Aya 51 – 56: Mola Mmoja Na Dini Moja
Maana
Katika Juz. 2 (2:172) Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawaambia waumini: "Kuleni vizuri tulivyowaruzuku na mumshukuru Mwenyezi Mungu." Katika Aya hii anawaambia Mitume: Kuleni katika vitu vizuri na fanyeni mema. Hakika mimi ni Mjuzi wa mnayoyatenda.
Lengo la kauli zote hizo ni kubainisha kuwa dini ya haki ni takua na matendo mema sio kujinyima raha. Kila utakalolifurahia na kuburudika nalo basi hilo ni jema mbele ya Mwenyezi Mungu, ikiwa hakulikataza; sawa na lilivyo jema kwako. Kuna Hadith isemayo: "Hakika Mwenyezi Mungu ni Mzuri na hupenda uzuri."
Na kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alikuwa akivaa kila ali- chokimudu katika sufu, pamba (cotton) na vitambaa vinginevyo. Hakuwa akikataa vitu vizuri, lakini hakujikalifisha navyo.
Alikuwa akila haluwa na asali na akizipenda. Akila nyama ya ngamia, kondoo na kuku. Pia alikuwa akila matango na maboga kwa tende mbichi, na akipenda kula tende kwa siagi, mkate kwa nyama na maini ya kuchoma na mkate wa kuchanganywa na mchuzi.
Kwa ujumla Mtume (s.a.w.) alikuwa akila na kuvaa kile anachokimudu, akikosa huvumilia na kuwa na subira. Na kitu kizuri zaidi ni kula kwa jasho. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) anasema: "Ni katika uzuri zaidi mtu kula kutokana na chumo lake."
Na hakika umma wenu huu ni umma mmoja na mimi ni Mola wenu, basi nicheni.
Neno umma lina maana nyingi; miongoni mwazo ni hizi:-
1. Kundi la watu: Kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Ingieni motoni pamoja na umma zilizopita." Juz. 8 (7:38).
2. Muda: Mwenyezi Mungu anasema: "Na akakumbuka baada ya muda." Juz. 12 (12:45).
Neno muda limefasiriwa kutokana na neno umma.
3. Mila: Kama ilivyo katika Aya hii tuliyo nayo.
Aya hii inaashiria mila za Mitume wote. Msemo katika neno umma wenu, unaelekezwa kwa watu wote, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu iliyokuja moja kwa moja 'lakini walikatiana jambo lao ...' ambapo maana ni kwa nini watu wanachukiana na kuwa vikundi mbali mbali, kukawa na kikundi cha Musa, cha Isa na cha Muhammad na hali Mungu wao ni mmoja, dini yao ni moja na lengo lao ni moja? Kuna Hadith isemayo: "Mitume wote ni ndugu, mama zao ni mbali mbali na dini yao ni moja."
Unaweza kuuliza, kwanini sharia za mitume ni tofauti na dini yao ni moja? Jibu: Kutofautiana sharia hakusababishi kutofautiana dini maadamu msingi ni mmoja; kwa mfano serikali za kikiristo zinatofautiana kikanuni na kisheria, lakini zinakuwa pamoja kiitikadi na kidini.
Lakini walikatiana jambo lao kwa vitabu mbali mbali. Kila kundi linafurahia kwa waliyo nayo.
Hapa wanazungumziwa wafuasi wa Mitume; yaani mitume wako kwenye dini moja, lakini wafuasi wao wako kwenye dini mbali mbali. Kila kundi likafuata Kitabu wanachokiamini na kukikana kingine. Mayahudi waliamini Tawrat baada ya kuipotoa na kuikana Injil na Qur'an. Wanaswara nao waliipotoa Injil na wakiamini pamoja na Tawrt iliyopotolewa na wakaikana Qur'an.
Tazama tuliyoyaandika kwa anuani ya 'Kila mmoja avutia dini yake' Juz. 1 (2: 111-113).
Basi waache katika upotevu wao kwa muda.
Baada ya Mtume (s.a.w.) kuwafikishia risala ya Mola wake na akawaondolea nyudhuru zote kwa jinsi alivyowahadharisha, Mwenyezi Mungu alimwamrisha kuachana nao na awaache na upotevu wao.
Hili ni karipio na kiaga kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyokuja moja kwa moja Je wanadhani kuwa vile tunavyowapa mali na watoto ndio tunawahimizia kheri? Lakini hawatambui.
Wamedanganyika na watoto na mali wakadhani kuwa watadumu nazo, lakini hakujua kuwa Mungu amewawekea muda maalum, kisha awanyakue kwa mnyakuo wa Mwenye nguvu na ushindi.
إِنَّ الَّذِينَ هُمْ مِنْ خَشْيَةِ رَبِّهِمْ مُشْفِقُونَ {57}
وَالَّذِينَ هُمْ بِآيَاتِ رَبِّهِمْ يُؤْمِنُونَ {58}
وَالَّذِينَ هُمْ بِرَبِّهِمْ لَا يُشْرِكُونَ {59}
وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوْا وَقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَىٰ رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ {60}
أُولَٰئِكَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ {61}
وَلَا نُكَلِّفُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۖ وَلَدَيْنَا كِتَابٌ يَنْطِقُ بِالْحَقِّ ۚ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ {62}