Aya 12 -17: Kuumbwa Mtu Na Mbingu
Mwenyezi Mungu Na Mtu
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameashiria kwenye Aya nyingi kuhusu kuumbwa mtu; sio kwa kuwa tujue tumetoka wapi, tumepatikana vipi na tuko vipi tu, iwe ni basi. Hapana! Bali ni tuuatumbue ukuu wa muumbaji katika kutuumba kwetu, kama tunavyoutambua katika kuumba mbingu na ardhi.
Tunapaswa tumwamini na tuende na mwongozo wake kwa kutumai kupata thawabu zake na kuepukana na adhabu yake.
Miongoni mwa Aya hizo ni ile isemayo:
هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنْسَانِ حِينٌ مِنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُنْ شَيْئًا مَذْكُورًا {1}
Ndio! Hakuwa kitu kinachotajwa kisha akawa kitu. Ama yule ambaye amemfanya aweko kutoka asikokuwako, anatutanabahisha pale aliposema:
'Na hakika tumemuumba mtu kutokana na asili ya udongo.'
Katika Aya hii Mwenyezi Mungu Mtukufu ameonyesha chimbuko la mtu, vipi alivyomgurisha kutoka hali moja hadi nyingine. Lengo la kwanza katika hilo ni kujua dalili za kuweko muumba na utukufu wake, tufikirie na tumwangalie kiumbe huyu wa ajabu katika sura yake, umbile lake, akili yake na utambuzi wake.
Mtu huyu Mwenye historia na maendeleo, kiumbe huyu ambaye ana nguvu na uwezo kuliko kiumbe yeyote mwengine, ambaye wajuzi wameileza taadhima yake hii kwa neno: "Na kwako wewe umekunjwa ulimwengu mkubwa," ametokea wapi na ameumbwa kutokana na nini?
Aya inatujibu kwamba yeye ameumbwa kutokana na udongo uliotokana na mchanga na maji, katika asili ambayo imeumbiwa wadudu na mimea. Hapa ndio pana dalili na hoja. Kwani inavyojulikana ni kuwa kitu kimoja hakiwezi kutoa vitu viwili vinavyopingana, utambuzi na kutotambua; upofu na kuona. Kwa hiyo hapa kuna siri wala hakuna tafsiri ya siri hii isipokuwa kwa nguvu yenye uwezo na yenye ujuzi wa kitu hicho.
Ni nguvu hii ambayo imefarikisha na kupamabanua baina ya vitu viwili vinavyopingana ambavyo vimeumbwa kwa asili moja. Baada ya kuashiria malengo ya Aya zinazozungumzia kuumbwa kwa mtu, sasa tunabainisha makusudio ya Aya tulizonazo.
Na hakika tumemuumba mtu kutokana na asili ya udongo.
Makusudio ya mtu hapa ni mwanadamu, sio Adam mwenyewe. Kauli yake Mwenyezi Mungu inayofuatia: 'Kisha tukamjaalia awe tone' inafahamisha hivyo. Adamu na wanawe wote wanatokana na udongo uliotokana na mchanga na maji. Tofauti ni kuwa Adam ameumbwa kutokana na mchanga na maji, moja kwa moja; na wanawe ni kupitia chakula kinachozalikana kutokana na ardhi na maji.
Kisha tukamjaalia awe tone katika makao yaliyo makini katika uti wa mgongo wa baba hadi kwenye mfuko wa uzazi wa mama.
Kisha tukaumba tone kuwa pande la damu na tukaliumba pande la damu kuwa pande la nyama.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (22:5).
Na pande la nyama tukaliumba kuwa mifupa na mifupa tukaivika nyama.
Pande la nyama akaligawanya mifupa, mishipa na nyama, kisha kwenye mkusanyiko huo akaumba aina mbali mbali. Ufafanuzi uko katika elimu ya upasuaji.
Kisha tukamfanya kiumbe mwengine mtu aliye kamili kama siye yule aliyekuwa tone damu nyama n.k.
Basi ametukuka Mwenyezi Mungu mbora wa waumbaji.
Wala hakuna kitu kinachofahamisha hakika hii kuliko kuumbwa ulimwengu na nidhamu yake na kuumbwa mtu na ubainifu wake, moyo wake, akili yake n.k. Tunakariri tuliyoyasema mara kwa mara, kwamba imekuwa ni desturi ya Qur'an Tukufu kutegemeza mabadiliko ya ulimwengu kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu Yeye, ambaye umetukuka utukufu wake, ndiye sababu ya kuumbwa ulimwengu.
Kisha hakika nyinyi baada ya hayo ni maiti.
Na anayekufa marejeo yake ni kwa muumba wake.
Kisha hakika nyinyi siku ya Kiyama mtafufuliwa muulizwe mliyokuwa mkiyafanya.
Maana Ya Mbingu Saba
Hakika tumeumba juu yenu tabaka saba. Nasi katika kuumba si wenye kughafilika.
Wakati wa kufasiri Juz. 1 (2: 29), nilisema kuwa kutajwa mbingu saba hakufahamishi kuwa ni hizo hizo tu, na kwamba sababu ya kutajwa kwake huenda ikawa ni kwa mambo yanayohusika hapo. Nilitosheka na kauli hiyo wakati huo, kwa sababu mimi si mjuzi zaidi wa hilo, kwani si mtaalamu wa elimu ya falaki.
Nilipofikia kufasiri Aya hii tuliyo nayo nikasoma makala ya kisayansi katika jarida la Misr liitwalo Akhbar la tarehe 17 Julai 1969, yenye kichwa cha maneno 'Mwenyezi Mungu na mtu na mwezi,' kama ifutavyo:-
"Imethibitishwa kisayansi kwamba katika anga za mbali kuna aina za ulimwengu zaidi ya ulimwengu huu tunaoishi - yaani mkusanyiko wa sayari tunazoziona kwa macho makavu au kwa darubini - na kwamba kila ulimwengu katika aina hizo una jua lililo na nguvu zaidi ya hili jua letu linaongaza kila siku kwenye ardhi; na pembezoni mwake kunazunguka nyota kadhaa.
Haiwezekani kufikia kwenye sayari yoyote katika sayari hizo pamoja na kwamba tuna vyombo vilivyoweza kugundua sehemu hizo, kutokana na umbali wa kasi ya mwanga kufikia huko. Jua na nyota za sehemu hizo ziko mbali nasi kwa mwendo wa kasi ya mwanga ya mamilioni ya miaka. Lau kama tutakadiria mtu kusafiri kufikia huko, basi itamchukua mamilioni ya miaka kwa kasi ya mwanga kuweza kuifikia sayari iliyo karibu zaidi ya ulimwengu huo. Hii ndio hakika iliyothibitishwa na sayansi na wamekubaliana nayo wataalam wa kisasa."
Kwa hiyo basi makusudio ya mbingu saba ni ulimwengu (dunia) wa aina saba na sio sayari saba, kwamba kila ulimwengu una sayari na nyota zake zisizokuwa na idadi na kwamba mtu hawezi kuzifikia kwa sababu hawezi kuishi mamiloni ya miaka. Ama ardhi saba zilizoashiriwa katika (65:12) ni kuwa katika ulimwengu huo wa aina saba kila mmoja una sayari ya ardhi.
وَأَنْزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً بِقَدَرٍ فَأَسْكَنَّاهُ فِي الْأَرْضِ ۖ وَإِنَّا عَلَىٰ ذَهَابٍ بِهِ لَقَادِرُونَ {18}
فَأَنْشَأْنَا لَكُمْ بِهِ جَنَّاتٍ مِنْ نَخِيلٍ وَأَعْنَابٍ لَكُمْ فِيهَا فَوَاكِهُ كَثِيرَةٌ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ {19}
وَشَجَرَةً تَخْرُجُ مِنْ طُورِ سَيْنَاءَ تَنْبُتُ بِالدُّهْنِ وَصِبْغٍ لِلْآكِلِينَ {20}
وَإِنَّ لَكُمْ فِي الْأَنْعَامِ لَعِبْرَةً ۖ نُسْقِيكُمْ مِمَّا فِي بُطُونِهَا وَلَكُمْ فِيهَا مَنَافِعُ كَثِيرَةٌ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ {21}
وَعَلَيْهَا وَعَلَى الْفُلْكِ تُحْمَلُونَ {22}