Swala Ya Tahdhari (Ihtiyatwi):
i. Swala hii husaliwa ili kufidia upungufu unaodhaniwa katika idadi ya rakaa za Sala baada ya kuwa na shaka na idadi ya rakaa hizo.
ii. Ni lazima isaliwe mara tu baada ya kumaliza kusali na kabla ya kufanya mambo yabatilishayo Sala, kama vile kuzungumza na kugeuka kulia na kushoto kutoka uelekeo wa kibla.
iii. Ni lazima masharti ya Sala yakamilike ndani yake.
Namna Ya Kuisali:
Ni lazima iwepo nia, Takbira ya kuhirimia, kusoma sura Alhamdu pekee kimyakimya bila kudhihirisha sauti hata Bismillah, vilevile ni lazima kufanya rukuu, sijda mbili, tashahhud na kutoa salam, sawasawa iwe rakaa moja au mbili.
Ni Wakati Gani Tunasujudu Sijda Mbili Za Usahaulifu?:
Sijda mbili za usahaulifu huwa wajibu kwa mtu anayesali ikiwa atatokewa na moja ya mambo yafuatayo:
i. Kuzungumza katika sala kwa kusahau.
ii. Kusahau sijda moja inapopita mahali pa kuifanya.
iii. Kuacha kusoma tashahhud kwa kusahau.
iv. Kutoa salam mahali ambapo sio pa kutoa salam.
v. Kutilia shaka kati ya rakaa ya nne na ya tano akiwa katika hali ya kukaa.
Mas’ala Mbalimbali Kuhusu Sijda Mbili Za Usahaulifu:
i. Sijda mbili ni wajibu mara tu baada ya sala.
ii. Nia ni lazima katika sijda mbili za usahaulifu.
iii. Ni sunna kusoma Takbira ya kuhirimia.
iv. Hakuna rukuu katika sijda mbili za usahaulifu.
Namna Ya Kufanya Sijda Mbili Za Usahaulifu:
Zenyewe ni sijda mbili zinazosaliwa kwa kukaa, ni lazima azifanye mara tu baada ya kumaliza sala na kabla ya kufanya mambo ya nje ya sala, tena kwa kufuata utaratibu ufuatao:
a. Nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.
b. Ni sunna kusoma Takbira ya kuhirimia.
c. Kusujudu: Ni sunna kusoma maneno yafuatayo:
بسْمِ الله وَبالله السَلَامَُ عَليْكَ أيَّهَا النَبيُ وَرَحْمَهُ الله وَبَرْ كَا تُهُ
d. Kukaa katika hali ya utulivu.
e. Kusujudu mara ya pili kama awali.
f. Baada ya sijda mbili ni lazima kusoma tashahhud na kutoa salam moja kwa kusema:
الحَمْدُ لِلَه أشْهَدُ أنْ لَاإلهَ إّلَا الله وَحْدَ ةُ لَا شَرِيْكَ لَهُ وَ أشْهَدُ أنَّ مُحَمَّدَا عَبْدُةُ وَرَسُوْلُهُ.
اللهم صَلَّ عَلَي مُحَمَّدٍ وَاَلِ مُحَمَّدٍ. السَلَامُ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَهُ الله وَبَرْ كَاتُهُ.
Shaka Zinazobatilisha Sala:
i. Shaka kuhusu idadi ya rakaa za sala yenye rakaa mbili na tatu, pia shaka kuhusu rakaa mbili za mwanzo wa sala yenye rakaa nne kabla ya kakamilisha sajda mbili katika rakaa ya pili.
ii. Shaka kati ya rakaa ya pili na ya tano na kuendelea.
iii. Shaka kati ya rakaa ya tatu na ya sita na kuendelea.
iv. Shaka kati ya rakaa ya nne na ya sita na kuendelea.
Shaka Zenye Kupuuzwa:
i. Shaka katika utekelezaji wa kifungu miongoni mwa vifungu vya sala baada ya kuwa umepita mahali pake.
ii. Shaka baada ya kutoa salam.
iii. Shaka ya mtu mwenye hali ya kushakiashakia.
iv. Shaka ya Imamu au maamuma kuhusu idadi ya rakaa. Katika hali hii Imamu anaweza kuwa na uhakika wa kusali kwake na Maamuma akawa na shaka, au Maamuma akawa na uhakika lakini Imamu akawa na shaka. Katika hali hii yule mwenye shaka amfuate yule mwenye uhakika.
v. Shaka katika Sala ya Sunna. Kwani anaweza kufuata moja ya pande mbili za shaka na akakamilisha Sala yake.