wizi na unyang’anyi au kitokanacho na kipato kisicho cha halali kisharia.

vi. Chombo cha kufanyia udhu kisiwe cha dhahabu au fedha. vii. Viungo vya udhu viwe tohara.

vii. Kuwepo na muda utoshao kufanya udhu na kusali.

viii. Utaratibu baina ya viungo vya udhu: Yaani aoshe uso kwanza kisha mkono wa kulia na kisha wa kushoto, na baada ya hapo apake kichwa na kisha miguu yake miwili.

ix. Mfululizo baina ya viungo vya udhu: Yaani wakati wa kuchukua udhu asipitishe muda mrefu kabla ya kwenda kiungo kingine kwa kiasi ambacho itapelekea kukauka kwa viungo vya mwanzo kabla ya udhu kukamilika.

x. Atende matendo ya udhu yeye mwenyewe, na wala mtu mwingine asimfanyie udhu, isipokuwa katika hali ya dharura. (Hii ina maana kwamba, kama ukimwambia mtu akuoshe uso na mikono n.k. udhu wako utabatilika; lakini kama huwezi kufanya udhu mwenyewe kwa sababu za ugonjwa unaweza kuomba msaada kwa mtu mwingine).

xi. Lisiwepo tatizo au hatari yoyote ile iwezayo kutokea kutokana na kutumia maji, kama vile maradhi, hofu ya kiu, au kuihofia nafsi yake au nafsi yenye kuheshimika.

xii. Kisiwepo kizuizi chochote katika viungo vya udhu kinachoweza kuzuia maji kugusa ngozi, kama vile mafuta na rangi.

xiii. Kichwa na miguu viwe vikavu kabla ya kupaka maji.

  • 1. Sura Al-Maidah: 6.